*Asema ahadi yake anaikumbuka na iko pale pale...ila kwa sasa ni miradi ya maendeleo

*Awaambia kupanga ni kuchagua na bora akawa mkweli

*Asisitiza Serikali inawajali wafanyakazi na inatambua mchango wao


Na Said Mwishehe, Michuzi TV
RAIS Dk.John Magufuli amesema ahadi yake ya kupandisha mishahara kwa watumishi wa umma kabla hajaondoka madarakani anaikumbuka na iko pale pale lakini amewaambia kwa sasa bado yupo madarakani, hivyo wavute subira.

Amefafanua kupanga ni kuchagua, hivyo badala ya kuongeza mishahara ya wafanyakazi wa umma , Serikali imeamua kujenga nchini kupitia miradi mikubwa mbalimbali ya maendeleo kwa kutumia fedha za ndani na kwake la kujenga nchi ni muhimu kwani faida yake itaonekana kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

Rais Magufuli amesema hayo leo Mei 1,2019 mkoani Mbeya wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafayakazi Duniani (Mei Mosi) ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza jitihada zinafanywa na Serikali kuhakikisha wafanyakazi wa kada zote wananuifa na miradi ya maendeleo.

"Kauli mbiu ya Siku ya Wafanyakazi ya mwaka huu inasema hivi Tanzania ya uchumi wa kati inawezekana, wakati wa mishahara na maslahi bora kwa wafanyakazi ni sasa.Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) amenikumbusha ahadi yangu ambayo niliitoa kwenye maadhimisho kama haya mwaka jana kuhusu nyongeza ya mshahara.

"Nilitoa ahadi kwamba kabla ya kuondoka madarakani nitaongeza mshahara lakini ni vema wakaelewa bado sijaondoka madarakani,"amesema Rais Magufuli.

Amefafanua kwa namna ambavyo miradi ya maendeleo inafanyika nchini na maelezo ambayo ameyatoa ni kwamba nchi inakwenda vizuri kiuchumi na hivyo wafanyakazi wote wanapaswa kuvuta subira kwani subira huvuta heri.

"Mambo yanayofanyika katika Taifa letu ni makubwa. Baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia kuna nchi ziliamua wafanyakazi wasilipwe fedha ili kujenga nchi yao. Kwa Tanzania tumeamua kuanzisha miradi kwa ajili ya maendeleo yetu.

"Wafanyakazi mimi ni mtumishi wenu, Serikali inawapenda na kuwajali.Pia huwa ninasikiliza ya wafanyakazi, wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wavuvi na makundi mengine, hili ni Taifa letu na lazima tulijenge kwani hakuna wa kutusaidia kulijenga. Hatua ambazo tunachukua ni kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

"Nawapenda watanzania wote na mimi nimekuwa mwalimu, mke wangu ni mwalimu, hivyo tunafafahamu changamoto za wafanyakazi. Waziri Mkuu Majaliwa naye ni mwalim na mkewe ni mwalimu,Waaziri Mhagama naye ni mwalimu, hivyo tunatambua shida zenu.

"Naomba wafanyakazi muamini kuwa Serikali inawapenda wafanyakazi wote na ndio maana .tuliamua kuchukua jukumu la kubeba kikokotoo cha zamani ambacho ni kigumu na hata nchi za ulaya hawana hicho,"amesema Rais Magufuli.

Ameongeza badala ya kuongeza posho na mishahara kwa wafanyakazi ni vema kwanza fedha ndogo ambayo inapatikana ikatumika kufanya maendeleo na mbali ya miradi ya maendeleo Serikali imeendelea kulipa madeni ya aina mbalimbali ambayo yamegharibi mabilioni ya fedha. Pia Serikali imeendelea kuajiri watumishi wapya wa kada mbalimbali pamoja na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.

"Serikali imekuwa ikilipa madeni, na hadi jana takwimu zinaonesha kuna ajira mpya zikiwemo za walimu 19,000 wapya , madaktari na watumishi wengine wa sekta ya afya wapya 11,000 wameajiriwa. Na hapo bado hujaweka sekta nyingine.

