Pichani kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Jumia Tanzania, Bw. Zadock Prescott aakifafanua jambo leo mbele ya Waandishi wa Habari namna walivyojiunga na Soko la Hisa la New York na kuwa kampuni ya kwanza kabisa ya kiteknolojia kuanzishwa Afrika kufanya hivyo, akaongeza na kubainisha kuwa wanataka kuonyesha Dunia ubunifu wa kidigitali unaotokea Afrika na fursa kutoka Afrika kwa upande wa teknolojia na biashara ya mtandaoni,pichani kushoto ni  Meneja Uhusiano wa Umma na Masoko, Jumia Travel Tanzania, Geofrey Kijanga
kampuni inayoongoza kwa utoaji wa huduma za uuzaji na manunuzi kwa njia ya mtandao, imetangaza rasmi kuwa imeorodheshwa katika Soko la Hisa la New York nchini Marekani. Kuorodheshwa huku ni matokeo ya mafanikio ya timu nzima, wafanyakazi wote wa Jumia Afrika nzima. Tukio hili lilisherehekewa kwa ishara ya kupiga kengele kwenye kila nchi ambapo Jumia inafanya shughuli zake muda sawa sawa na jijini New York.

Ikiwa imeanzishwa mwaka 2012, Jumia ilianza mkakati wa kuboresha maisha ya kila siku barani Afrika, kwa kutumia teknolojia kuleta ubunifu, urahisi na unafuu wa upatikanaji wa huduma kwa wateja. Jumia pia inaziwezesha biashara kukua, kwa kutumia jukwaa ililonalo kuwafikia na kuwahudumia wateja barani kote Afrika. 

Kwa sasa, Jumia inafanya shughuli zake katika nchi 14 ikiwa na wauzaji takribani 81,000 wakiwa wanafanya biashara na mamilioni ya wateja. Jukwaa la biashara kwa mfumo wa mtandaoni limetoa ajira za moja kwa moja kwa wafanyakazi takribani 5,000 Afrika.

“Mafanikio haya kwa kiasi kikubwa yamefanikishwa na bidii ya timu yetu, imani ya wateja wetu, pamoja na kujitolea kwa wauzaji na washirika wetu. Wadau wetu wote wanastahili pongezi kwa hatua hii muhimu, na ndiyo kwanza tuko mwanzoni mwa safari ndefu na kubwa. 

Tutaendelea kujikita zaidi kwenye azma yetu na kufanya kazi kwa bidii zaidi kuwasaidia wanunuzi, wauzaji, washirika na wadau wote wanaofaidika na mapinduzi ya kiteknolojia,” walisema Sacha Poignonnec na Jeremy Hodara ambao ni waanzilishi na Wakurugenzi Wakuu ambao walikuwepo jijini New York, nchini Marekani wakati wa kufanyika kwa tukio hilo.
Akielezea sababu zilizopelekea mpaka Jumia kujiunga na Soko la Hisa kubwa zaidi duniani, Afisa Mtendaji Mkuu wa Jumia Tanzania, Bw. Zadock Prescott amebainisha kuwa, “kwa kujiunga na Soko la Hisa la New York na kuwa kampuni ya kwanza kabisa ya kiteknolojia kuanzishwa Afrika kufanya hivyo, tunataka kuonyesha dunia ubunifu wa kidigitali unaotokea Afrika na fursa kutoka Afrika kwa upande wa teknolojia na biashara ya mtandaoni.”

“Jumia kuorodheshwa rasmi kwenye Soko la Hisa la New York ni ishara kwamba kuna ubunifu unatokea barani Afrika - inaionyesha Afrika kuwa ni bunifu, inabadilika na kuwa ya kisasa zaidi. Hatua hii muhimu itatusaidia kuwavutia wauzaji wengi zaidi kwenye mtandao wa Jumia. 

Kwa sababu wauzaji na washirika wengi bado hawajatufahamu vizuri, na pindi wakitujua, tunaamini kuwa watatamani kufanya kazi na sisi,” alisema Bw. Prescott na kuhitimisha kuwa, “Tunaamini pia hii itatusaidia kujenga uaminifu zaini na wauzaji wetu, hususani kwa wale ambao bado hawajaanza kuzoea mfumo wa mtandaoni, wengi sasa watatuona kama kampuni imara na, tunaamini itatusaidia kwenye ukuaji na wateja kukubali huduma zetu. Hivyo basi, ningependa kuchukua fursa hii kuishukuru timu nzima kwa kufanya kazi kwa bidii, kujitolea kwa wauzaji na washirika pamoja na imani kutoka kwa wateja wetu.” 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...