Madaktari Bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo wameanza kutoa huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mtwara, Ligula ikiwa ni moja ya mkakati wa MNH wa kuwajengea uwezo wataalam wa afya wa hospitali za rufaa za mikoa nchini ili kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa Muhimbili.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Ligula Dkt. Lobikieki Kissambu amesema wataalam hao watatoa huduma katika maeneo mbalimbali ikiwemo upasaji, magonjwa ya mfumo wa mkojo, magonjwa ya kike na uzazi, meno, macho, watoto, magonjwa ya koo, pua na masikio, maabara pamoja na magonjwa ya ndani.Amesema ujio wa wataalam hao utasaidia kupunguza gharama ambayo hospitali imekua ikitumia kusafirisha wagonjwa wanaopata rufaa kwenda Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.

Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi kwa mwezi hutoa rufaa kwa wagongwa 10 hadi 20 hivyo hutumia takribani shilingi milioni 300 kwa mwaka kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa hao.‘’Wataalam hawa kutoka Muhimbili watatusaidia kuwajengea uwezo wataalam wetu hasa ukizingatia hospitali ya Ligula ina upungufu mkubwa wa Madaktari Bingwa mpaka sasa hospitali hii ina Daktari Bingwa mmoja tu, lakini pia ujio huu utatusaidia kupunguza gharama za kusafirisha wagonjwa ambao wanapata rufaa ya kwenda kutibiwa Muhimbili. Amesema Mganga Mfawidhi.

Hata hivyo amesema katika kukabiliana na ukosefu wa Madaktari Bingwa hospitali hiyo imewapeleka shule Madaktari watatu ambao wanasomea ubingwa katika upasuaji, mifupa pamoja na koo, sikio na pua. Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya kike na uzazi kutoka Muhimbili Geofrey Marandu amesema mbali na kutoa huduma za afya lakini pia watawajengea uwezo watalam hao na kuhakikisha huduma hizo zinakua endelevu.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mtwara Dkt. Lobikieki Kissambu (kulia) akizungumzia ujio wa wataalam wa afya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, kushoto ni Daktari Bingwa kutoka Muhimbili Innocent Mosha.
Baadhi ya wagonjwa wakisubiri kupatiwa huduma katika hospitali hiyo mapema hii leo.
Watoa huduma katika Idara ya magonjwa ya dharura wa hospitali ya Ligula wakielekezwa na Daktari kutoka Muhimbili namna ya kumuhudumia mgonjwa ambaye amezidiwa.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya macho kutoka Muhimbili Judith Mwende (kushoto) akiangalia maendeleo ya mgonjwa wa macho ambaye alifanyiwa upasuaji wa macho mwezi wa tatu mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. 
Mtaalam wa kupima usikivu kutoka MNH, Sista Theresia Uisso akimuelekeza mgonjwa namna ya kuishi kulingana na tatizo linalomkabili, kushoto ni Madaktari wanafunzi wakifuatilia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...