Mkutano wa waandishi wote wa habari za michezo unatarajiwa kufanyika Jumapili Februari 10 mwaka huu kujadili Rasimu ya Kwanza ya Mapendekezo ya Marekebisho ya Katiba ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA).

Kabla ya mkutano huo wa wadau wa habari za michezo, pia kutafanyika mkutano wa wahariri wa habari za michezo Februari 6 mwaka huu, lengo ikiwa ni kupitia rasimu hiyo kwa pamoja kabla ya kuifikisha kwa wadau wengine. Mikutano yote itafanyika Dar es Salaam, lakini ukumbi utatangazwa hivi karibuni.

Ni imani ya Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya TASWA kwamba mikutano hiyo yote miwili itakuwa na tija na itakuwa muongozo mzuri katika kuandaa Katiba bora kwa maslahi mapana ya waandishi wa habari za michezo nchini. Hivyo kamati inawaomba waandishi wote wa habari za michezo wajitokeze kwa wingi , ili kwa pamoja wajadili namna ya kuboresha rasimu ambayo ilitolewa Desemba 9 mwaka jana.

Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya TASWA imeandaa mapendekezo ya rasimu iliyoandaliwa kwa kuangalia Katiba za vyama mbalimbali duniani vinavyohusiana na waandishi wa habari za michezo na pia kupitia muongozo kutoka Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS), ambacho TASWA ni mwanachama.

Pia Kamati imechambua Katiba ya sasa ya TASWA na kupokea maoni kutoka kwa waandishi wa habari za michezo kuhusu maeneo yenye upungufu kwa nia ya kuiboresha.

Maeneo mbalimbali yamefanyiwa kazi katika rasimu hiyo baadhi yakiwa ni sifa za mwanachama, wajibu wa mwanachama, muundo wa uongozi, sifa za viongozi na pia ukomo wa uongozi. Pia kuna mapendekezo katika rasimu hiyo ya kuanzishwa kamati mbalimbali kwa nia ya kuisaidia Kamati ya Utendaji.

Kamati ya Katiba ya TASWA imeundwa kutokana na agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe aliyeitaka BMT isitishe uchaguzi wa TASWA uliokuwa umepangwa kufanyika Novemba 25 mwaka jana na badala yake BMT ikutane na viongozi wa TASWA pamoja na baadhi ya wanahabari wa michezo kuona namna ya kuifanyia marekebisho Katiba ya TASWA iendane na wakati.

Nawasilisha,Amir Mhando
Katibu wa Kamati ya Katiba/ Katibu Mkuu TASWA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...