Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Amos Nungu akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Wiki ya Ubunifu   kushoto ni Kiongozi Mkuu wa mfuko wa ubunifu wa maendeleo, (HDIF)David McGinty.
Makamu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza, Jane Miller akifafanua kuhusu fursa kwa wabunifu, wafadhili na sekta binafsi kuhamasisha masuala ya ubunifu.

Na Karama Kenyunko
TEKNOLOJIA ya Habari na Mawasiliano (Tehama) imekuwa kwa kasi nchini Tanzania na kuchangia kuleta mapinduzi makubwa  kwa kukuza na kuimarisha ustawi wa watanzania.

Pamoja na matokeo chanya na hasi ya mapinduzi ya teknolojia nchini lakini imekuwa mkombozi kwa masuala ya maendeleo hususan kwenye  sekta za afya, maji, usafi wa mazingira na elimu.

Mapinduzi hayo ya Tehama yamechangiwa na uwepo wa vijana na watu mbalimbali ambao wamekuwa wakiitumia  ipasavyo kuhakikisha inatatua changamoto zinazoikabili jamii kwa kubuni vitu mbalimbali.

Kwa kuliona hilo,  Mfuko wa Ubunifu kwa Maendeleo ya Watu (HDIF) kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) iliandaa Wiki ya Ubunifu kwa lengo la kuwakutanisha wadau wengi ili kubadilishana uzoefu na namna ya kuendelea sekta hiyo.

Kwa mwaka huu wadau  zaidi ya 3,000 wa ubunifu nchini walishiriki  katika Wiki ya Ubunifu katika Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Iringa ambao  walijadiliana namna ya kukuza na kuendeleza masuala ya ubunifu.

Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Amos Nungu anasema kuwa tume hiyo kwa kupitia Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia wamefungua milango kwa wabunifu mbalimbali kutoa fursa za kuendeleza ubunifu nchini.

"Kwa kushirikiana na HDIF na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweden (SIDA), tumetoa Sh bilioni 1.9 kwa wabunifu bora 32 na kumbi za bunifu 15 zilizoshinda mashindano tuliyoyaandaa mwaka jana," alisema Dk Nungu.

Anaeleza kuwa wameweka  utaratibu wa kuwatafuta wabunifu wote na kuweka kwenye makundi kulingana na viwango vya ubunifu wao na kwamba kwa kupitia maonesho mbalimbali wanawakutanisha pamoja na wadau ili kujua namna ya kuboresha bunifu zao.

Dk Nungu anasema kwa miaka mitano mfululizo HDIF na COSTECH wamekuwa wakishirikiana kuinua ubunifu nchini kupitia sekta za afya, maji na elimu na kuboresha mfumo mzima wa ubunifu ikiwemo uwezeshaji na miundombinu.

"Tunalenga  kuwa na mfumo thabiti wa ubunifu kwa kuhakikisha kuwa wabunifu, wataalamu mbalimbali na jamii inakutana ili kujifunza vitu ambavyo wabunifu hawa wanavifanya," anasisitiza.

Pia anasema maonesho  yanatoa fursa kwa wabunifu, watafiti kutoka vyuo vikuu nchini, wajasiriamali na jamii kwa ujumla kuona namna ya kukuza uchumi wa viwanda kupitia ubunifu.

"Katika kutekeleza lengo la kufikia uchumi wa viwanda, sekta yetu ya ubunifu yenyewe ina mchango mkubwa kwani inazalisha ajira na kutangaza bidhaa zetu ndani na nje ya nchi," alifafanua.

Sekta ya maji.

Moja ya mambo ambayo yalileta hamasa katika wiki hiyo ni matumizi ya teknolojia ya kadi kabla ya kupata huduma ya maji.

Teknolojia  hiyo imebuniwa Shirika la Catholic Relief Service (CRS) mradi ambao unatekelezwa wilayani Karatu Mkoa wa Manyara.