"Ndugu zangu wafanyakazi kupanga ni kuchagua, tungeweza kuamua tusiajiri ili fedha hizi tuongezeane posho.Nataka kusema ahadi yangu iko palepale, muda wangu haujaisha na kwa maono yangu uchumi bado unakuwa kwa asilimia saba na Tanzania ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika ambayo uchumi wake unakuwa kwa kiwango cha hali ya juu,"amesema Rais Magufuli.

Ameongeza kwa uchapakazi unaoendelea kufanyika nchini kupitia watanzania wa makundi mbalimbali anaamini kuna mambo mazuri yanakuja mbeleni na ameona ni bora awe mkweli badala ya kudanganya tu ataongeza mshahara halafu usiwepo.

Wakati huo huo Rais Magufuli ametumia nafasi hiyo kuelezea kuwa ni kweli ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka Sh.bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia Sh.trilioni 1.3.Pia mapato ambayo sio ya kodi nayo yameongezeka na  hasa baada ya mashirika na kampuni kutoa gawio kwa serikali na mwaka jana wamepata gawio la zaidi ya Sh.bilioni 700 na hayo ni mafanikio makubwa.

"Pamoja na ukusanyaji wa mapato kuongeza kuna changamoto  ambazo zipo ikiwemo ya fedha nyingi kutumika kwa ajili ya kulipa mshahara kwani kwa kila mwezi Serikali inalipa Sh. bilioni 580.

"Bahati nzuri siku hizi mishahara inalipwa kwa wakati.Tukishalipa mshahara kiasi ambacho knabaki tunatakiwa kulipa madeni na nyingine kutumika kufanya maendeleo na hivyo kiasi kidogo ambacho kinabaki ndio tunajiuliza kiende wapi.

"Jinsi tunavyojiuliza, ndivyo ambavyo hata wakulima nao wanajiuliza kuhusu mbegu yake ya mavuno ale kwasababu ya njaa au atunze kwa ajili ya mbegu.Ndivyo ambavyo wafanyabiashara nao wanavyojiuliza nini wafanye kuhusu mtaji wao.

"Serikali tumeona ni busara kiasi kidogo ambacho kinabaki kikatumika katika miradi ya maendeleo ili iwe kichocheo.Kwa kutumia utaratibu huo ndio maana ujenzi wa reli ya kisasa unaendelea kwa kutumia fedha za ndani ambazo zimetolewana Watanzania wote,"amesema Rais Magufuli.

Pia amesema kuna ujenzi wa barabara katika meneo mbalimbali nchini, na kwamba kwa taarifa ya jana tu Benki ya Maendeleo Afrika imeidhinisha mkopo wa ujenzi wa barabara wa kilometa 110 ambazo ni nyingi.

Rais Magufuli amesema wameamua kukarabati na kujenga meli mpya katika maziwa mbalimbali,kuna upanuzi wa  bandari ya Dar es Salaam,Tanga na Mtwara. "Tumenunua ndege mpya nane, upanuzi wa viwanja vya ndege 11".

Ameongeza kuna ujenzi wa umeme wa maji katika maporomoko ya mto Rufiji ambako zitapatikana megwati 2100, pia kuna mradi wa umeme Kinyerezi na lengo ni kuwa na megawati 5000."Kero kubwa ni bei kubwa ya umeme na lengo la Serikali ni kuwa na umeme wa kutosha na kisha kupunguza bei.

"Mbali ya miradi ya maendeleo pia Serikali imendeelea kuboresha huduma muhimu kwa ajili ya wananchi ambapo .Katika sekta ya afya tunaendelea na ujenzi wa vituo vya afya 64 nchini ambavyo vinatumia fedha nyingi,tunanunua dawa na vifaa tiba  ambapo bajeti yake ni kubwa.

"Kwa upande wa maji nako kuna miradi mingi inaendelea na zaidi ya Sh.trilioni moja zinatumika kufanikisha miradi hiyo katika miji 21 nchini.Hatua mbalimbali Serikali inafanya ili kuhakikisha nchi inapiga hatua kimaendeleo,"amesema Rais Magufuli.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...