NA K-VIS BLOG, Khalfan Said, Simiyu
MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF) umeibuka mshindi wa kwanza kundi la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kutwaa kombe katika maonesho ya Nanenane viwanja vya Nyakabindi nje kidogo ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu leo Agosti 8, 2019.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, alimkabidhi kombe hilo Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko huo Bw. Anselim Peter wakati wa kilele cha sherehe za nanena kitaifa ambapo Waziri Mkuu alikuwa mgeni rasmi.
WCF ni Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ambapo unatoa Fidia kwa mfanyakazi aliyeumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi.
Awali Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko huo Bw. Anselim Peter aliwaambia waandishi wa habari kuwa wadau wengi waliotembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika maonesho ya Nanenane viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu, walitaka kujua utaratibu wa kufuata ili kudai fidia wapatapo matatizo ya kuumia, kuugua au hata vifo vitokanavyo na kazi.
Mkurugenzi wa Uendeshaji Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Anselim Peter aliyasema hayo leo Agosti 8, 2019 wakati akitoa tathmini ya ushiriki wa Mfuko huo katika maonesho ya mwaka huu ambayo yamefikia kilele leo.
“Lengo letu la kushiriki maonesho haya lilikuwa ni kutoa elimu kwa wadau wetu ambao ni waajiri, wafanyakazi na wananchi kwa ujumla kuhusu shughuli za Mfuko hususan mafao yanayotolewa na Mfuko na namna ya kuwasilisha madai ya fidia. Jambo ambalo tumejifunza kwa wengi waliotembelea banda letu hususan wafanyakazi walitaka kuelimishwa ni hatua zipi za kuchukua ili kudai fidia pindi wanapoumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi.” Alisema. Napenda kusisitiza kuwa wafanyakazi wanapopata ajali inayotokana na kazi watoa taarifa mapema kwa waajiri wao watakao wajazia fomu maalum ya kutolea taarifa ya ajali ambayo itawawezesha kupata matibabu stahiki kwa wakati na kuutaarifu Mfuko kuhusu ajali husika. Wanapokwenda kupata matibabu wahakikishe fomu za matibabu zinazotolewa na WCF zinajazwa kikamilifu na madaktari na waziwasilishe WCF pamoja na nyaraka za utambulisho kadiri inavyoelekezwa na Mfuko. Jambo ambalo tunapenda kila mfanyakazi na mwaajiri azingatie ni kwamba taarifa za matukio au madai ya ajali, ugonjwa ama kifo lazima iwasilishwe katika Mfuko ndani ya miezi 12 toka tukio la ajali, ugonjwa ama kifo lilipotokea.
Alisema katika kuboresha huduma za Mfuko kwa wadau wake, WCF inaendelea kufungua ofisi zaidi mikoani na ipo katika hatua za mwisho kuzindua mfumo wa kuwasilisha madai kwa njia ya mtandao kwani hii itasogeza huduma za Mfuko karibu zaidi wadau hasa wafanyakazi na waajiri.
Alitoa mfano wa mfanyakazi mmoja ambaye aliumia wakati akiwa kazini na kukatika vidole vitatu vya mkono wa kulia aitwaye Bw. Kurya Shamoga ambaye alitembelea maonesho ya Nane nane na alipoona banda WCF alifurahi sana na kuanza kueleza jinsi WCF ilivyoshughulikia matibabu yake hadi kupona, mkononi alikuwa ameshika fomu ya kufungua akaunti ya benki baada ya kutakiwa kuwasilisha akaunti WCF ili malipo yake ya fidia ya kudumu yaweze kufanyika.
 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (kushoto), akimkabidhi kombe la ushindi wa kwanza, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Anselim Peter baada ya kuibuka kidedea kundi la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwenye kilele cha maonesho ya Nanenane viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu leo Agosti 8, 2019.
 Bw. Peter akiungana na kikosi kazi cha WCF kilichokuwa kimeweka kambi Nyakabindi kutoa elimu ya Fidia kwa Wafanyakazi baada ya kubeba kikombe na cheti cha ushindi wa tatu.
Mkurugenzi wa Uendeshaji Mkuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Anselim Peter kwa furaha akiwa amekamata kikombe na cheti cha ushindi wa kwanza kundi la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kwenye kilele cha maonesho ya Nanenane kitaifa viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu Agosti 8, 2019.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...