Na Ripota Wetu,Ruvuma

BAADHI ya Wakulima wa Tumbaku wilaya ya Namtumbo, wameupongeza mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) kuweka utaratibu wa uchunguzi wa Afya kwa wakulima wa zao hilo waliojiunga kwenye vyama vya msingi vya Ushirika.

Wakulima hao wamesema, ni jambo la mfano na kuigwa na mashirika mengine ya umma hapa nchini kwani mpango wa huo wa NHIF utasaidia sana kuwa na wakulima wenye Afya njema ambao wataweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na hivyo kuongeza idadi ya wananchi wengi ambao watajiunga na mfuko huo.

Wakizungumza wakati wa ufunguzi wa mpango wa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa yasio ambukiza na Ushauri wa kitaalam kwa wakulima wa Tumbaku ambao ni wanachama wa wa Chama cha msingi vya ushirika Namtumbo AMCOS.

Walisema, NHIF imefanya uamuzi sahihi hasa wakati huu ambao baadhi ya wanachama wanajianda kusafisha mashamba yao kwa ajili ya msimu mpya wa kilimo 2019/2020.Fadhil Kitete alisema, mpango huu wa uchunguzi wa Afya una manufaa makubwa kwa wana ushirika kwani watapata kufahamu hali ya Afya na kutibiwa katika Hospitali yoyote Nchini.

Hassan Kwitenda ameshauri kiwango cha shilingi 76,800 ambacho mwana Ushirika anapaswa kuchangia mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa ajili ya kupata matibabu katika kipindi cha mwaka mmoja ni kikubwa na kushauri kipunguzwe ili kutoa nafasi kwa wakulima wengi waweze kujiunga na mfuko huo.

Alisema, hapo mwanzo Serikali ilitaka kila mwana Ushirika na mwananchi kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii(CHF) ambayo gharama yake ilikuwa elfu Ishirini,lakini sio watu wote waliojiunga na mfuko huo kwani baadhi walishindwa kutokana na kukosa fedha.

Kwa upande wake Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) Dkt Mchelle Starmius alisema, katika ufunguzi huo walifanya uchunguzi wa Kisukari,Moyo(Pressure)kuangalia uwiano kati ya uzito na urefu, na kutathimini hali ya lishe kwa wanachama.

Alisema, zoezi la uchunguzi litahusisha wanachama wa Vyama vyote 22 vya Msingi vya Ushirika katika wilaya ya Namtumbo lina lenga kuweka ufahamu wa Afya za wanachama na atakayebainika kuwa na matatizo atapewa ushauri wa kitaalam na kupewa matibabu katika Hospitali yoyote hapa nchini kwa gharama za mfuko huo.

Alisema, mpango huo una faida kubwa kwa mwanachama kwani ataweza kutambua hali yake,kupata ushauri sambamba na kupata tiba sahihi ya ugonjwa alionao.

Hata hivyo,amewashauri wakulima wa Tumbaku na mazao mengine ya kimkakati Kahawa,na Korosho ambayo yanalimwa kwa wingi mkoa wa Ruvuma kujiunga kwa wingi kwenye vyama vya msingi vya ushirika ili wapate nafasi ya kuwa Mwanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulioboreshwa ambao utamwezesha kupata fao na kadi ya Matibabu.

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Sophia Kizigo amewaondoa wasiwasi Wanachama wa Vyama vya Ushirika kuwa, Huduma za matibabu zinazotolewa na NHIF ni tofauti na zinazotolewa na Mfuko a Afya ya Jamii kwani wale watakaojiunga na NHIF watapata fursa ya kutibiwa katika Hospitali yoyote hapa Nchini ikilinganisha na CHF ambayo mwanachama anatibiwa ndani ya wilaya yake.

Alisema,Serikali kwa kutambua kero wanayoipata wanachama wa CHF ndiyo maana imekuja na mpango mpya abao unamwezesha mwanachama wa chama cha Ushirika kuchangia shilingi 76,800 ambazo zitamwezesha kupata matibabu bora na imeongeza Bajeti ya fedha kutoka shilingi Biliono 30 hadi kufikia Bilioni 200 kwa mwaka.

Katika Hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Aden Nchimbi, Kizigo ameipongeza NHIF kuboresha huduma kwa mwanachama na kuwataka wananchi wa Namtumbo kuona kuwa,hiyo ni fursa muhimu ambayo itamsaidia kupata matibabu katika Hospitali yoyote hapa Nchini.

Alisema, na kila Mtanzania anatakiwa kuwa na Afya njema ambayo itamwezesha kushirika kikamilifu kazi za kujiletea maendeleo na mpango huo utawasaidia wanachama hata kupunguza gharama za matibabu pale wanapokwenda kupata huduma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...