Mkurugenzi wa Taasisi ya Nipe Fagio, Ana Rocha akielezea matokeo ya siku ya usafi duniani iliyofanyika hivi karibuni katika mikoa mbali mbali ya Tanzania. Picha na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.

Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
*Maelfu wajitokeza kushiriki nchi nzima
*Dar es Salaam yabainika kuwa eneo lililochafuliwa zaidi

Zaidi ya watu elfu ishirini na sita walijitolea kushiriki kwenye Siku ya Usafi Duniani ya kwanza na kukusanya zaidi ya tani mia nne za taka kutoka maeneo mbalimbali nchini. 

Kwa mujibu wa Ana Rocha, Mkurugenzi wa Taasisi ya Nipe Fagio walioratibu tukio hilo nchini watu 26,419 walijitokeza kushiriki Siku ya Usafi Duniani katika maeneo mbalimbali ya nchi na kukusanya jumla ya kilo 466,378 za uchafu sehemu kubwa ikiwa ni plastiki zitokananzo na vifungashio vya chakula na vinywaji. 

Amesema jiji la Dar es salaam ndio mkoa ambao umeathirika zaidi na uchafu nchini. Taka nyingi zaidi zilizokusanywa kwenye Siku ya Usafi Duniani zilitoka maeneo ya Buza Majumba 3 wilaya ya Temeke, eneo la Jangwani wilaya ya Ilala pamoja na Kimara Mwisho kwenye Manispaa ya Ubungo. 

“Pamoja na kwamba tatizo la taka bado ni kubwa, uelewa wa jamii kuhusu madhara ya uchafuzi wa mazingira unaeongezeka na Watanzania wanajitokeza kuchukua hatua. Tunawashukuru wote waliojitokeza pamoja na wadau waliosaidia kulifanya tukio hili liwe na mafanikio makubwa.”

Rocha amesema kwamba matukio 102 ya usafi yalifanyika katika mikoa 13 na zaidi ya miji 30 ambapo jumla ya mifuko 18,547 ya taka ilikusanywa. 

“Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba matukio ya kufanya usafi sio suluhisho la kudumu na hayawezi kuwa mbadala wa mifumo ya udhibiti taka. Lengo la tukio hili ilikua ni kuhamasisha jamii kuhusu uchafuzi wa mazingira, kutoona taka, na udhibiti hafifu wa taka. 

Tukio hili lazima lifuatiwe na mageuzi katika udhibiti wa taka yakiongozwa na wenye viwanda nchini hususani ambao vifungashio vya bidhaa zao vinachangia tatizo la taka. Nawaasa wenye viwanda wote nchini kuchangia na kushiriki katika jitihada za kuweka mifumo ya ukusanyaji na udhibiti wa taka. Plastiki na vifungashio vingine hazitakiwi kuchafua mito, kingo za barabara pamoja na bahari. Taka ni rasilimali muhimu zinatakiwa kusagwa na kutumika kutengeneza bidhaa, hii itasaidia kuongeza ajira na kuboresha uchumi,” amesema. 

Ukaguzi wa taka uliofanyika kwenye Siku ya Usafi Duniani ulibaini vyanzo vikuu vya uchafuzi wa mazingira ambapo taka nyingi zaidi zilibainika kuzalishwa na bidhaa maarufu hapa nchini ikiwa ni pamoja na mifuko ya kubebea vitu, makopo na chupa za bia, vifungashio vya maziwa, chupa za maji, vifungashio vya sabuni, viberiti, ndala, pombe kali, vichungi vya sigara, ice cream pamoja na vinywaji baridi kama soda na juisi. 

Kwa kushirikiana na Taasisi ya Let’s Do It! World pamoja na wadau wengine zikiwemo halmashauri za majiji na manispaa ilitoa mafunzo ya udhibiti taka na kuendesha kampeni ya uhamasishaji na vilevile ilitoa vitendea kazi kama mifuko, glovu pamoja na maji ya kunywa kwa waliojitolea kushiriki zoezi hilo. 

Kampeni hii iliyoasisiwa nchini Estonia mwaka 2008 imewaleta pamoja watu milioni 15 kutoka nchi 158 katika zoezi hilo lililofanyika Septemba 15. 

Taasisi ya Let’s Do It imepanga kufanya kazi na viongozi mbalimbali wa jamii nan a wadau kutengeneza mkakati wa udhibiti taka. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...