Na Evance Ng’ingo
HIVI karibuni mfanyabiashara mkubwa nchini na Afrika nzima
kwa ujumla, Mohamed Dewji, Moo alitekwa na watu
wasiojulikana ambao hadi sasa jeshi la Polisi linaendelea
kuwasaka. Habari za kutekwa kwa Moo zimetangazwa kwenye vyombo vya
habari vya ndani na nje ya nchi ambapo kwa namna moja au
nyingine limetia dosari taswira ya nchi hii inayosifika kwa amani
duniani.
Tukio hilo limewashtua watu wengi ndani na nje ya nchi huku
akiombewa apatikane akiwa salama, lakini pia kuna watu ambao
wanatumia tukio hilo kama mwanya wa kuikosoa serikali kwa
madai ya kuwa imeshindwa kumpata mfanyabiashara huyo hadi
sasa. Wapo ambao wanalibeza jeshi la Polisi kuwa limeshindwa
kumsaka na kumpata mfanyabiashara huyo huku wengine
wakidai kuwa limeshindwa kukabiliana na matukio ya utekwaji
watu nchini.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Jeshi hilo hivi karibuni
linaonesha kuwa mwaka juzi, walitekwa watu tisa ambapo
watano walipatikana wakiwa hai na wanne hawajulikani walipo
hadi sasa huku watuhumiwa sita wamekamatwa na kufikishwa
mahakamani na mmoja aliuliwa na wananchi.
Mwaka 2017 walitekwa watu 27 ambapo 22 walipatikana wakiwa
hai, wawili wamekufa huku watatu hadi sasa hawajapatikana
watatu wamefariki huku watu 11 wamefikishwa mahakamani. Kwa mwaka huu Januari hadi Oktoba watu 21
walitekwa na Jeshi limewaokoa 17 huku wanne hawajapatikana
hadi sasa na watuhumiwa 10 wamefikishwa mahakamani.
Kwa takwimu hizi zinaashilia kuwa jeshi hilo linaweza
kukabiliana na matukio ya utekwaji nchini licha ya changamoto
za kiteknolojia zinazolikabili. Binafsi ningependa kuwasihi wanasiasa na watu wengine
mbalimbali kuwa na imani na jeshi hilo katika kumsaka na
kumpata mfanyabiashara huyo tajiri.
Tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara mkubwa wa kiwango cha
Mo ni la kwanza kutokea nchini hasa ikizingatiwa kuwa
takwimu za waliotekwa hakuna mfanyabiashara wa kiwango cha
Mo hivyo ni tukio linalohitaji umakini zaidi. Utekwaji wa aina hii unahitaji nguvu ya ziada katika kuukabili na
kuwa jeshi la Polisi peke yake haliwezi kufanikisha bila ya
kuwapo kwa ushirikiano thabiti wa wananchi.
Ushirikiano huo wa wananchi sio tu kuishia kusaidia kupatikana
kwa Mo lakini pia ni pamoja na kushiriki katika kuwafichua
watu wenye tabia za utekaji kwa ujumla. Jamii ikishiriki kikamilifu ni wazi kuwa matukio kadhaa ya
utekwaji hayataendelea kuwapo nchini hasa ikizingatiwa kuwa
tangia mwaka juzi kumekuwa na matukio ya aina hiyo.
Lakini pia ni lazima kwa hoteli na maeneo makubwa ambayo
hutembelewa na watalii nchini kuhakikisha kuwa yanalindwa na
walinzi kutokea kwenye kampuni zenye uzoefu na uwezo
mkubwa wa ulinzi.
Pia ufungwaji wa kamera za kurekodia matukio ni muhimu zaidi
katika kuwafichua kwa urahisi watekaji na wahalifu wengine
kwa ujumla. Watanzania, wanasiasa, viongozi wa dini, wasomi na jamii nzima
kwa ujumla tushirikiane kukemea matukio ya utekwaji wa watu
ili kunusuru haiba ya nchi yetu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...