Balozi wa Finland Pekka Makka ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa utekelezaji wa miradi ya Sekta ya Elimu inayofadhiliwa na Finland ambayo imewezesha uboreshaji katika maeneo mbalimbali ya sekta hiyo.

Balozi Makka ametoa pongezi hizo jijini Dodoma alipofika ofisi za Wizara na kukutana na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha kwa lengo la kushukuru kwa ushirikiano pamoja na kuaga baada ya kumaliza muda wake ambapo amesema kupitia utekelezaji wa miradi hiyo wameiona sekta ya elimu ikiboreshwa.

Makka amesema Wizara ya elimu imeboresha miundombinu katika shule mbalimbali nchini na kuweka mazingira mazuri ya wanafunzi kujifunza, huku akipongeza walimu kwa kuboresha mbinu za ufundishaji. 

Balozi huyo amesema Finland itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uboreshaji wa sekta ya elimu hususan katika maeneo ya Elimu ya Ufundi, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ili kupanua wigo wa upatikanaji wa mafunzo nchini.

“Tumeona maboresho makubwa katika sekta ya elimu, nasi kama wafadhili tumefarijika na hakika tunaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendelea kuboresha sekta hii muhimu, na ninaahidi kuwa Balozi anayekuja kunipokea ataendeleza ushirikiano huu,” amesema Makka.

Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameishukuru Finland kwa ufadhili wa Euro milioni 52 kwa ajili ya miradi, ambapo amesema kupitia ufadhili huo Tanzania imeshirikiana na Finland kuongeza fursa za elimu na mafunzo kwa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, hususan kwa kuwajengea uwezo watekelezaji wa mpango wa ‘Intergrated Post Primary Education (IPPE)’ na mpango wa ‘Intergrated Programme for Out of School Adolescents (IPOSA)’. 

Miradi mingine aliyoitaja ambayo imefadhiliwa na Finland ni pamoja elimu ya afya na michezo katika vyuo vya ualimu ambayo ililenga kuwajengea maarifa na ujuzi wakufunzi na walimu tarajali waweze kufundisha shuleni kwa kuzingatia umuhimu wa michezo shuleni na kwa maendeleo ya taifa, mradi wa Tehama, (TANZAICT) unaotekelezwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), mradi ambao umewezesha kuwepo na mifumo ya kukuza ubunifu na kuwezesha mfuko wa kufadhili wabunifu wadogo.

Aidha, Naibu Waziri amesema ushirikiano kati ya Wizara na Finland utakaoendelea unalenga zaidi katika Mafunzo ya Ufundi na Ubunifu na kwamba umekuja kwa wakati sahihi ambapo nchi inaelekea katika uchumi wa kati kupitia viwanda.

“Ili kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda ni lazima tuwe na rasilimaliwatu ya kutosha iliyoelimika na yenye maarifa na ujuzi kwa ajili ya viwanda na pia itakayoweza kujiajiri,” amesisitiza Ole Nasha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...