Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara

Serikali imesema kuwa tarehe 10 Januari 2019 itasaini mikataba na wamiliki wa viwanda vya ubanguaji wa korosho waliojitokeza kwa ajili ya kubangua korosho za serikali za msimu wa mwaka 2018/2019 zilizonunuliwa na serikali kwa bei ya Shilingi 3300 kwa kilo.

Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 8 Januari 2019 wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Bodi ya Korosho (CBT) Mkoani Mtwara.Alisema kuwa hivi karibuni serikali ilitangaza kuwa korosho ghafi zote zitabanguliwa nchini hivyo utekelezaji wa jambo hilo umeanza, ambapo Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko itaingia mikataba ya ubanguaji.

Pamoja na wamiliki wa viwanda kupewa kazi ya kubangua korosho lakini pia serikali imewakaribisha wananchi kujitokeza kubangua korosho za serikali kupitia vikundi au mtu mmoja mmoja. “Wananchi wenye uwezo wa kubangua tunawaomba waende Shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo-SIDO) kwa ajili ya kujiandikisha ambapo mpaka sasa watu 126 kwa ajili ya ubanguaji na Tani 29 zimechukuliwa kwa ajili ya kuanza kubanguliwa” Alisisitiza Mhe Hasunga

Katika mkutano huo Waziri huyo wa kilimo Mhe Japhet Hasunga amempongeza Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kushuhudia utiaji wa saini mkataba wa mauziano ya mahindi kati ya Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula (NFRA) na Shirika la Chakula Duniani (WFP) wa Bilioni 21 zitakazoiwezesha NFRA kunua mahindi kwa wakulima hivyo kuimarisha soko la nafaka nchini. 
Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza mpango wa serikali kusaini mikataba ya ubanguaji wa korosho wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Bodi ya Korosho (CBT) Mkoani Mtwara, leo tarehe 8 Januari 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Bodi ya Korosho (CBT) Mkoani Mtwara, leo tarehe 8 Januari 2019.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Prof Siza Tumbo akifatilia mkutano wa Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Bodi ya Korosho (CBT) Mkoani Mtwara, leo tarehe 8 Januari 2019.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...