TANZANIA PRIVATE SECTOR FOUNDATION 


TAMKO LA KUMUUNGA MKONO MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA MSIMAMO WAKE THABITI NA MAELEKEZO KWA WIZARA YA FEDHA NA MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA JUU YA UMUHIMU WA KUPANUA WIGO WA WALIPA KODI 

Kwa niaba ya Wadau wa Sekta Binafsi, Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Menejimenti, tunachukua fursa hii kwa mara nyingine tena kumpongeza Mheshimiwa Dokta John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumshukuru kwa Hotuba yake na Maagizo yake aliyoyatoa wakati akizungumza na Wizara ya Fedha na Mipango, Watendaji wa TRA na Taasisi zingine za Umma tarehe 1 Aprili 2019. Tumefarijika sana na juhudi zake binafsi za kuona umuhimu wa kuhakikisha kuwa Nchi yetu ina Mazingira Bora na ya Kuvutia Uwekezaji na Ufanyaji Biashara. 

Mheshimiwa Rais, amezitaja na kukemea Changamoto za Kodi kuwa ni kubwa na nyingi; utitiri wa taasisi za usimamizi na gharama zao ambazo zimekuwa zinatukwaza sana Sekta Binafsi kwa muda mrefu. Mzigo wa kodi ni mkubwa kwa wachache ambao wameandikishwa kwa sekta binafsi na hivyo maagizo yake kwamba zirekebishwe haraka yametupa faraja na hamasa ya kuongeza mchango wetu katika Uchumi wa Nchi Yetu tukielekea katika Uchumi wa kati na wa Viwanda. 

Sekta Binafsi tupo tayari kukaa na Serikali kupendekeza na kufikia muafaka wa njia mbalimbali za kupanua wigo wa walipa kodi, ili kwa pamoja, tufanyie kazi maagizo haya wa Mheshimiwa Rais. Sekta binafsi tutakutana ili kujadili na hatimaye kuwasilisha mapendekezo yetu kwa Mheshimiwa Rais kupitia Waziri wa Fedha na Mipango yatakayosaidia kuongeza wigo na kupunguza mzigo wa kodi kwa wadau. 


Katika kuratibu zoezi hili, TPSF na Sekta Binafsi katika ngazi zote kuanzia mawilayani na mikoani hadi Taifa tutashirikiana na Serikali na Taasisi za Sekta ya Umma ili kwa pamoja tujadiliane na kukubaliana hatua za haraka za kuchukuliwa kurekebisha mapungufu na changamoto alizoziainisha na kuzitolea maagizo Mheshimiwa Rais. Tuna uhakika kuwa tukitekeleza azma yake tutapanua wigo wa kulipa kodi na mapato ya Serikali na Uchumi wetu utaimarika na kuongezeka kwa kasi kubwa. 

Aidha, Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kumteua Naibu Katibu Mkuu (Sera) katika Wizara ya Fedha na Mipango. Sekta Binafsi tyumepokea uteuzi huu kwa mikono miwili na kuuona kama ni mwanzo mzuri wa kujengea uwezo wa Wizara katika kufanyia kazi masuala ya Sera, badala ya kutegemea TRA kama mshauri pekee. Tuna imani kwamba mtizamo wa Wizara ya Fedha na Mipango ni wa kukuza uchumi kupitia Sera ya Kodi lakini Mamlaka ya Mapato mtizamo wake ni wa kukusanya kodi hivyo basi kuna mgongano wa maslahi. Wizara pia itakuwa na uhuru wa kufanyia kazi masuala mtambuka. 

TPSF tunaungana na Mheshimiwa Rais kuhimiza na kuhamasisha Watanzania wote tulipe kodi kwa manufaa ya maendeleo yetu wenyewe. TPSF inamhakikishia Mheshimwa Rais kwamba tupo tayari kushirikiana na Serikali kupanua wigo wa walipa kodi pamoja na kushiriki kikamilifu katika Kamati za ushauri kuhusu masuala ya kodi, kama alivyoelekeza. Tuna uhakika kuwa kodi zikipunguzwa na taratibu za ulipaji zikiboreshwa na kufanywa rafiki zaidi, WaTanzania tutakuwa tayari kulipa kodi halali bila kushurutishwa au kutishwa. 

Tunaahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali na Sekta nzima ya Umma kwa kuwa na majadiliano ya kudumu yenye nia ya kuboresha mazingira ya kuwekeza, kushindana ndani na nje ya nchi na kuhakikisha kuwa WaTanzania, wadau wa Sekta Binafsi, wananufaika kutokana na jitihada hizi na kukuza uchumi wao na Taifa Zima kwa Ujumla. 

Imetolewa na Salum Shamte 
Mwenyekiti - Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) 
April 3, 2019 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...