Matokeo ya ubunifu huo yameonesha kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 187 na kupunguza upotevu wa maji.

 Mhandisi wa maji kutoka ), Ephraim Tonya anasema kuanza kutumika kwa teknolojia hiyo ni baada ya kupata ufadhili HDIF.

Tonya anasema  kabla ya kutumika kwa mfumo huo, asilimia 30 ya maji yalikuwa yakipotea kutokana na watu kuyachezea na kwamba hata ukusanyaji wa mapato haukuwa mzuri.

Anaeleza kuwa waliona haja ya kubuni njia mbadala ya teknohama ili kuwezesha ukusanyaji wa mapato ambayo yatatumika na halmashauri pamoja na kudhibiti upotevu wa maji bila sababu maalum.

"Tulikuja na teknolojia mpya ya kutumia kadi ambapo malipo hufanyika kabla ya kuchota maji na tukasitisha malipo ya baada. Kwanza, tuliboresha miundombinu kwa kichimba visima ili mwananchi anapolipia huduma hii  aweze kuipata kwa wakati. Kwa njia hiyo tulifanikiwa kuongeza mapato kwa asilimia 187 ambazo ni mara mbili ya kusudio letu la ukusanyaji wa mapato," anasema Tonya.

Anaongeza kuwa fedha zilizokuwa zikipatikana katika mradi huo zimewezesha vikundi vilivyokuwepo wilayani humo kwa kufanya marekebisho  na kuboresha  miundombinu ya maji ili kutatua tatizo lolote linaloweza kusababisha ukosefu wa maji kwa wakati.

Anaendelea kueleza kuwa mradi huo umesaidia kuwajengea uwezo vijana walio katika mazingira magumu na wale wanaotoka vijijini kuhusu masuala ya ujenzi, ujasiriamali na namna ya kuandika maandiko ya kibiashara ili waweze kupata mikopo kutoka katika fedha za ndani za halmashauri.

Mtafiti kutoka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Arusha, Hans Komakech anasisitiza  kuwa  kabla ya kuanzisha mfumo wa malipo kabla waliangalia kama mfumo huo unatumika vizuri na kwamba hakuna mtu yoyote anayeachwa kwa sababu ya ugumu wa teknolojia hiyo.

Anasema  waliangalia namna mapato yanayopatikana upande wa maji kama yanaweza kutumiwa na mamlaka za maji kuwekeza katika miundombinu ya maji safi katika maeneo mengi.

"Teknolojia ya malipo kabla ni nzuri na inafanya kazi ya kukusanya fedha lakini changamoto iliyopo ni kwamba hakuna mfumo wa kuangalia watu wasio na fedha kwa wakati huo ili waweze kukopeshwa  nao wapate maji kwa sababu mfumo huo unawataka watu wote kufanya malipo kabla ya kupata maji bila kijali kipato,’’ anasisitiza Komakech.

Vilevile, anasema  kwa sasa wanaangalia uwezekano wa kutengeneza mfumo wa kuwasaidia watumiaji wa kipato cha chini kupata huduma hiyo bila kufanya malipo kabla na badala yake watafanya malipo baada ya kutumia maji.

Sekta ya Afya

Sekta ya afya nchini nayo haikuachwa nyuma katika kutumia Tehama katika kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi.

Kama inavyoelekezwa kwamba matumizi ya Tehama Tehama kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali na hii imeonekana katika sekta ya afya ambapo asilimia 70 ya hospitali na vituo vya afya kutumia teknolojia.

Ofisa Tehama kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sultana Seif  alibainisha mafanikio hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu hali ya utumiaji wa Tehama katika sekta ya afya kwenye maonesho hayo.


Anasema mfumo wa Tehama wa E-health uliopo wizarani umesaidia kufuatilia utoaji wa chanjo kwa watoto kwa kutambua siku aliyozaliwa, chanjo alizopata na ambazo hakuzipata ili kuhamasisha  wazazi kuwapeleka watoto wao kliniki kupata chanjo husika kwa ajili ya kuwakinga na magonjwa mbalimbali.


