Afisa Usajili Msaidizi NIDA Bw. Makame Khamis Makame akitoa ufafanuzi kwa mgeni rasmi namna hatua za awali za Usajili wa Vitambulisho vya Taifa zinavyofanywa.
Kaimu Mkurugenzi NIDA Zanzibar Bw. Hassan H. Hassan akielezea jambo kwa mgeni rasmi na ujumbe wake wakati wa sherehe za uzinduzi wa jengo la ofisi za NIDA. Kulia ni Mh. Dkt. Khalid Salum Mohamed (Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi), wa pili kushoto ni Mh. Mohamed Aboud (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais) na wa pili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Dkt. Arnold M. Kihaule.

Baadhi ya watumishi wa NIDA Visiwani Zanzibar wakiwa wenye nyuso za furaha wakati wa sherehe za uzinduzi wa Jengo la Ofisi za NIDA wilaya ya Kati Dunga.



Mkurugenzi Mkuu NIDA, Dkt Arnold M. Kihaule akiiwasilisha taarifa ya ujenzi wakati wa sherehe ya Uzinduzi wa Jengo la NIDA Wilaya ya Kati Dunga.



Mh. Dkt. Khalid Salum Mohamed akizungumza mbele ya wageni waliohudhuria sherehe ya uzinduzi wa Jengo la NIDA wilaya ya Kati Dunga.



Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi, Mh. Dkt. Khalid Salum Mohamed(katikati mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na watumishi wa NIDA wakati wa Sherehe ya uzinduzi wa Jengo jipya la NIDA wilaya ya Kati Dunga.

………………………..

Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe Dkt Khalid Salum Mohamed amezindua jengo la ofisi ya Usajili wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi wanaoishi Wilaya ya Kati Dunga – Tanzania Zanzibar.

Uzinduzi huo ulifanyika na kushirikisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zikiwemo Taasisi za Muungano.

Akihutubia kwenye sherehe hizo Waziri Dkt. Khalid Salum Mohamed amewataka wananchi na wadau muhimu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA); kuhifadhi na kutunza miundombinu ya Mfumo wa Taifa na Utambuzi kwani taarifa zinazopatikana katika mfumo huo zitasaidia kupata takwimu sahihi ambazo zitaimarisha uchumi wa Nchi.

Aidha amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa juhudi zake za kuboresha mradi wa Vitambulisho vya Taifa unaosimamiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kujenga Ofisi za Usajili katika Wilaya mbalimbali nchini, na kusisitiza umuhimu wa Vitambulisho hivyo kwa wananchi, Kiuchumi, Kijamii na Kiusalama.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Vitambulisho vya Taifa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Dkt. Anold Mathias Kihaule amesema, zaidi ya asilimia 96.5 ya wananchi wa Zanzibar wameshaandikishwa na zaidi ya asilimia 90 tayari wameshazalishiwa vitambulisho vyao.

Dkt Kihaule amesema kukamilika kwa jengo la ofisi ya usajili wilaya ya Kati Dunga limegharimu zaidi ya Shilingi za Kitanzania Bil. 1.9 na kufanya mpaka sasa jumla ya kiasi cha Shilingi Bil 32 kuwa zimetumika katika kujenga majengo 13 nchi nzima ambapo kwa upande wa Zanzibar jengo hilo linakuwa ni la kwanza kukamilika katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa majengo ya ofisi za usajili.

Pia ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mchango wake mkubwa ilioutoa ikiwamo upatikanaji wa viwanja na kupatiwa msamaha wa kodi mbalimbali (exemption) ambazo zimesaidia kukamilika kwa jengo hilo linalotarajiwa kuhudumia zaidi ya wakazi 47,000.

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa imeahidi kuendeleza mikakati ya ujenzi wa majengo ya Ofisi ili kusogeza karibu zaidi huduma kwa Wananchi, ambapo katika awamu ya pili ya Ujenzi itakayoanza hivi karibuni itakuwa na ujenzi wa ofisi zingine tatu kwa Unguja na Pemba.

Awamu ya kwanza ya ujenzi mbali na Tanzania Zanzibar; maeneo mengine yaliyopata majengo ya Ofisi ni mikoa ya Mwanza, Morogoro, Dar-es-salaam, Kibaha na Arusha.

Ujenzi wa Ofisi hizo umetokana na mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Korea Kusini kupitia Benki ya Exim Korea.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...