Na Said Mwishehe, Globu ya Jamii.

KABLA ya kuendelea naomba nieleze kitu kimoja nacho ni hiki. Eti kuishi kwingi kuona mengi. Sawa nimekubali kuishi kwingi ni kuona mengi. Ni kweli kuna mengi tunayaona. Nafahamu aliyeishi kwa zaidi ya miaka 60 ameona mengi zaidi kuliko aliyeishi miaka 20.

Hivyo sipingani na usemi wa wahenga wa kuishi kwingi kuona mengi. Hata hivyo swali ambalo najiuliza hayo mengi ya kuyaona kutokana na kuishi kwingi kwako ndio haya?

Kama  binadamu nikiri kuna mengi mazuri ambayo macho yangu yameyashuhudia. Mengi ambayo nimeyaona yanavutia,yanafurahisha na mengi yanafundisha pia.
Ni bahati mbaya katika huko huko kuishi kwingi na kuona mengi nako kumesababisha tunashuhudia na kuyaona ambayo hata shetani ambaye amekuwa akihusishwa na mabaya yooote ya dunia,  hayampendezi.

Kuishi kwingi sasa macho yameanza kushuhudia ukatili unaondelea nchini Afrika Kusini, Raia wa Afrika Kusini wanaua Waafrika wenzao bila woga, Wanaua bila huruma.Wanawachoma moto Waafrika wenzao kama wanachoma karatasi.

Nakubali kuishi kwingi ni kuona mengi lakini siko tayari kuona haya yanayoendelea Afrika Kusini yakaendelea kushuhudiwa na macho ya walio wengi.

Kama kuishi kwingi ni kuona mengi na mengi yenyewe ndio hayo ya Afrika Kusini, lazima tuseme hapana. Afrika ni moja, hivyo ni wajibu wetu kudumisha upendo , umoja na mshikamano.

Kupitia mitandao ya kijamii, luninga na redioa tunapata habari mbalimbali kuhusu yanayoendelea nchini Afrika Kusini.Wenye kutekeleza mauaji hayo wanadai kuwa wanafanya hivyo kutokana na ajira zao kuchukuliwa na wageni (Waafrika wenzao).

Wengine wanadai kuwa wanafanya mauaji hayo kwasababu wanaishi maisha magumu kwasababu tu wageni yaani Waafrika wenzao wanaishi vizuri kuliko wao na hiyo kwao hawako tayari.

Wanavamia maduka, wanapora mali na kufanya kila aina ya ukatili.Kweli kuishi kwingi ni kuona mengi lakini jamani tukubali, hiki sicho ambacho Afrika tunataraji kukiona.
 Nimekuwa nikiangalia mara kwa mara picha na  video zilizopo kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha ukatilii unaofanywa na baadhi ya wananchi wa Afrika Kusini dhidi ya wageni.

Kwa kweli inaumiza, inasikitisha, inahuzunisha na wakati mwingine nimebaki najiuliza hivi ni kweli Afrika tumefika mahali ya kuchukiana sisi kwa sisi?Siamini na nina jipa moyo hatujafika huko.

Kuna mahali niliona mtu ameandika kuwa kinachoendelea Afrika Kusini kitamalizwa na Waafrika Kusini wenyewe na hasa viongozi wa Serikali.Kwa ujinga wangu na kutofahamu mambo kwa kina au kutokana na uelewa mdogo naamini hili si la kumalizwa na Afrika Kusini peke yake bali ni la Afrika yote.


Ndio raia wa Afrika Kusini hawauani wenyewe kwa wenyewe bali wanaua Waafrika wenzao. Hivyo ni matukio ambayo yamevuka mipaka. Nigeria imekuwa mhanga kwenye mauaji hayo.Tumeona nao ambavyo wameamua kulipiza kisasi kwa kuvamia maduka ya Waafrika Kusini yaliko kwenye nchi yao na kuyachoma moto.
Afrika hatupaswi kufikia hatua hiyo.Hatuna sababu ya kuumiza sisi kwa sisi.Ni utamaduni wa hovyo na tunapaswa kuutakaa kwa nguvu zetu zote wana Afrika.

Wakati naendelea kutafakari ya Afrika Kusini na ukatili unaoendelea dhidi ya wageni nikakumbuka wimbo wa Bob Marley wa Africa Unite(Afrika tuungane)Ni wimbo wa miaka mingi na ujumbe wake ulikuwa mkubwa sana.

Kwa bahati mbaya wachache kati yetu tumesahau nia njema ya kutaka kuliunganisha Bara la Afrika.Bob Marley aliona mbali na matarajio makubwa kwa Waafrika.

Leo hatunaye mwanamuziki huyo maana alishatanguliza mbele za haki miaka mingi.Kama kuishi kwingi ni kuona mengi Bob Marley asingekubali kushuhudia haya yanayoendelea Afrika Kusini.

Sote tunafahamu kazi kubwa ambayo imefanywa na viongozi wa Bara la Afrika kwa nyakati tofauti miaka ya nyuma. Viongozi wa nchi mbalimbali za Afrika mkakati wao namba moja ilikuwa ni kuziunganisha nchi za Afrika.

Wengi wameshiriki na kufanya vikao mara kadhaa vya kuiunganisha Afrika.Inasikitisha kuona waliopo sasa wanasahau namna ambavyo waasisi wa nchi hizo wametumia muda mwingi kuikomboa Afrika.

Tunafahamu kuna nchi nyingi za Afrika zilijitoa kwa hali na mali kuhakikisha Afrika Kusini inakuwa huru.

Nitoe rai kwa raia wa Afrika Kusini kama wataona hiki nilichoandika, waache kufanya ukatili huo.

Ni ukatili ambao hata sheteni hawezi kukubali pamoja na ufedhuli wake wote wa hapa duniani.Umoja wa Afrika umetoa tamko la kulaani mauaji hayo.Ni hatua nzuri.

Ni majuzi juzi tu nchi za Kusini mwa Afrika zimetoka kwenye mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika(SADC).Moja ya makubaliano yao ni kuhakikisha nchi za jumuiya hiyo zinajikita katika uwekezaji wa viwanda.Wakakubaliana kufunguliwa kwa milango ya kibiashara na uwekezaji.

Swali dogo tu tena la kipuuzi kwa kinachoendelea Afrika Kusini nani anaweza kuwekeza kwa sasa.Ndio maana naona haja ya viongozi wa Bara la Afrika kuzungumza na kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

Najua wapo wanaoweza kusema sina cha maana nilichoandika lakini ukweli utabaki pale pale na ukiweza kuchukua hili tu Afrika Kusini kinachoendelea hakifurahishi wengi.

Najua katka masuala ya diplomasia kuna lugha zao za kuonesha hakuna tatizo.Akina sie tusio wana diplomasia tunasema hakuko sawa na ni wakati wetu Waafrika kusema hapana.Kibaya zaidi si mara ya kwanza kutokea kwa matukio hayo.Unaweza kujiona uko salama leo lakini kesho ikawa zamu yako.Tuchukue tahadhari kabla ya hatari.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...