Seif anasema mfumo huo ambao umeanza kutumika, pia umeleta matokeo chanya kwa kuwa wanauwezo wa kufuatilia upatikanaji wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba kwenye hospitali na vituo vya afya vilivyopo hadi vijijini.

Anaeleza kuwa walipoanza kutumia mfumo huo mwaka 2015, watumishi wengi wa sekta hiyo hawakuukubali kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha wa Tehama lakini kutokana na mafunzo mbalimbali, wameukubali na kwamba unatumika bila tatizo.

"Hivi sasa utekelezaji wa mkakati wa kutoa huduma bora za afya hufanyika kwa njia ya teknolojia ambapo taarifa zote zinakusanywa na kutumwa moja kwa moja wizarani hivyo kusaidia kufanya maamuzi," anasema Seif.

Anaongeza kuwa "lengo la mfumo huu wa E-health ni kusaidia na kufikia vituo vya afya vilivyopo vijijini kutoa huduma bora kwa wakati na usawa."

Anafafanua kuwa serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa sekta ya afya inatolewa kwa njia ya kidijiti kwa kuboresha huduma hizo.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, lengo la mfumo huo ni kuhakikisha kuwa kila mtanzania anapata huduma zinazostahili kwa wakati na usawa.

"Kila mtu anahitaji   kupata huduma bora za afya hivyo, tulitafuta namna bora ya kuboresha huduma zetu kwa kutumia Tehama. Pamoja na hayo, tumezingatia usiri na usalama wa taarifa za wateja wetu," anaeleza.

Anasema  wadau wa maendeleo na taasisi nyingine za serikali zimeshiriki kutengeneza mfumo huo kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa kuandaa mazingira ya usawa na haki.

Miongozo hiyo inasaidia wadau kufanya kazi kwa kufuata miongozo iliyowekwa kwa sababu kumekuwa na changamoto ya wadau wa maendeleo kuanzisha miradi ya afya na kisha kuiacha bila kuiendeleza hivyo hupoteza rasilimali na haileti manufaa.

Meneja Program wa Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Vijana kutoka Shirika la  Amref, Dk Serafina Mkua anasema serikali imefanya mabadiliko makubwa kwenye sekta ya afya kwa njia ya kidijiti.

Dk Mkua anasema  serikali inaelekea kuondoka kwenye data ambazo zinakusanywa kupitia makaratasi na kwenda kwenye mfumo huo wa  E-health ambapo sasa watatumia simu na  kompyuta kukusanya taarifa.

"Miongozo ambayo imewekwa ni kitu kizuri ambacho kitasaidia wadau wote katika kutekeleza mikakati ambayo ipo lakini pia  kuleta bunifu zinazofuata miongozo ambayo ipo tayari.  Itasaidia  kuboresha utendaji lakini pia utoaji wa huduma kutokana na mabadiliko hayo," anasema Dk Mkua.

Naye, Mkurugenzi wa Ufundi wa HDIF, Muzafar Kaemdin anasema mfumo wa teknolojia kwenye sekta ya afya utasaidia kupunguza matumizi ya makaratasi ambayo huchelewesha wagonjwa kupata huduma.

Anasema matumizi ya makaratasi wakati wa uchukuaji taarifa za wagonjwa hutumia muda mrefu kuliko kutoa huduma husika hivyo matumizi ya Tehama yatachochea utoaji wa huduma bora za afya kwa wakati.

"Tumewakutanisha wadau wa afya tunaowafadhili pamoja na serikali hivyo tulichojifunza ni wadau wa maendeleo kuhakikisha wanajua ni watu gani wa kuwasiliana nao ili kuanzisha mifumo ambayo haikuwahi kuanzisha ili kusaidia kutoa huduma za afya na sio kila mdau kuwa na miradi  inayofanana nchini hii haitasaidia hivyo ni muhimu kuwasiliana na serikali kabla ya kuanzisha miradi," alieleza Kaemdin.

