Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini makubaliano ya ushirikiano na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa lengo kuu la kuboresha utoaji mafunzo katika sekta ya ngozi ili kuchangia kukuza sekta hiyo nchini na kusaidia  juhudi za kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.

Akizungumza wakati wa tukio la utiaji saini makubaliano hayo Aprili 25, 2019  katika Taasisi ya DIT Dar es Salaam, Mkuu wa DIT Profesa Preksedia Ndomba amesema makubaliano hayo yanalenga kupanua wigo wa utoaji mafunzo na kuimarisha mafunzo ya ufundi na kuzalisha nguvu kazi mahiri ya kuhudumia sekta ya ngozi kupitia mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Alisema DIT inalenga kutumia baadhi ya programu zinazotolewa katika vyuo vya VETA ili kupata vijana walioiva katika fani mbalimbali watakaojiunga kwenye programu zinazotolewa na Taasisi hiyo katika ngazi ya ufundi Sanifu.

Profesa Ndomba alisema kupitia makubaliano hayo taasisi hizo zitaanza utekelezaji wa utoaji na uboreshaji wa mafunzo hayo katika vyuo vya DIT- Kampasi ya Mwanza, Chuo cha VETA Dakawa na Chuo cha VETA Dodoma ikiwa ni pamoja na kuboresha karakana na kuweka vifaa vya kisasa vya utoaji mafunzo hayo.

Alisema kwa sasa DIT–Kampasi ya Mwanza inafanya usajili wa kutoa mafunzo ya ngazi ya tatu ya ufundi ili kuwezesha vijana wanaohitimu katika chuo cha VETA Dakawa kwa ngazi ya pili ya ufundi stadi kujiunga na chuo cha DIT Mwanza na kuendelea hadi ngazi ya Ufundi Sanifu.

“Tunaamini kupitia ushirikiano huu tutaweza kuongeza udahili katika chuo chetu cha Mwanza na kuzalisha wataalamu zaidi watakaoweza kuitumikia sekta ya ngozi na walimu wa kufundisha fani hii katika vyuo vya VETA.” Alisema

Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema ushirikiano huo utaisaidia VETA kuongeza uzalishaji wa mafundi stadi kwa ajili ya viwanda vya ngozi na bidhaa zitokanazo za ngozi.

Alisema kwa sasa VETA kupitia chuo chake cha VETA Dakawa inatoa mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi katika ngazi ya kwanza na ya pili ya ufundi na kwamba kupitia ushirikiano huo wahitimu wa chuo hicho wataweza kupata nafasi za kujiendeleza na mafunzo kwa ngazi ya tatu kupitia DIT-Kampasi ya Mwanza.

Dkt Bujulu aliongeza kuwa kupitia DIT, VETA itapata waalimu wa kufundisha fani hiyo mpaka ngazi ya tatu katika chuo cha Dakawa na kuweza kupanua wigo wa utoaji mafunzo katika vyuo vingine vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini, hasa maeneo ya wafugaji ili kusaidia wafugaji  kuongeza thamani ya mifugo yao.

“kwa sasa tuna changamoto ya wataalam pamoja na vifaa vya kufundisha fani hii katika vyuo vyetu na ndiyo maana hatujaweza kutoa mafunzo hayo hadi ngazi ya tatu ya ufundi….kupitia ushirikiano huu tunaamini changamoto hii itapata ufumbuzi.” Alisema

Alisema pia VETA itaanzisha mafunzo ya usindikaji na uchakataji ngozi katika chuo cha VETA Dodoma ambacho kwa sasa kinaendesha fani ya Usindikaji Nyama ili kujihakikishia upatikanaji wa malighafi bora ya ngozi itakayotumika katika uzalishaji wa bidhaa za ngozi.
 Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt Pancras Bujulu (kulia) na Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam Profesa Preksedia Ndomba (kushoto) wakitia saini makubaliano ya ushirikiano wa kuboresha utoaji mafunzo katika sekta ya ngozi tukio lililofanyika Dar Salaam. Waliosimama ni Wanasheria wa VETA na DIT walioshuhudia zoezi hilo.
 Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt Pancras Bujulu (kulia) na Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam Profesa Preksedia Ndomba (kushoto) wakitia saini makubaliano ya ushirikiano wa kuboresha utoaji mafunzo katika sekta ya ngozi tukio lililofanyika Dar Salaam. Waliosimama ni Wanasheria wa VETA na DIT walioshuhudia zoezi hilo
Picha ya pamoja ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt Pancras Bujulu (aliyeketi kulia) na Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam Profesa Preksedia Ndomba (aliyeketi kushoto) na baadhi ya wataalamu  wa VETA na DIT baada ya zoezi la utiaji saini makubaliano ya ushirikiano wa kuboresha utoaji mafunzo katika sekta ya ngozi tukio lililofanyika Dar Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...