NA MWAMVUA MWINYI,MKURANGA 

MKOA wa Pwani, umekemea serikali za vijiji zisiingilie kuuza maeneo yenye misitu hata kama hayajahifadhiwa kisheria na badala yake waisimamie na kuilinda. Aidha kila halmashauri imeelekezwa kuimarisha ulinzi wa raslimali za misitu ,ili kuhakikisha kunakuwa na usalama wa misitu na raslimali zake. 

Hayo yalibainishwa na mkuu wa wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga,kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo,   katika siku ya upandaji miti kimkoa iliyofanyika msitu wa Vikindu Mkuranga,wakati akisoma taarifa ya mkuu wa mkoa huyo .

Alisema, endapo maeneo ya msitu ama misitu ya hifadhi utavamiwa katika eneo la mwenyekiti ama mtendaji wa kijiji atawajibishwa kutokana na kutosimamia kikamilifu ulinzi na usalama wa misitu hiyo. 

Sanga alieleza misitu iliyopo kwenye ardhi huria (general land) inakatwa hovyo kutokana na maeneo hayo kutomilikiwa kisheria. Alieleza kwamba, serikali ya vijiji hutumia uwepo wa maeneo hayo kama fursa kwa kuuza maeneo na ardhi kwa wageni. 

Katika hatua nyingine alibainisha, wavamizi 4,500 waliovamia misitu ya hifadhi ya Kazimzumbwi, Ruvu Kusini, Uzigua, Masanganya, Namuete, Utete, Tamburu ,Mhoro mkoani Pwani wameondolewa.

"Kumekuwa na juhudi mbalimbali zilizofanyika hadi sasa, ambapo 2017 /2018 serikali kupitia wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) iliamua kuweka mipaka ya kudumu kuzunguuka maeneo ya misitu ya Kazimzumbwi, Mtanza Sona, Kipo, Namakutwa /Namuete na Uzigua kwa ajili ya kudhibiti uvamizi wa misitu hiyo jambo ambalo lilikuwa halijafanyika kipindi cha nyuma"alifafanua Sanga.

Hata hivyo alisema ,kila mwananchi anapaswa kuelewa umuhimu wa misitu, madhara ya ukataji miti kwa jamii na kwa vizazi vijavyo. 

Awali ofisa misitu Mkoani Pwani, Pierre Ntiyamagwa alisema, ongezeko kubwa la watu na ukosefu wa nishati mbadala kumetoa msukumo wa mahitaji makubwa zaidi ya mazao ya misitu hususan kuni, mkaa, mbao na maeneo ya makazi.

Akielezea kuhusu siku hiyo ya upandaji miti alieleza jumla ya miche 5,680 imepandwa .

Pierre alisema, mkoa huo una jumla ya misitu 87 yenye hekta 335,712 zilizohifadhiwa kisheria na hekta milioni 2.2 za misitu kwenye ardhi huria kati ya hiyo misitu 27 inasimamiwa na serikali kuu chini ya wakala wa huduma za misitu na misitu 57 iko kwenye hifadhi za vijiji. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...