* Jamii yashauriwa watoto wanakuwa salama kwa kupiga vita vitendo vya unyanyasaji

Na Leandra Gabriel, Globu ya Jamii
KATIKA kuelekea kilele cha siku ya mtoto wa Afrika inayofanyika kila tarehe 16 Juni kila mwaka shirika la maendeleo la  BRAC Tanzania limeadhimisha siku hiyo kupitia mradi wake wa elimu ya makuzi na malezi kwa watoto unaojulikana BRAC Play Lab.

Akizungumza katika hafla hiyo Afisa Ustawi wa jamii Manispaa ya Temeke Eva Komba amesema kuwa shirika hilo limekuwa msaada mkubwa sana katika suala zima la malezi na kuwataka wazazi wahudhurie semina za mafunzo kuhusiana na malezi ya watoto.

Amesema kuwa Play Lab zilizoanzishwa kwa ajili ya malezi wazazi wazitumie kwa kuwapeleka wao ili wapate kujifunza kupitia  huku akihaidi kuwa serikali itazidi kutoa ushirikiano kwa mashirika hayo.

Aidha amewataka wadau mbalimbali wa namna hiyo kushiriki katika shughuli za kijamii hasa elimu na afya.

Kwa upande wake wake Meneja programu ya elimu Suzan Bipa amesema kuwa  mradi huo wa BRAC unaotumia michezo unafadhiliwa  na mfuko wa maendeleo wa LEGO na ni moja ya miradi bunifu ya maendeleo ambayo unahudumia watoto wa umri wa miaka 3 hadi 5 kutoka familia maskini kwa kuhakikisha wanapata elimu ya awali.

"Sisi kama BARC kila siku ni sherehe ya mtoto wa Afrika kwa sababu programu mbalimbali ambazo sisi tunazitekeleza nchini ni endelevu na siku zote tunalenga kuhakikisha watoto wanalindwa, wanatunzwa na kuendelezwa" ameeleza Suzan.

Amesema kuwa mipango yao inalenga kuwawezesha wanawake ambao ni walezi wakuu wa watoto na wao wataendelea kuchangia majukumu muhimu ya maendeleo ya watoto.

Aidha amesema kuwa mafanikio ya mradi huo umetokana na ushirikiano bora  toka kwa wazazi na walezi katika suala zima la malezi ikiwemo utunzaji wa usalama kwa watoto pamoja na haki zao.

Vilevile ameeleza kuwa mradi huo wa Play Lab BRAC ulichaguliwa kutumika kutokana na mtindo wake uliokuwa wa ubunifu wa kujifunza ambao unatoa fursa ya mafunzo kwa watoto walio katika mazingira magumu kwa kuwapa mafunzo bora yenye gharama nafuu.

Kuhusu rasilimali zitumikazo kwa watoto hao Suzan ameeleza kuwa wazazi wamekuwa wakishiriki kwa karibu katika kutengeneza vifaa vinavyotumika katika Play Lab hizo na pia kusaidia walimu wakati wa darasa.

BRAC nchini inatekeleza mradi wa Play Lab katika Mikoa ya Mbeya na Dar es Salaam na hadi sasa watoto 1200 wanapata mafunzo hayo na tangu kuanza kwake zaidi ya watoto 2400 wamemaliza mafunzo hayo kupitia vituo 80 vya Play Lab.

Imeelezwa kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006 zaidi ya watu milioni 4.13 katika Mikoa 25 wamefikiwa ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu, biashara ndogondogo, kilimo na chakula na hiyo yote ni kwa malengo ya kupunguza umaskini.

Licha ya miradi hiyo kwa watoto BRAC inasaidia watoto wa kike walioacha shule kwa sababu za mimba za utotoni na kukosekana kwa ada kwa ajili ya masomo yao kwa kuwapa mitaji na mafunzo mbalimbali.
 Meneja wa programu ya elimu BRAC Suzan Bipa akizungumza wakati wa maadhimisho hayo ambapo ameeleza kuwa wataendelea kuwa karibu na wazazi ili azma ya kuwasaidia watoto itimie, leo jijini Dar es Salaam.
Afisa ustawi wa jamii Manispaa ya Temeke Eva Komba akizungumza wakati wa hafla ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambapo amesema kuwa serikali ipo pamoja na itaendelea kushirikiana na mashirika ya namna hiyo, leo jijini Dar es Salaam.


 Watoto wakionesha shughuli mbalimbali ambazo ni zao la waliofundishwa kupitia Play Lab ya BRAC, leo jijini Dar es Salaam.

 Watoto wakiwa na uongozi wa BRAC wakikata keki wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto Afrika yaliyofanyika katika viwanja vya Bandari, leo jijini Dar ea Salaam.
Uongozi wa BRAC wakiwalishwa keki na watoto wakati wa maadhimisho hayo, leo jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...