Meneja
Mahusiano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Anjela Mziray akisisitiza
jambo kwenye kikao kazi cha wanachama wa vyama vya waandishi wa habari
mikoa ya Mtwara na Lindi.
Meneja
Uhusiano wa NHIF, Anjela Mziray akifafanua jambo, kulia kwake ni Kaimu
Meneja wa Mkoa wa Mtwara, Gidion Katondo na Meneja wa Mkoa wa Lindi Bw.
Emmanuel Mwikwabe, Kulia ni Wenyeviti wa Mtwara, Martina Ngulumbi na
Christopher Lilai.
Washiriki wa kikao kazi wakifuatilia mada juu ya shughuli zinazofanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Wanachama wa vyama vya waandishi wa habari mikoa ya Lindi na Mtwara wakifuatilia ufafanuzi wa hoja mbalimbali.
Sehemu ya wanachama hao wakifuatilia mada.
Meneja wa Mkoa wa Lindi Bw. Emmanuel Mwikwabe akiwasilisha mada ya maboresho yaliyofanywa na Mfuko.
Na Grace Michael, Mtwara
Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umewahimiza waandishi wa habari
kushirikiana nao katika kuendelea kuelimisha na kuhamasisha wananchi
kuhusu umuhimu wa bima ya afya pamoja na kushiriki kuulinda Mfuko huo
ili uweze kudumu na kunufaisha wengi.
Rai
hiyo imetolewa na Meneja Mahusiano wa NHIF, Anjela Mziray wakati wa
kikao kazi kilichofanyika mkoani Mtwara kikihusisha wanachama wa vyama
vya waandishi wa habari katika Mikoa ya Lindi na Mtwara.
“Nawaomba
sana ndugu zangu tuendelee kushirikiana katika kuhakikisha
tunahamasisha wananchi kupitia vyombo vyetu ili waelewe na kutumia
huduma za Mfuko huu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu
lakini pia ili Mfuko uendelee kuwa imara tuendelee kuunganisha nguvu
katika kuulinda Mfuko wetu,” alisema Mziray.
Alisema
kuwa endapo wanahabari watashiriki vyema juhudi za Mfuko za kufikisha
taarifa kwa wananchi zinazohusiana na umuhimu wa kutumia huduma za
matibabu kwa mfumo wa bima, wananchi wengi wataweza kujiunga na hatimaye
kuwa na uhakika wa kupata matibabu.
“Kwa
sasa bima ya afya ndio suluhisho kwa huduma za matibabu kwa wananchi
wetu na ili wafanikiwe kujiunga ni lazima tuhakikishe tunawafikia kwa
njia mbalimbali ikiwemo ya elimu na uhamasishaji hivyo kama ambavyo
mmekuwa wadau wazuri wa Mfuko tangu mwanzo tuendelee kuwafikia wananchi
wetu kupitia program mbalimbali za uelimishaji,” alisema Bi. Mziray.
Kwa
upande wa wanachama wa vyama vya waandishi wa habari katika Mikoa ya
Lindi na Mtwara, wameupongeza Mfuko kwa juhudi kubwa ambazo umefanya
hususan za kuanzisha mpango wa Ushirika Afya ambao utawasaidia kwa
kiwango kikubwa wakulima ambao awali hawakuwa na fursa hiyo.
“Mfuko
umekuwa ni mkombozi mkubwa kwa afya za wananchi wengi tukiwemo na sisi
waandishi wa habari, mfano mzuri sisi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara ni
wanufaika na tumeweka kipaumbele sana katika suala hili kwa kuwa
tunafahamu kabisa kuwa gharama za matibabu ni kubwa na bila bima ya afya
ni ngumu mtu kumudu gharama hizo, hivyo niendelee pia kuwahamasisha
wanahabari wa mikoa mingine kuhakikisha wanajiunga na Mfuko lakini pia
kuendelea na uhamasishaji,” alisema Katibu wa Chama cha Waandishi wa
Mkoa wa Lindi Bw. Christopher Lilai.
Mfuko
umesema unaendelea na maboresho mbalimbali ya huduma zake ikiwemo
kuongeza wigo wa wanachama kupitia makundi mbalimbali lakini pia
upatikanaji wa huduma za matibabu kirahisi kupitia uimarishaji wa mifumo
wa TEHAMA.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...