Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Majimaji wilaya ya Tunduru waliojitokeza kwa ajili ya uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu wakati wa kampeni ya uchunguzi wa ugonjwa huo kwenye vijiji vinavyozungukwa na machimbo ya madini na maeneo ya machimbo iliyoendeshwa na Shirika lisilo la Serikali ya MDH kwa kushirikiana na Hospitali ya wilaya ya Tunduru.
Baadhi ya watoto wa kijiji cha Majimaji wakiwa katika mstari wakisubiri kufanyiwa uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa Tb wakati wa zoezi la uchunguzi wa ugonjwa huo kwa vijiji na maeneo yanayzungukwa na machimbo ya madini wilayani Tunduru chini ya usimamizi wa Shirika la MDH kwa kushirikiana na Hospitali ya wilaya ya Tunduru.

Na Mwandishi wetu, Tunduru

SHIRIKA lisilo la Kiserikali la MDH kwa kushirikiana na Hospitali ya wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma limeanza Kampeni ya kupima  ugonjwa wa kifua kikuu kwa wananchi wa vijiji vinavyozungukwa na machimbo kama hatua  ya kumaliza  ugonjwa huo. Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma inatajwa kuwa miongoni mwa wilaya ambazo zimeathirika kwa kiwango kikubwa na ugonjwa huo hapa Nchini.

Kampeni hiyo iliwahusu wananchi wa vijiji vya Majimaji,Muhesi na Magomeni ambapo watu wanaojihusisha na uchimbaji wa madini wanatajwa kuwa kundi mojawapo  ambalo  limeathirika sana na ugonjwa wa kifua kikuu.

Kampeni hiyo inafanywa na Shirika linalojihusisha na uborehaji wa Huduma za Afya(MDH)  kwa kushirikiana na Hospitali ya wilaya ya Tunduru  chini ya kitengo cha Kifua kikuu na Ukoma  na inalenga kuwafikia   watu wote wanaoishi katika  maeneo ya machimbo  na vijiji  vyote vinavyozungukwa na shughuli za uchimbaji.

  Afisa mradi wa Uibuaji wa wagonjwa wa Kifua Kikuu katika Jamii kutoka Shirika la MDH mkoa wa Ruvuma  Dkt Nixson John alisema,zoezi la uchunguzi wa Wagonjwa wachimbaji  wa Madini pamoja na vijiji vinavyozunguka maeneo hayo linafanyika katika wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma.

Kwa mujibu wa Dkt Nixson zoezi hilo lilianza  tarehe 12 hadi 17 Mwezi Mei  ambapo katika  wilaya ya Tunduru uchunguzi ulifanyika  kwenye machimbo ya wachimbaji wadogo katika kata ya Muhesi na Majimaji ambapo idadi ya wahisiwa wa ugonjwa  wa kifua kikuu 202 ,na  sampuli 200 za makohozi zilikusanywa.

Alisema, mpaka sasa watu waliogundulika na maambukizi ya vimelea vya kifua kikuu ni 9 kati ya sampuli zilizokwishapimwa  kati yao  mtoto mmoja yeye alianzishiwa dawa kutokana na kukidhi vigezo na mtu mzima mmoja nae alianzishiwa kwa kuwa na dalili za kifua kikuu nje ya  mapafu na zoezi la upimaji wa sampuli  bado unaendelea.

Dkt Nixson alisema, wataalam walioshiriki katika kazi hiyo ni kutoka Hospitali ya wilaya ya Tunduru wakiongozwa na Mratibu wa Kifua kikuu na Ukoma Dkt Mkasange Kihongole ambapo shirika la MDH ni watekelezaji wa Mradi chini ya ufadhili wa  mfuko wa Dunia wa  Mapambano ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu,Malaria na Ukimwi(Global Fund).

Kwa upande wake Mratibu wa Kifua kikuu na Ukoma wa Hospitali ya wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema, watu wanaoishi katika vijiji  vinazungukwa na machimbo na wale wanaoishi katika maeneo ya machimbo wako katika hatari zaidi kupata ugonjwa.

Alisema, hali hiyo inatokana  na muingiliano wa mara kwa mara  na mkusanyiko mkubwa wa watu kutoka katika maeneo mbalimbali ambao baadhi tayari wamepata maradhi ya Kifua kikuu  hivyo ni rahisi  wale waliopata ugonjwa huo kuambukiza Watu wengine.

Dkt Kihongole alisema, kampeni  ya uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo   katika wilaya ya Tunduru imefanyika katika vijiji vitatu vya Muhesa,Majimaji na Magomeni ambapo jumla ya sampuli zilizochukuliwa kwa ajili ya  kufanyiwa  uchunguzi  ni  200 na mpaka sasa zilizopimwa na kupata majibu ni wagonjwa 9 na zoezi la upimaji bado linaendelea.

Alisema, ugonjwa wa kifua kikuu ni miongoni mwa magonjwa kumi Duniani ambayo yanaongoza kwa kuuwa watu,ndiyo maana kwa kutambua ukubwa wa tatizo  Serikali kwa kushirikiana na mfadhili Shirika la MDH limeanza  uchunguzi na upimaji kwa wananchi kwa kuwafuata vijijini kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa vimelea vya TB badala ya kuwasubiri ofisini.

Alisema,  kimsingi  hatua  hiyo itasaidia  kuwafikia watu wengi na hivyo kuokoa maisha na kusisitiza kuwa,ugonjwa wa TB unatibika na kuwataka wananchi kuwa na mazoea ya kufanya uchunguzi wa Afya zao mara kwa mara.

Kihongole  alibainisha kuwa, ugonjwa huo huambukiza sehemu mbalimbali za mwili wa Binadamu kama vile Uti wa mgongo,Tumbo,Figo,Utumbo,mifupa,Ubongo,Macho na Ngozi ambapo mtu mmoja mwenye kifua kikuu anaweza kuambikiza mpaka watu wengine 15.

Alisema, vimelea vya kifua kikuu huishi katika sehemu za giza na zisizo ingiza Hewa vizuri,mfano Nyumba yenye msongamano na isio na madirisha,Darasa lenye madirisha machache n ahata kwenye gari ambalo halina hewa ya kutosha.

Alisema, kwa watoto wadogo  dalili mojawapo ya kifua kikuu ni kikohozi kwa wiki mbili au zaidi,Homa za mara kwa mara,kupungua uzito/kutoongezeka uzito,  zaidi ya siku tatu,kutokwa na jasho.

Mmoja wa watoa huduma ngazi ya jamii  anayeishi katika kijiji cha Majimaji kata ya Majimaji Ismail Sitambuli alisema, kampeni hiyo itawasaidia wananchi wengi wanaoishi na kifua kikuu bila kujitambua kujielewa na kuanza matibabu haraka.

Alisema, katika mpango huo Wananchi pia wataokoa rasilimali fedha na muda wanaoutumia kutembea umbali mrefuhadi Hospitali kufuata huduma.

Hata hivyo ameiomba Serikali kuwa,huduma ya uchunguzi wa vimelea vya Kifua kikuu n ahata magonjwa mengine ni vema iwe endelevu kwa sababi itasaidia kwa kiwango kikubwa kuokoa maisha ya Watanzania hasa wale wanaoishi maeneo ya vijiji na machimbo ya madini ambao wanakabliwa na tatizo kubwa la kufikiwa kwa Huduma za Afya.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...