Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
SERIKALI imeazimia kuzindua Chaneli ya Utalii inayotegemewa kurushwa kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mnamo mwezi Disemba mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Susan Mlawi wakati wa Kikao cha Kamati inayofuatilia uanzishwaji wa chaneli hiyo.

Bi. Susan amesema kuwa vikao vya wadau na wataalam mbalimbali vitakavyowezesha uanzishwaji wa chaneli hiyo vinaendelea ambapo katika kikao hicho imetolewa taarifa ya hatua zilizofikiwa ambazo zimeonekana kuleta mafanikio makubwa.

"Tumekusudia kuifanya chaneli hii ambayo tunatarajia uzinduzi wake utafanyika mwezi Disemba mwaka huu kuwa na vipindi bora vyenye kugusa utalii wa kila aina. Aidha, tunategemea kuweka lugha mbalimbali ambazo zitasaidia watu wengi kutoka mataifa mbalimbali kuweza kuitazama."

Ameongeza kusema kuwa hadi kufikia muda huu tayari fedha za mitambo itakayoweza kuanzisha chaneli hiyo zimeshapatikana na ametoa rai kwa TBC kutoa kipaumbele katika maandalizi ya chaneli hiyo na kuandaa utaratibu maalum wa kusimamia matangazo yake.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa ni muhimu chaneli hiyo ionekane sehemu mbalimbali duniani ili kupata wadau wengi watakaoweza kuweka matangazo yao na kuiwezesha chaneli hiyo kujiendesha.

Amefafanua kuwa matangazo kupitia chaneli hiyo itakayotangaza utalii wa Tanzania yataingiza fedha nyingi ambazo zitasaidia kujiendesha badala ya nchi kutumia fedha nyingi kuutangaza utalii nje ya nchi.

"Kupitia chaneli hii, tunataka utalii uchukue sura mpya katika kuvutia uwekezaji kwani itawezesha Tanzania kujitangaza kiutalii katika nchi mbalimbali duniani na kuongeza Pato la Taifa," alisema Prof. adolf Mkenda.

Naye Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo amesema, nchi ikiwa na chaneli yenye maudhui ya utalii itasaidia Watanzania kufahamu kwa urahisi vivutio vilivyopo nchini pia itawafanya wadau mbalimbali kufahamu sio tu utalii bali pia masuala ya kiutamaduni.

Vile vile chaneli hii itawawezesha wadau kufahamu maeneo mahususi ya upigaji picha za mnato na jongefu ambazo zitaifanya nchi kujulikana zaidi nje ya nchi kupitia picha.

Uanzishwaji wa chaneli ya utalii kupitia TBC ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa wakati alipotembelea shirika hilo mnamo mwaka 2017.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...