Kauli ya serikali

Hata hivyo,  Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha anasema kuwa serikali imeweka kipaumbele katika teknolojia ili kufikia Mpango wa II wa Maendeleo wa kufikia uchumi wa viwanda.

Ole Nasha anasema  ubunifu ni kichocheo cha kufikia uchumi wa kati kwa kuhakikisha kunakuwa mazingira wezeshi kwenye sekta za afya, elimu na viwanda.

"Ubunifu unasaidia kujenga uchumi unaoendeshwa na viwanda kwa kuondoa kero kwa watanzania. Kuendelea kutumia teknolojia za bunifu za wenzetu kutoka nje, haitasaidia kutatua changamoto za zetu kwa sababu hazifanani hivyo tutafute teknolojia zitakazoendana na mahitaji halisi ya Tanzania," anasema  Ole Nasha.

Anasema kuwa ili kufikia viwango vya ubunifu vinavyohitajika, serikali imeongeza fedha za ubunifu kwa Costech na kufungua dirisha la kushughulikia masuala ya ubunifu.

"Katika maonesho ya ubunifu yaliyofanyika Dodoma, tulipata washindi 30 na kazi zao zitaenda atamizi kwa ajili ya kuzifanyia kazi na kutumika katika masuala mbalimbali.
Wapo watu wengi ambao ni wabunifu wa kawaida kwenye jamii, ambao hawatambuliki hivyo wadau muhakikishe mnawafikia ili kutumia ubunifu zao zinazoendana na maisha halisi," anasisitiza.

Kwa mujibu wa Ole Nasha, wabunifu wengi ni wale wanaokumbana na changamoto za kila siku na kujaribu kuangalia namna ya kutatua changamoto hivyo, aliwataka wabunifu nchini kubuni teknolojia zenye manufaa ya kuondoa changamoto  na sio kujifurahisha kwa sababu wanaweza kukosa soko.


Anasema serikali katika hatua za mwisho za kukamilisha sera ya sayansi, teknolojia na ubunifu  itakayotoa mwongozo wa namna ya kutekeleza masuala ya ubunifu na kuwatambua wabunifu kwa ajili ya maendeleo.

Aidha, anasema  wako tayari kufadhili bunifu mbalimbali zinazoweza kuondoa changamoto nchini na kuchangia maendeleo ya uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake, Kiongozi wa HDIF, David McGinty anasema wadau wa maendeleo wamechangia Tanzania kupanda viwango vya kimataifa vya ubunifu.

Amesema wanaendelea kuhamasisha ubunifu kwa wanafunzi wa vyuo na sekondari kutumia teknolojia kwa ajili ya kujifunzia.

McGinty anasema wanaangalia ubunifu katika sekta za maji, afya, elimu na usafi wa mazingira kwa sababu ni miongoni kwa changamoto zinazoikabili jamii ya kitanzania.

"Serikali iendelee kuwekeza zaidi kwenye sekta za elimu na afya kwa ajili ya maendeleo ya nchi  kwa sababu ubunifu kwa kutumia  teknolojia ni njia mojawapo ya kuleta mabadiliko chanja inapotumiwa vizuri," anasema McGinty.

Naye, Makamu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza, Jane Miller anasema wanaendelea kuhamasisha wananchi  kuonesha kazi za ubunifu wanazofanya pamoja ili waweze kuwaunganisha  kwa lengo la kuleta mabadiliko ya ubunifu nchini.

Miller anasema ni lazima watumie ubunifu kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Tanzania katika sekta hizo ili kufikia malengo ya uchumi wa viwanda.

Anasisitiza kuwa  wataendelea kufadhili HDIF kwa ajili ya kutekeleza na kuinua masuala ya ubunifu nchini kwa sababu ili kuwa na maendeleo ni lazima kuhusisha ubunifu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...