Mbunge wa Mtama Nape Nnauye akipeana mkono na Rais Dkt. John Magufuli mara baada ya kuomba msamaha leo Ikulu jijini Dar es Salaam.

Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MBUNGE wa Mtama Nape Nnauye amemwambia Rais Dkt. John Magufuli kuwa hakuwa na amani, wala hakuwa anapata usingizi lakini sasa moyo wake unaamani na atalala usingizi.

Nape ameyasema hayo leo Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na Rais na kufanya naye mazungumzo ambayo kwa sehemu kubwa ilikuwa ni kumuomba msamaha Rais kwa mambo yaliyotokea siku za karibuni.

Akizungumza mbele ya Rais Magufuli akiwa Ikulu leo Septemba 10, 2019 jijini Dar es Salaam Nape amesema kuwa "Leo nimefurahi sana kumuona baba yangu, Mwenyekiti wangu wa CCM na Rais wangu. Baada ya kumuomba msamaha na kunisamehe hakika moyo wangu unaamani kubwa, nilikuwa sipati usingizi, ilifika mahali naamka saa nane ya usiku  usingizi unakata, leo nitalala na nina amani moyoni," amesema Nape.

Amefafanua "Mimi kama mtoto wa CCM, kama mwanaye nikasema ni vizuri nije niongee na baba yangu ,amenipa fursa ya kuja kuniona, ameniambia amenisamehe na amenipa fursa kubwa.

"Kwa hiyo mheshimiwa Rais kama baba yangu, kama mzee wangu nashukuru kwa fursa uliyonipa na pia  kwa kunisikiliza, kwa kunisamehe, pia kwa kunishashauri na kunielekeza ninafanyaje huko mbele ninako kwenda."

Wakati Nape anajiandaa kuondoka Ikulu akiwa ameshikana mkono na Rais Magufuli na kumwambia hakuwa anapata usingizi na moyo wake haukuwa na amani lakini sasa anayo amani moyoni mwake baada ya Rais kumsamehe.

Rais Magufuli baada ya kumsikiliza Nape, amesema hivi "mimi nishamsemehe, nimemsamehe kwa dhati  ya moyo wangu, Nape amekuwa hata akiandika meseji nyingi, ameshaandika meseji ya kuomba msamaha saa nane usiku.

"Amekuwa akiniomba msamaha, na ukiangalia meseji zake unaona kabisa huyu mtu anaomba msamaha. na leo aliniomba aje anione na hata wasaidizi wangu wamekuwa wakipata hiyo habari, amejaribu kwenda kwa mzee Mangulla, kwa mzee Apson na amefika mpaka kwa mama Maria Nyerere." ameeleza Rais Magufuli.

"Amehangaika kweli lakini sisi tumeumbwa kusamehe, na leo umemuoana asubuhi amekuja, nikasema siwezi kuzuia kumuoana. Nikasema ngoja niache shughuli zangu na kubwa zaidi, ameniambia baba nisamehe." amesema Rais

"Kusamehe kunaumiza lakini nasema kwa dhati kabisa nimemsamehe, nimesamehe kabisa. Ameeleza yaliyokuwa yanamsibu lakini pia ameeleza watu waliokuwa wanamhubiri, wengine wako kwenye chama.

"Lakini nimesema yote nimemsamehe, huyu bado ni kijana mdogo na ana maono mazuri katika maisha yake, nikiendelea kumshikilia kwenye moyo wangu kwanza ni dhambi kubwa kwa Mwenyezi Mungu na tumefundishwa katika maandiko yote kusamehe saba mara sabini.

"Mungu amsaidie katika shughuli zake, akafanye kazi vzuri, akalee mke wake na familia yake, akakitumie chama, akawatumikie wananchi wa jimbo lake," amesema Rais Magufuli na baada ya maelezo hayo Nape alimwambia Rais hakuwa na amani katika moyo wake.

Hata hivyo Rais Magufuli alimuuliza  hakuwa na amani? Nape akajibu ndio, na wakati mwingine hakuwa anapata usingizi. Wakati anaondoka Rais alimshauri Nape awe anasali sana na kumuomba Mungu, ambapo Nape naye akasikika akimueleza Rais kuwa anasali. Baada ya hapo kicheko kikachukua nafasi yake na Nape akaondoka Ikulu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...