Na Veronica Simba – Tanga
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), itatoa vyeti maalum
kwa wakandarasi wa miradi ya umeme vijijini, watakaokamilisha kazi kwa
wakati na viwango stahiki, ili kuwapa motisha na utambuzi utakaowapa
sifa ya kupewa tenda nyingine mbalimbali na Serikali.
Hayo yalibainishwa Oktoba 22, 2019 jijini Tanga, na Mwenyekiti wa
Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini
(REB), Mhandisi Styden Rwebangila, akiwa katika ziara ya kazi kukagua
utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, mkoani humo.
Mhandisi Rwebangila ambaye aliambatana na wajumbe kadhaa wa Bodi
husika pamoja na wataalamu kutoka Wakala huo, alisema baada ya kukagua
magenge na ghala la vifaa vya Mkandarasi Derm Electrics (T) Ltd katika
wilaya za Handeni, Korogwe, Kilindi na Lushoto, wameridhishwa na kazi
yake lakini wakamtaka asibweteke bali aendeleze jitihada ili
akamilishe kazi kwa wakati.
“Kama akiendelea hivi, basi atakuwa ni miongoni mwa watakaopata vyeti
maalum vya utambuzi kutoka REA,” alisema Rwebangila.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka REA, Mhandisi Jones
Olotu, ametoa wito kwa wakandarasi wote 16 wanaotekeleza miradi ya
umeme vijijini, awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza, kuhakikisha
wanawaunganishia umeme wateja katika maeneo yao wakiwemo wale wasio na
uwezo wa kugharamia utandazaji mfumo wa nyaya katika nyumba zao.
Olotu alisema, siyo lazima mwananchi afunge mfumo wa nyaya ili
kuunganishiwa umeme kwani kuna njia mbadala ya kutumia kifaa cha Umeme
Tayari (UMETA), ambavyo kila Mkandarasi amepatiwa 250 kwa kila eneo
analotekeleza kazi kwa ajili ya kuwafungia wananchi wenye uhitaji.
“Natoa wito kwa wakandarasi wote husika; Mteja yeyote ambaye yuko
ndani ya wigo, kama hajafanya ‘wiring’, afungiwe UMETA, awekewe balbu
tatu na ashauriwe kufanya ‘wiring’ taratibu. Atakapokamilisha,
atabadilishiwa mfumo,” alisisitiza.
Kamati hiyo ya Ufundi ya Bodi ya REA, imeanza mzunguko wa pili wa
ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali inakotekelezwa miradi ya umeme
vijijini, hususan mahali ambako utekelezaji unasuasua, ili kujua
kulikoni pamoja na kutafuta ufumbuzi wake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REB), Mhandisi Styden Rwebangila (kushoto), akikagua moja ya transfoma katika ghala la Mkandarasi Derm Electrics (T) Ltd, anayetekeleza mradi wa umeme vijijini mkoani Tanga. Wa pili kutoka kulia ni Mjumbe wa Bodi hiyo, Louis Accaro na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu. Timu hiyo ilikuwa ziarani mkoani Tanga, Oktoba 22, 2019.
Matukio mbalimbali wakati Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa
Wakala wa Nishati Vijijini (REB), ilipofanya ziara katika Wilaya
mbalimbali za Mkoa wa Tanga, Oktoba 22, 2019, kukagua utekelezaji wa
miradi ya umeme vijijini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...