Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WADAU wa masuala ya lishe nchini zikiwemo asasi za kiraia nchini Tanzania wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli kwa kutambua lishe bora ni jambo muhimu katika kuboresha afya za wananchi huku wakitoa maombi na ku[endekeza mambo gani yafanyike kuhakikisha eneo la lishe linapewa kipaumbele.

Wameyasema hayo Machi 19,2019 wakati wa mkutano wa tathmini ya pili ya utekelezaji wa mkataba wa lishe.Mkutano huo ulifanyika ukumbi wa Kambarage Hazina katika Jiji la Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya Asasi za kiraia, Mkurugenzi Mtendaji wa PANITA Tumaini Mikindo ametumia nafasi hiyo kueleza kuna mambo muhimu katika kuboresha hali ya lishe nchini Tanzania.

Amefafanua Serikali ilitenga fedha katika bajeti kwa mwaka wa 2017/18 zipatazo Sh.bilioni 11 na mwaka 2018/19 zimetengwa kiasi cha Sh. bilioni 14 kwa ngazi za mikoa na wilaya kwa kigezo cha Sh.1000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano na kwamba hilo ni jambo jema na linapaswa kupongezwa.

Amesema utekelezaji wa bajeti hii unaonesha mambo kadhaa ambapo ameyataja ni sehemu kubwa ya bajeti hiyo ilitoka kwenye Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund) ikifuatiwa na ruzuku ya Serikali Kuu kwenda halmashauri na kwa kiwango kidogo toka kwenye mapato ya ndani ya halmashauri. 

Aidha mikoa ambayo inapata fedha za wafadhili au wadau wa maendeleo imekuwa haiweki fedha za vyanzo vya ndani katika bajeti za lishe au zikiweka basi ni kwa kiwango kidogo sana.

Pia wanaona bado utekelezaji wa matumizi ya fedha zilizotengwa, hasa zinazotoka vyanzo vya ndani vya halmashauri ni hafifu, na kwa baadhi ya halmashauri hazitoi fedha hizo kabisa.

"Hii inamaanisha nini? Kwa kipindi cha kati tutapata matokeo chanya kwa sababu fedha za wafadhili zipo. Lakini mafanikio haya hayatakuwa endelevu pindi miradi ya wafadhili itapomaliza muda wake. 

"Hivyo basi mwito wetu kwa serikali kuu ni kwamba kupitia halmashauli ijenge tabia ya kutenga na kutoa fedha kulingana na mipango waliyoipitisha.Aidha tunatambua kuwa vipaumbele ni vingi; lakini kwa hizo fedha kidogo zinapatika kutoka vyanzo vyetu vya ndani, basi kuwe na uwiano wa mgawanyo katika vipaumblele ikijumilisha kipaumbele cha lishe,"amesema. 

Amesema kuwa utaratibu huo utasaidia kuweka mfumo thabiti na endelevu katika kuboresha hali ya lishe ambao utajengeka juu ya msingi bora unaowekwa na fedha za wafadhili pindi miradi hiyo itakapokwisha.

"Vile vile matumizi ya hadidu za rejea za kamati za lishe za Mikoa na Halmashauri ni hafifu, hivyo kushindwa kufikia malengo ya NMNAP 2016/21. Hivyo ni mwito wetu kuwa Mikoa na Halmashauri zitilie mkazo matumizi ya hadidu hizo za kamati za lishe zinazolenga kuimarisha uratibu wa kazi za lishe katika ngazi za mikoa na halmashauri,"amesema.

Pia Mikindo amesema kuwepo na sera jumuishi ya kisekta ya lishe ni jambo muhimu, ili kuweka msingi bora zaidi wa kuratibu na kusimamia mukhtadha mzima wa kuboresha hali ya lishe kwa haraka ziadi. Aidha ametumia nafasi hiyo kueleza waamshukuru Makamu Rais Mama Samia Suluhu kwa kuwashirikisha katika mkutano huo adhimu cha kujadili utekelezaji wa mkataba wa lishe.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, manaibu makatibu wakuu, wadau wa maendeleo wa kitaifa na kimataifa, watendaji wa Serikali kutoa Ofisi pamoja na TAMISEMI.

"Nitoe shukrani za dhati kwa niaba ya asasi za kiraia kwa Serikali wa kutualika katika mkutano huu; na si hivyo tu na pia kutupa fursa ya kutoa salamu katika hadhara hii. Hii ni uthibitisho tosha Serikali ya awamu ya tano inavyothamini na kutambua mchango wa wadau ikiwemo Asasi za Kiraia katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya taifa hili kuelekea uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo 2025."amesema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...