Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema itatangaza orodha ya kwanza ya majina ya wanafunzi walioomba na kupangiwa mikopo Alhamisi, Oktoba 17 mwaka huu.

Hatua hiyo inafuatia kukamilika kwa kazi ya uchambuzi wa maombi ya mikopo yapatayo 55,444 ya wanafunzi ambao wamepata udahili katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake jijini Dar es salaam leo (Jumatatu, Oktoba 14, 2019), Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema wanafunzi watakaopangiwa mikopo wataweza kupata taarifa zao kupitia akaunti zao kwenye mtandao wa taasisi hiyo.

Pamoja na kutangaza orodha hiyo, Badru amesema HESLB pia imeamua kutoa fursa kwa waombaji 4,794 ambao bado hadi sasa hawajakamilisha maombi yao kukamilisha kwa kuambatisha nyaraka muhimu mtandaoni.

“Tulitoa siku sita ambazo zinakamilika kesho, Oktoba 15, lakini bado kuna hao ambao tunawaona katika mfumo kuwa bado hawajakamilisha … inawezekana wapo ambao hawahitaji tena mkopo, lakini inawezekana wapo wahitaji wa kweli … kwa hiyo tumeamua hatutafunga mfumo wetu na wanaweza kuendelea kukamilisha,” amesema Badru.

“Wanaweza kuingia katika akaunti zao na kukamilisha, lakini kwa wale ambao watafika vyuoni wakiwa bado hawajakamilisha, tunakutana na maafisa mikopo Ijumaa wiki hii mjini Morogoro na wawahudumie wanafunzi hawa wakiwa vyuoni kwa kupokea nyaraka zinazokosekana na kuziwasilisha kwetu ili wote wenye uhitaji wapangiwe mkopo,” ameongeza Badru.

Kwa mujibu wa Badru, utoaji wa mikopo pia huzingatia makundi maalum kama yatima waliowasilisha nakala za vyeti vya vifo vya wazazi, wenye ulemavu walioambatisha barua kutoka kwa waganga wakuu wa wilaya au mkoa na waombaji mkopo ambao kutokana na hali duni ya kiuchumi, walifadhiliwa katika masomo yao ya sekondari au stashahada.

Kuhusu malengo ya mwaka huu wa masomo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB amesema Serikali imetenga TZS 450 bilioni ambazo zitawanufaisha jumla ya wanafunzi 128,285. Kati yao, wanafunzi zaidi ya 45,000 watakuwa ni wa mwaka wa kwanza na wengine 83,285 ni wanufaika wa mikopo wanaoendelea na masomo. Bajeti ya mwaka wa masomo 2018/2019 ilikuwa TZS 427.5 bilioni na iliwanufaisha jumla ya wanafunzi 123,329.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya Juu HESLB Abdul-Razaq Badru akizungumza na waandishi habari kuhusiana na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya Juu jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...