Hafsa Omar - Dodoma

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wametoa maoni mbalimbali kwa Wizara ya Nishati, kuhusu kuanzishwa kwa ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (ISA).

Walitoa maoni hayo Dodoma, Novemba 12, 2019 wakiwa ni sehemu ya wadau wa sekta husika ili kuboresha Mkataba huo kabla haujawasilishwa kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Novemba 14 mwaka huu ili kuomba uridhiwe.

Akifafanua hoja mbalimbali zilizowasilishwa na Wajumbe wa Kamati hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Mariam Ditopile, Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani alisema kuwa manufaa ya ISA yanaonesha kuwa ni makubwa zaidi kwa nchi ya Tanzania na yanaweza kuendelea kuwepo kwa kipindi kirefu zaidi.

Waziri alikuwa akijibu hoja kuhusu uhakika wa Tanzania kutojitoa kwenye Mkataba huo kama ambavyo imekuwa ikitokea katika baadhi ya mikataba iliyowahi kuridhiwa.

Akieleza zaidi, alisema, Tanzania imekuwa ikijitoa kwenye mikataba kama hiyo baada ya kuona kuwa manufaa ni kidogo ikilinganishwa na majukumu ya uanachama, hata hivyo, alisema kwa upande wa ISA, uwezekano wa kujitoa haupo kutokana na faida ambazo nchi itapata.

Kuhusu hoja kwamba kwanini imechukua muda mrefu kuridhia Mkataba husika tangu uliposainiwa; Waziri alieleza kuwa, ulikuwepo umuhimu wa kufahamu vizuri zaidi mazingira ya utekelezaji wa Mkataba huo na pia kupata uzoefu wa kutosha kutoka nchi nyingine ambazo zilikuwa zimeridhia.

“Kwa sasa inaonekana kuna haja ya kuridhia hasa ikizingatiwa kuwa tayari Tanzania imetengewa Mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 385 kwa ajili ya miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua. Aidha, Tanzania inaendelea kupata nafasi za masomo ili kujenga uwezo wa wataalamu.”

Aidha, Kamati pia ilitaka kufahamu ni kwa namna gani Tanzania imejiandaa katika kuhakikisha inanufaika ipasavyo na ISA, ambapo Waziri Kalemani alieleza kuwa Wizara ya Nishati inaendelea kubainisha maeneo mbalimbali nchini ambayo yanafaa kwa uendelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme wa jua.

Alitaja maeneo ambayo yamebainishwa hadi sasa kuwa ni Manyoni (Singida), Same (Kilimanjaro) na Zuzu (Dodoma).

Vilevile, alifafanua kuwa, ili kunufaika na fedha zilizotengwa, ni lazima upembuzi yakinifu ufanyike. “Hivyo, Wizara kwa kushirikiana na TANESCO, imefanya upembuzi yakinifu wa awali ambapo eneo la Mkwese wilayani Manyoni, limeonekana linafaa kwa ajili ya mradi wa kuzalisha megawati 150 za umeme.

“Umoja wa Ulaya upo katika hatua za mwisho kutoa msaada wa kulifanyia upembuzi yakinifu wa kina, eneo la Mkwese, Manyoni.”Aliongeza kuwa, kutokana na rasilimali kubwa ya jua iliyopo nchini, Wizara inaendelea kuainisha maeneo ambayo yataandaliwa Mpango wa Utekelezaji utakaohusisha upembuzi yakinifu ili kuyaandaa kunufaika na fedha za ISA.

Alisema, mpango wa utekelezaji utakaoandaliwa utahusisha sekta na Nyanja nyingine za matumizi ya nishati jua ikiwa ni pamoja na kilimo na umwagiliaji.

Hoja nyingine iliyoibuliwa ni kuhusu namna gani serikali inawahakikishia wazalishaji binafsi wa umeme hususan wanaozalisha kwa kutumia nguvu ya jua, kuendelea kupata fursa za uwekezaji, katika mazingira ambayo gridi ya Taifa inazidi kusambaa katika maeneo mengi zaidi nchini.

Akitoa ufafanuzi kwa hoja hiyo, Waziri Kalemani alieleza kuwa, serikali inawahakikishia wawekezaji hao kuwa fursa zitaendelea kuwepo kwani yako maeneo ambayo pamoja na uwepo wa gridi ya Taifa, yataendelea kuhitaji umeme mbadala.

Akitaja maeneo hayo, alisema ni pamoja na visiwa mbalimbali nchini ambavyo vitachukua muda mrefu kufikiwa na gridi ya Taifa. Mengine ni katika hospitali, ambazo alisema hata kama zina umeme wa gridi bado zinahitaji umeme mbadala. Pia, katika mitambo mbalimbali ya maji ambayo inahitaji umeme wa gharama nafuu.

Akitoa msimamo wa Kamati, Makamu Mwenyekiti Mariam Ditopile, pamoja na kuipongeza Wizara kwa hatua hiyo, aliiasa kuyatumia makubaliano ya ISA kama kichocheo cha kuupa kipaumbele uzalishaji wa umeme jua nchini ili uzalishwe kwa kiwango kikubwa zaidi nchini ambacho kitaweza kuingizwa katika gridi ya Taifa.

Kwa upande wao, Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu na Katibu Mkuu Dkt Hamisi Mwinyimvua, waliishukuru Kamati kwa ushirikiano na miongozo mbalimbali ambayo wamekuwa wakiitoa kwa Wizara.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akitoa ufafanuzi kwa hoja za Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu kuanzishwa kwa ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (ISA), Novemba 12, 2019. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati, Mariam Ditopile na kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.
 Kutoka kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini Mariam Ditopile, Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt Hamisi Mwinyimvua, wakiwa katika kikao cha kupokea maoni ya wadau (Kamati) kuhusu kuanzishwa kwa ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (ISA), Novemba 12, 2019.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini Mariam Ditopile (katikati), akiongoza kikao cha kupokea maoni ya wadau (Kamati) kuhusu kuanzishwa kwa ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (ISA), Novemba 12, 2019. Kulia kwake ni Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...