MKAZI wa kijiji cha Mpanji kata ya Mbati wilayani Tunduru Awetu Mussa(52) amefariki Dunia baada  ya kujeruhiwa sehemu mbalimbali ya mwili wake  na kundi kubwa la Tembo.

 Tukio hilo lilitokea tarehe 22 Mwezi huu, ambapo marehemu alipatwa na mkasa huo wakati  akielekea shambani na mumewe Ahmad Kisanje ambapo  wakiwa njiani majira  ya asubuhi walikutana na kundi  hilo la Tembo ambao walipumzika chini ya mti na mara baada ya kuwaona walibadili mwelekeo wa safari yao na kuanza kuwafuata.

Kwa Mujibu wa mume wa marehemu  Ahmadi Kisanje ni kwamba,  licha ya marehemu kujitahidi kukimbia kwa lengo la kuokoa maisha yake lakini alizidiwa mbio na Tembo hao ambao walimuangusha chini na kumkanyaga  ambapo Awetu  alifariki Dunia papo hapo.

Kisanje alisema,yeye aliweza kunusurika kutokana na kujificha nyuma ya kisiki kikubwa  huku akishuhudia mke wake akipoteza Dunia kwa kukanyagwa maeneo mbalimbali ya mwili.

Tembo hao ambao wanatembea makundi makubwa kuanzia 20 na kuendelea, wanatoka katika Hifadhi ya Selou na mapori yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi wa misitu  wamekuwa wakiharibu mazao mashambani na  kuleta tahuruki kubwa kwa wananchi  hivyo  kusababisha hata kushindwa kwenda  katika shughuli zao mashambani.

Ameiomba Serikali kupeleka Askari  wa Wanyama poli wengi katika kijiji hicho ili kurudisha hali ya amani na utulivu kwani kama Tembo wataachwa  bila kudhibitiwa kuna hatari ya wananchi kushindwa kwenda katika shughuli za uzalishaji mali.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru  ambaye alifika nyumbani kwa Marehemu kwa lengo la kuipa pole familia ya  iliyompoteza mpendwa wao alisema, Serikali imesikitishwa na tukio hilo  na imeshapeleka Askari  kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama poli(TAWA)kanda ya Songea  ambao wameanza kazi ya kufukuza tembo kurudi katika makazi yao ya kawaida.

Homera ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Tunduru amewataka Wananchi wa kijiji hicho na maeneo mengine kuchukua taadhari pindi wanapokwenda mashambani na  kuaghailisha safari zao pindi wanapoona dalili za uwepo wa wanyama hao.

Alisema, serikali inathamini sana maisha ya wananchi,lakini ni lazima nao wawe na tabia ya kuchukua taadhari ikiwemo kutolima jirani na maeneo ambayo yamehifadhiwa  kwa ajili ya wanyama.

Akiongea katika mkutano na wananchi wa kijiji hicho Mkuu wa wilaya alisema, serikali haitalipa fidia wala  kutoa kifuta jasho  kwa mtu yoyote atakayejeruhiwa  na wanyama ambaye anafanya shughuli zake katika maeneo yasioruhusiwa kufanya shughuli za kibinadamu.

Kwa upande wake, mkuu wa kikosi cha  Mamlaka ya usimamizi Wanyamapoli kanda ya kusini Ruben Joseph amewataka wananchi kuwa makini pindi wanapokwenda mashambani na ikiwezekana kusubiri kwa muda wakati huu ambao wanaendelea kurudisha makundi hayo ya Tembo katika hifadhi.

Wakati huo huo kundi  kubwa la Tembo linakadiliwa kufikia 30 wamevamia shamba lenye ukubwa wa ekari tano  la mtendaji wa kijiji cha Mbesa wilaya ya Tunduru Rasso Kundeka na kuharibu  na kula matikiti zaidi ya  elfu tano.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera kulia akimpa pole Mzee wa kijiji cha Mpanji kata ya Mbati Ahmed Kisanje baada kufiwa na mkewe Awetu Musa kutokana na kushambuliwa na kuawa na Tembo alipokuwa njiani kuelekea shambani .
Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyapori kanda ya Kusini Ruben Joseph akiongea na wananchi wa kijiji cha Mpanji wilaya ya Tunduru baada ya kutokea kifo cha mkazi wa kijiji hicho baada ya kushambuliwa na Tembo wakati akienda shambani,katikati Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mpanji wilaya ya Tuunduru wakinyanyua mikono kama ishara ya kukubali kuanza ujenzi wa zahanati baada ya wananchi hao kukosa huduma za Afya kwa miaka mingi ambapo Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera(hayupo pichani) kuchangia mifuko 100 ya saruji na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori kanda ya Kusini nayo kutoa mifuko 10.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera wa pili kushoto akiangali mabaki ya Tikiti baada ya kundi kubwa la Tembo kuvamia na kufanya uharibifu wa mazao katika shamba la mtendaji wa kata ya Mbesa Rasso Kudeka.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera akikagua shamba la Afisa Mtendaji wa kata ya Mbesa Rasso Kundeka ambalo kundi la Tembo lilivamia na kufanya uharibu mkubwa wa mazao ikiwemo Matikiti,viazi na mbaazi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...