Na: Moshy Kiyungi,Tabora.

Humu nchini walikuwapo wanamuziki wengi waliotingisha katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva, wengi wao wamefifia ama hawapo tena kimuziki.

Harmonize ndilo jina linalotajwa kila kona kwa kwa kipindi hiki kwa jinsi alivyoweza kukonga nyoyo za wapenda muziki huo.

Maudhui katika nyimbo zake zimepelekea kualikwa kwenye shughuli kubwa za Kitaifa, ambako amekuwa akiwanyenyua vitini baadhi ya viongozi wakubwa, wakimtuza pamoja na kucheza naye.

Mfano halisi ni kwenye sherehe za kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere zilizofanyika mjini Lindi Oktoba 14, 2019.

Harmonize alifanya ‘kufuru’ kwa wimbo wake amkisifia Rais John Pombe Magufuli kwa mambo makubwa ya maenedeleo ya nchi yaliyafanywa kwa kipindi kifupi na serikali ya awamu ya tano chini.

Aliwainuwa vitini baadhi ya viongozi akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, walioingia uwanjani kusakata muziki sambamba na msanii huyo.

Wakati huohuo rais Magufuli alikuwa akifurahi, baadaye akampongeza Harmonize, pamoja na kumshawishi kugombea ubunge jimbo la Tandahimba.

Baada ya ushawishi huo Harmonize mwenyewe amepokea kauli hiyo kwa mikono miwili.

Kuipitia ukurasa wa wake wa mtandao wa Instagram, Harmonize amemjibu rais kwa kusema…Thanks a lot…!!! My President…!!! Doctor John Pombe Magufuli Kama ilivyo Ada Ya kwamba KaulinYako Tukufu Ni Sheria Nikiwa kama mwananchi wa Kawaida Sinabudi Kutii…!!! Lakini Pia Wananchi wa Wenzangu wa Tandahimba Wameipata .Hii Kauli Yako Tukufu…!!! Bila Shaka Kwapamoja Tunaifanyia Kazi…!!! Mungu Ibariki Tanzania Mungu Ibariki Serikali ya awamu ya tano.

Harmonize ni nani?

Wasifu wa Harmonize unaonesha kuwa mara baada ya kuzaliwa Aprili 15, 1994, katika kijiji cha Chitoholi mkoani Mtwara, alipewa jina la Rajab Abdul Kahali, japo hupenda kujiita ‘Konde Boy’.

Ni mwanamuziki mwenye talanta za kutunga na kuimba nyimbo za miziki ya Bongo Flava pamoja na Afro Pop, wakati mwingine hubofya Piano, pia ni mtayarishaji wa rekodi.

Miaka ya nyuma mkoa wa Mtwara ulitoa wanamuziki waliokuwa wakipiga muziki hususan wa asili ya Kimakonde. Baadhi yao ni kama Halila Tongolaga na Che Mundugwao.

Pia kulikuwa na bendi ya Mitonga Jazz, iliyokuwa ikiwasha moto kwa muziki wa asili hususan katika wimbo wao wa ‘Mariana’.

Katika miaka ya 1990 hadi 2000, tulimshuhudia masanii maarufu wa kucheza na Nyoka, Norbert Chenga, ambaye ni wa kabila la Wamakonde toka Mtwara, aliyekuwa akiongoza kikudi cha Muungano Dancing Troupe cha jijini Dar es Salaam.

Harmonize alianza kuvuma kwa vibao vyake vya kwanza vya Aiyola cha mwaka 2015, Bado cha mwaka 2016, Matatizo ya 2016 na baadaye akatoa nyimbo akishirikiana na msanii mwenzie kutoka lebo moja ya Wasafi Classic Baby (WCB), Diamond Platnumz.

Wimbo wa ‘Kwa ngwaru’ ulibamba karibia maeneo yote ya Afrika ya Mashariki na Kati kabla ya kuachia kibao kingine kiitwacho ‘Inama’ ambacho kiliongezewa nakshi kwa sauti ya mwanamuziki Fally Ipupa toka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Utamu wa radha ya wimbo huo uliongezeka baada ya kumshirikisha msanii kutoka nje ya Tanzania, aitwaye Burna pamoja na Diamond Platnumz.

Harmonize hivi sasa anatamba na kibao kiitwacho ‘Never give Up’, wimbo ambao unaelezea historia ya maisha yake kuanzia alivyo kuwa na maisha magumu sana. Harmonize anasimamiwa na Joel Joseph au kwa jina lingine Mr Puaz.

