Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amevitaka vyama vya msingi vya ushirika mkoani Rukwa kuhakikisha wanalipa madeni wanayodaiwa na wadau wa kilimo ikiwemo mabenki pamoja na wauzaji mbalimbali wa pembejeo ili wadau hao waweze kuendeleza uaminifu na hatimae kuwa na mahusiano mazuri yatakayoleta maendeleo ya wananchi katika mkoa.

Amesema kuwa kutolipa madeni chama kinajiweka katika mazingira ya kutokopesheka na wadau kukosa uaminifu hata kwa vyama vingine na kunasababisha wadau hao kushindwa kufikisha huduma kwa wakulima na hatimae kilimo kukosa tija, vyama vya ushirika kuyumba na kuongeza kuwa dawa pekee ya kukopa ni kulipa.

“ Vyama vya Msingi vina madeni tena madeni makubwa, kwa mfanokuna kile chama cha Katazi AMCOS pamoja na Rukwa Farmers vyote vipo kule Wilaya ya Kalambo vinadaiwa shilingi milioni 395, vyama viwili sijajua kwengine lakini pale Mpui wanadaiwa Shilingi Milioni 485 au 490, lakini wao wamejipanga nilikuta mzigo mkubwa sana wa mahindi, tani zaidi ya 600, na waliniambia deni wanamaliza, lakini vile vyama viwili hata mahindi yaliyoko kwenye maghala yalikuwa hayazidi magunia 250 sasa watalipaje deni, ukiuliza wanasema kwamba hawakupata mavuno ya kutosha, lakini nje ya hapo wanauza” Alieleza.

Hivyo alitoa rai kwa vyama vya ushirika kuliangalia jambo hilo kwa karibu kwa kuchambua vyama vyote vinavyodaiwa, wadau wanaowadai, siku waliyokopa na siku wanayotakiwa kurudisha mikopo, aina ya mikopo, walichorejesha tangu kukopa ili kuwa na orodha kamili na kuwafuatilia katika urejeshaji wa mikopo hiyo kwani kwa kufanya hivyo watajenga Imani kwa wanaowakopesha na hatimae kukopesha zaidi.

Mh. Wangabo aliyasema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Ufipa Cooperative Union Ltd (UCU) katika mkutano uliowajumuisha wadau wa kilimo katika mkoa ili kuona namna ya kuinua kilimo chenye tija pamoja na kuhuisha ushirika ndani ya mkoa.

Aidha, Wakati akiwasilisha mada yake kwa wakulima Meneja wa Benki ya Manedeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Kanda ya Nyanda za juu Kusini Dickson Pangamawe alisema kuwa viongozi wa shirika ndio nguzo ya wanaushirika, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha kuwa wanachama wanafaidika na ushirika huo na kuhakikisha kuwa mikopo wanayoipata inawafikia wakulima wao.

“ Nyinyi ndio mtakaotujengea uamini kule kwa wakulima, sisi kama benki ya kilimo tuna fursa ya mikopo ya aina zote, kama wakulima wapo ‘serious’ na uongozi wao utasimama imara, tutawakopesha wataweza kufanya shughuli zao za kilimo bila ya shida yoyote, kwahiyo nitoe rai kwa viongozi wa ushirika, mara nyingi kumekuwa na shida na wakulima wanashindwa kuwa waaminifu kwasababu wanashindwa kusimamiana vyema katika vyama vyao, kwahiyo nyie muwe imara ili kuturuhusu sisi tuweze kuwawezesha,” Alisisitiza.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Sumbawanga Abdillahi Nyangasa alishauri kuwa ili wakulima waweze kujikomboa alitaja mambo matatu makubwa ikiwemo Fedha, Masoko na Mkulima mwenyewe na kuongeza kuwa wao kama NFRA wanasimama katika kumhakikishia mkulima masoko na hivyo wakulima wanahitaji fedha za mikopo kutoka katika mabenki na wao kuwa tayari kutumia fedha hizo kwaajili ya manufaa ya kilimo chao.

“Mtazamo wa NFRA ni kuwafanya Wana Rukwa na Watanzania wengine tubadilike tuwe na uwezo wa kuuza bidhaa zetu za mazao ndani na nje ya nchi, bahati nzuri mkoa umeshaweza kulichukua hili na kulifanyia mkakati kwa maana ya ndugu zetu maafisa ugani, kazi ianzie shambani, tuna kiwango kikubwa sana tunachokipoteza cha mahindi tunayolima kwa hatua ya mwisho ya ubora, asilimia 30 mpaka 40 wakati mwingine mazao yanaharibika kwasababu ya kutozingatia kilimo chenye tija,” Alisitiza. 

Mkoa wa Rukwa una matrekta 124 yanayomilikiwa na wakulima binafsi hali iliyopelekea Mh. Wangabo kuvitaka vyama vya ushirika kusimamia kauli mbiu yao ya “ Ushirika, Pamoja tujenge uchumi” kwa kuanza na kumiliki matrekta ili kuwawezesha wanachama wao waweze kulima kwa tija na kuongeza mazao na sio kutegemea kilimo cha majembe au kutumia wanyama.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...