SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa wito kwa wajasiriamali wote nchini kupeleka bidhaa zao ili ziweze kuthibitishwa ubora wake na shirika hilo bure, kwani gharama zote zimeishalipwa na Serikali.

Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Yusuf Ngenya, wakati wa hafla ya kukabidhi vyeti na leseni 94 kwa wazalishaji wakubwa, wa kati na wadogo ambao bidhaa zao zimethibitishwa na Shirika hilo na kukidhi matakwa ya viwango vya ubora kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba, mwaka huu.

Kati ya vyeti na leseni 94 zilizotolewa, vyeti 25 vilitolewa kwa wajasiriamali wadogo ambao bidhaa zao zimekidhi matakwa ya viwango.

Dkt.Ngenya, alisema vyeti na leseni zilizotolewa zitawasaidia wazalishaji hao kuongeza imani kwa watumiaji, kwani wanapoona alama ya ubora ya tbs watumiaji wanakuwa na imani kubwa na bidhaa husika, hivyo kupanua soko.

Alisisitiza kwamba bidhaa zinapokuwa zinathibitishwa ubora na shirika hilo, bidhaa hizo zinakubalika moja kwa moja sokoni, zinahimili soko la ushindani na kuingia kifua mbele katika soko la nchi za Afrika Mashariki.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, inaendelea kuwahudumia wajasiriamali kuthibitisha ubora wa bidhaa zao bure, hivyo alitoa wito kwa wajasiriamali  kujitokeza kwa wingi kuthibitisha ubora wa bidhaa zao kwa kuwa gharama zote zinalipwa na Serikali.

Dkt. Ngenya aliishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwahudumia wajasiriamali kuthibitisha ubora wa bidhaa zao.

Dkt.Ngenya aliwahimiza wajasiriamali kuhakikisha wanazalisha bidhaa zenye ubora na Watanzania kuanza kupenda bidhaa za ndani ambazo zimethibitishwa ubora.

"Watanzania tununue bidhaa zenye ubora kuangalia alama ya tbs  hii itatufanya tuingie katika Tanzania ya viwanda kwa kupenda vya kwetu," alisema

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa kutoka Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), Ridhiwani Matange, alisema kazi inayofanywa na Shirika la TBS ni nzuri inajaribu kuweka nchi katika hali ya  usalama kwenye bidhaa mbalimbali.

Naye Mhandisi Cdi Nyakwela kutoka Kampuni ya Plasco wazalishaji wa Makaravati ya Plastiki ,alisema vyeti  hivyo walivyopatia  vitawasaidia kupata soko kubwa ndani na nje ya nchi.

Alisema kutokana na bidhaa hizo kuwa mpya watahakikisha wanajitangaza ili Watanzania waweze kuona kasi ya ujenzi wa Tanzania ya viwanda inavyokuja na teknolojia mpya.

"TBS wametupatia leseni ya ubora ni jukumu letu sasa kuhakikisha tunazalisha makaravati ya plastiki yenye ubora na viwango kinachotakiwa na sio kufanya ujanja ujanja," alisema Mhandisi Nyakwela

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...