Maisha ya Awali

Harmonize alisoma katika shule ya sekondari Mkundi iliyopo mjini Mtwara, baada ya kumaliza elimu yake alielekea jijini Dar es Salaam ambako alijishighulisha na shughuli mbalimbali za kumpatia riziki ya kila siku.

Kama wafanyavyo vijana wengi waingiapo jijini Dar es Salaam wasio na mitaji, Harmonize alikuwa akisukuma mkokoteni wenye madumu ya maji akiuza maji. Pia aliuza Kahawa kwa wafanyabiashara wengine na wakazi wa Kariakoo jijini humo.

Alianza kujihusisha na muziki mnamo mwaka 2011, ambapo alitoa nyimbo mbalimbali lakini hazikuweza kupata umaarufu mkubwa, hadi aliapokutana na Diamond Platnumz mnamo mwaka 2015 na kuanza kufanya mziki pamoja naye.
.

Harmonize wakati anaanza kazi ya muziki alitamani kushiriki onesho la Fiesta Mtwara, lakini hakuweza kupata fulsa ya kuperfom.

Alieleza kisa cha kuto kuperfom ni kwamba wakati akiwa njiani kwenda kuangalia Wasanii wenzake wakiperfom kwenye viwanja vya Nangwanda Sijaona, alikutana na kundi la vibaka wakamkaba na kumpora kila kitu.

Mwanamuziki huyo alisema baada ya tukio hilo aliamua kurudi hotelini akiwa amechanganyikiwa kutokana na kuporwa kila kitu ikiwa pamoja na nauli yake ya kurudi Dar es Salaam.

Harmonize alisema baada ya kufikiria sana aliamua kuchukua nguo zake zilizokuwa hotelini, akaamua kuziuza ili aweze kupata nauli ya kurudi Dar es Salaam.

Akiwa mjini Mtwara alipatiwa namba ya simu ya Diamond Platumz na mmoja wa watangazaji mjini humo ili akirejea Dar es Salaam, amtafute ili aweze kumsaidia kimuziki.

Harmonize alisema hakuamini siku alipomtumia ujumbe Diamond, naye hakusita kumjibu kuwa amekubali kumsaidia pamoja na kumpatia malazi nyumbani kwa Diamond huko Tegeta jijini Dar es Salaam.

Kabla ya sauti yake kutambulika mitaani, baadaye alichukuliwa na lebo ya Diamond Platnumz ijulikanayo kama WCB (Wasafi Classic Baby).

Harmonize akatokea kuwa mtu wa karibu sana na bosi wake Diamond, hadi kutuhumiwa kumuiga kwa kila kitu kuanzia kuongea, kucheka, kuimba, kucheza napozi mbalimbali.

Lakini yeye alitumia muda mwingi kujitetea kwamba hamuigi kwa kila kitu kama wanavyodai watu, lakini alikubali kuwa alikuwa akimkubali sana Diamond Platnumz huku akimuita ‘Bigi’.

Kwa sasa Harmonize kajiengua katika lebo hiyo kutokana na sababu ambazo hazijawekwa wazi. Lakini baada ya kuvunja mkataba na Wasafi Classic Baby (WCB), Harmonize alitakiwa kulipa shilingi milioni 500, ili kupata haki zake zote kutoka mikono ya Wasafi.

Kwa mujibu wa Harmonize, masharti ya kuvunja mkataba yapo katika makundi mawili. La kwanza, ni kulipa shilini milioni 500. Pili kama ataondoka kama yeye, asitumie jina la Harmonize pamoja na nyimbo ambazo msanii huyo alirekodi akiwa WCB.

Imefahamika kwamba mara atakapotoa kiasi hicho cha shilingi nusu bilioni, ataweza kutumia jina la Harmonize, haki ya kutumia nyimbo zake zote alizorekodi chini ya lebo hiyo, video alizofanya chini ya lebo hiyo ya Wasafi na kadharika.

Harmonize yaelezwa kwamba amelazimika kuuza nyumba zake tatu ili kupata ‘mkwanja’ huo ili wamalizane na WCB, naye kuwa huru.

Kujiengua kwa Harmonize katika lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), mtayarishaji wa muziki kutoka studio ya Wasafi, Lizer Classic, alitamka wazi kummisi msanii huyo aliyejitoa katika Lebo ya WCB, akaenda kuanzisha lebo yake ya Konde Gang.

Alisema kuondoka kwa Harmonize katika lebo hiyo, ni pengo kubwa kwakuwa ni mmoja wa wasanii ambao aliwazoea zaidi ambaye walianza pamoja toka chini. 

