Na Estom Sanga-DSM

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ,Dr. Mary Mwanjelwa ameuagiza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF kuendelea na Utaratibu bora zaidi wa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili Wananchi waweze kunufaika na Mpango huo ulioanzishwa na kutekelezwa na Serikali.

Dr. Mwanjelwa ametoa agizo hilo alipokutana na Menejimenti na Watumishi wa Mfuko huo akiwa katika ziara yake ya kikazi na kujitambulisha kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais Dr. John Magufuli hivi karibuni ambapo Naibu Waziri huyo alihamishiwa katika Wizara hiyo.

Naibu Waziri huyo amesema pamoja na mafanikio makubwa ambayo Mfuko huo umeyapata katika kuhudumia takribani Kaya Milioni Moja na Laki Moja za Wananchi wanaoishi katika umaskini, haupaswi kubweteka kwani suala la kupambana na Umaskini ni agenda muhimu katika Mipango ya Serikali ambayo pia imeainishwa kupitia ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Aidha Dr.Mwanjelwa ameagiza Watumishi wa TASAF kuwa Wabunifu na kufanya kazi kwa karibu zaidi na Wananchi hususani walioko katika Mpango ili Matokeo ya utekelezaji wa Shughuli za miradi yawe endelevu na yanayopimika ili hatimaye kero ya umaskini miongoni mwa Wananchi iweze kupunguzwa kama siyo kumalizika kabisa.

Akizungumzia utekelezaji wa shughuli za Miradi ya Ajira ya Muda, Naibu Waziri huyo wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ameagiza TASAF kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa kupitia utaratibu huo ni ile inayowanufaisha wananchi na malipo yafanywe kwa kuzingatia kanuni na taratibu za Serikali.

Wakati huo huo Dr. Mwanjelwa ametoa rai kwa halmashauri za wilaya kusimamia kwa karibu miradi inayotekelezwa na TASAF kwenye maeneo yao na kuonya kuwa pale ambapo itadhihirika kuwa halmashauri inakiuka taratibu wa miradi hiyo hatua zitachukuliwa haraka iwezekanavyo dhidi ya wahusika .

Akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Shughuli, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bwana Ladislaus Mwamanga amesema Mfuko huo umeendelea kutekeleza Maagizo ya Serikali ya kusaidia jitihada za Serikali katika kupambana na Umaskini nchini kote .

Bwana Mwamanga amezitaja sekta za Elimu, Maji,Afya ,Barabara,hifadhi ya Mazingira, Mifugo, Kilimo na uzalishaji mali na ujenzi wa rasilimali watu kuwa miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele tangu kuanzishwa kwa Mfuko huo takribani miaka 20 iliyopita miradi ambayo amesema imetekelezwa kwa mafanikio makubwa kwa kuwahusisha wananchi kwenye maeneo yao.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amebainisha pia kuwa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini licha ya changamoto kadhaa zilizotokana na ukubwa wa Mpango huo kumekuwa na mafanikio makubwa hususani katika kubadili fikra za Walengwa ambao kwa sasa wanaendelea kuboresha maisha yao kwa kutumia huduma za Mpango huo.Amesema maboresho muhimu yatafanywa kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali ili katika sehemu ya pili ya Mpango inayotarajiwa kuanza hivi karibuni kuwa na ufanisi zaidi ikiwa ni pamoja na kuyafikia maeneo ambayo hayakupata fursa hiyo katika awamu ya kwanza.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dr. Mary Mwanjelwa(aliyeshika kipaza sauti) akizungumza na Watumishi wa TASAF (hawapo pichani) kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bwana Ladislaus Mwamanga.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akitoa taarifa kwa Naibu Waziri Dr. Mary Mwanjelwa wakati alipofanya ziara ya utambulisho kwa watumishi wa taasisi hiyo.
Picha ya Juu na Chini baadhi ya Watumishi wa TASAF wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dr. Mary Mwanjelwa (hayupo pichani) ambaye alifanya ziara katika taasisi hiyo.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dr. Mary Mwanjelwa (aliyeketi katikati ) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa TASAF alipofanya ziara ya kujitambulisha .

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...