Baadhi ya nyimbo alizoachia Harmonize ni pamoja na Aiyola ya mwaka 2015, Bado aliyomshirikisha Diamond Platnumz ya mwaka 2016, Matatizo ya mwaka 2017, na Happy Birthday ya mwaka 2017.

Zingine ni Shula, Niambie, Don’t go, Nishachoka, Sina, Nakupenda zote za mwaka 2017.

Mwaka 2018 Harmonize alitoka na nyimbo za Kwa ngwaru aliyomshirikisha Diamond Platnumz, Dm Chick, Atarudi na Paranawe wimbo alimshirikisha msanii Rayvanny wa mwaka 2018.

Hamrmonize aliachia nyimbo za Niteke, Show me What you Gat, aliomshirikisha msanii Yemi Alade, Kainama alimshirkisha Diamond Platnumz na Burna boy, Ndoenda na Never give Up za mwaka 2019.

Alibaisha kuwa jina lake halisi anaitwa Rajab, lakini jina la Harmonize alipewa na Producer wa Record Lebel pamoja na mashabiki zake.

Harmonize alifika jijini Dar es Salaam mwaka 2009 alipohitimu kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Mkundi iliyopo Mtwara. Baada ya kuwasili hakuwa na shughuli ya kufanya, akajikita katika uuzaji wa Chai na Kahawa maeneo ya Kariakoo. Baadaye alifanya biashara Umachinga wa kuuza nguo na vitu mbalimbali.

Harmonize alianza harakati za muziki mwaka 2011, alishawahi kurekodi nyimbo katika studio lakini hazikuwa na ubora wa kupeleka katika vituo vya redio na kusambaza kwa watu.

Katika kipindi cha miaka minne aliyoingia katika maswala ya muziki, ilimuwezesha kujifunza kiasi pamoja na changamoto ya kubanwa na biashara zake, akashindwa kujisimamia vizuri katika mambo ya muziki.

Harmonize hakukata tamaa, alianza kutafuta Meneja kwa kumsimamia kazi zake miaka miwili kabla ya kukutana na uongozi wa WCB ambao uliompokea vizuri.

“Nimesha rekodi nyimbo nyingi ndani ya lebo ya Wasafi, nimeona nianze kwanza na Aiyola huu uwe mwanzo wangu, pia nimejifunza vitu vingi kutoka kwa lebo ya WCB, kutoka kwa msanii Diamond Platnumz” alitamka Harmozize.

Kwa upande wa historia ya mnaisha yake inaonesha kufanana na ya meneja wake Diamond, kwa kuona umuhimu wa kusaidia vijana wengine ndiyo maana akafungua studio nyumbani kwake na kuweza kutoa vipaji kwa vijana tofauti tofauti.

Harmonize amefunguka na kusema kuwa uongozi wake wa WCB, ulipomtaka kumtanguliza kama chambo alidhani wamedhamiria kumpoteza katika ramani ya muziki, ndiyo maana hawakutaka kuutambulisha kwenye radio na televisheni kitu ambacho kimezoeleka.

"Unajua mimi katika WCB nilikuwa kama chambo kwa sababu hata lebo ilipoanzishwa mimi ndiye niliyekuwa msanii wa kwanza kusaini, nikafanya vizuri wengine wakafuatia.

Hata hivyo kwenye mauzo ya muziki kwenye mtandao nimetangulizwa mimi, namshukuru Mungu kazi zimepokelewa vizuri. Uongozi ulikuwa na mtazamo chanya tofauti na nilivyowaza". Alisema Harmonize.

Msanii huyo alisema baada ya kiongozi wa lebo hiyo Diamond Platnumz kutoa albam, yeye alidhamiria kuomba uongozi wake ili afanye hivyo, kwakuwa aliaibika sana alipofika Marekani alipoulizwa yeye anazo album ngapi kama msanii, akakosa jibu.

"Nilipokuwa Texas nchini Marekani, mdada mmoja aliniambia kuwa mimi ni msanii kutoka Tanzania, akaniuliza mpaka sasa nina albamu ngapi? nikashindwa kumjibu, hii ilikuwa ni aibu nikabaini kwamba ukiwa na albamu kadhaa lazima watu wakuheshimu" aliongeza Harmonize.

Kila la heri Harmonize unayo mengi ya kufanya katika tasnia hiyo, usikate tamaa wala kusikiliza maneno ya watu ‘chapa kazi’.


Mwisho.

Makala hii imeandikwa kwa msaada mkubwa wa mitandao.
Mwandaaji anapatikana kwa namba: 0784331200, 0713331200, 0767331200 na 0736331200.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...