Na Said Mwishehe,Michuzi TV
BAADA ya Mbunge wa Kahama Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM), Jumanne Kishimba, kutoa mchango wake bungeni wa kuitaka Serikali kupeleka muswada bungeni utakaomwezesha mzazi kumshtaki mtoto ambaye anakataa kumpatia fedha wala kupokea simu yake wakati , umeibua mjadala mkubwa ndani ya jamii, ambapo baadhi ya wazazi na walezi wameunga mkono mapendekezo yake na kuomba yafanyiwe kazi.

Mbunge Kishimba wakati anachangia Bungeni hoja ya elimu katika mjadala wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021, amesema kuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto,ipeleke muswada bungeni utakaomwezesha mzazi kumshtaki mtoto ambaye anakataa kumpatia fedha wala kupokea simu ya mzazi wake.

Wakati anajenga hoja yake katika hilo Kishimba alisema kuwa mzazi au mlezi ambaye hamsomeshi mtoto wake iko sheria ya kushitakiwa kwa kutotimiza wajibu wake wa kusomesha mtoto lakini hakuna sheria ambayo inaweza kutumika kumshtaki mtoto ambaye ameshindwa kumsaidia fedha mzazi wake au hata kupokea simu, hivyo ameshauri Serikali kuangalia kwa kina suala hilo ili kuwepo na sheria inayotpa nafasi mzazi kumshitaki mtoto asiyesaidia wazazi ambao walitumia fedha nyingi kumlea na kumsomesha tena wengine kwa wazazi kuuza mifugo yao.

Alipokuwa akitoa mchango wake huo wabunge mbalimbali walionekana kufurahishwa kwa kutoa vicheko .Hata hivyo Kishimba alibaki akisimamia hoja yake. 

Akizungumza kuhusu mchango wa mbunge huyo, Damian John (62) amesema amemfuatilia mbunge huyo na mchango na kubaini ana hoja inayoeleweka na hivyo kina kila sababu ya kuiunga mkono na kwamba wabunge wenye mawazo kama ya Kishimb, ndiyo wanaotakiwa kwa sasa kwa sababu wanalenga kupatia ufumbuzi matatizo yanayoikabili jamii.

Ameseam kuna watoto wengi ambao wamesomeshwa na wazazi kwa shida na kujinyima, lakini wanapopata kazi wanajichimbia mijini bila kujua wazazi wao wanaishije vijijini.

Kwa upande wake Adelina Damian (55),yeye amesema amewapongeza wananchi wa Kahama kumpata kiongozi imara, anayejua matatizo ya wananchi na kwamba amekuwa akifuatilia michango yake Bungeni, ni mtu ambaye ana mawazo ya kusaidia maendeleo ya taifa.

"Itakuwa ni jambo la kushangaza iwapo wananchi wa Kahama hawatamchagua tena Kishimba ili kuwaingoza kwenye uchaguzi wa 2020. Kama watoto wangetimiza majukumu yao hata TASAF isingekuwepo," alisema na kuwataka wananchi wa Kahama wasifanye makosa wakati uchaguzi ujao.

Kwa kukumbusha zaidi Kishimba wakati anazungumza bungeni alisema: "Unakuta wazee kijijini wanahangaika na TASAF (mpango wa kunusuru kaya masikini), lakini mtoto ana maisha mazuri Dar es Salaam kila siku anafanya siku ya kuzaliwa,"alisema Kishinmba na kuongeza.Mbona Serikali mwanafunzi anapofikisha kidato cha sita humpatia mkopo wenye riba anaolazimika kuulipa akianza kazi. 

"Mimi nina kosa gani kumdai mwanangu? Kwanini wazazi tujiandae kulalamika na kutoa radhi? Kwanini Serikali isitusaidie? Mwanasheria Mkuu wa Serikali uko hapa. Mwanangu nimemtunza, nimemsomesha kwa nini nijiandae kuja kutoa radhi? Anatakiwa kunisaidia. Niruhusiwe kama hakutoa fedha, hakupokea simu, mimi niende polisi nikamshtaki." Wakati wa mchango wake huo, Kishimba alikuwa akishangiliwa na wabunge wakuonekana kuafikiana naye.

Kishimba ambaye kwenye mchango wake alijikita kwenye suala la elimu, alisema hatuwezi kuondoa elimu ndani ya maendeleo, lazima twende nayo. Kishimba kwenye mchango wake, alijipambanua kwamba anasimama sehemu ya elimu peke yake.

Alisema suala la ajira tusielekeze kuitupia lawama peke yake, lazima tutafute ufumbuzi ambao unaweza kusaidia kuipunguza angalau kwa nusu au kuimaliza kabisa.Kabla ya kuzama kwenye jambo hilo, Kishimba alisema ataanza na utaratibu wa chini wa watoto kwenda shule abusuhi. "Kama hatuna nafasi za kazi ni vizuri tumuombe Waziri wa Elimu, afikirie upya utaratibu huo hasa kwa watu ambao ni wakulima, wafugaji, wafanyabishara ndogo ndogo," alisema Kishimba na kuongeza;

"Watoto wetu wanaondoka asubuhi saa 12 kwenda shule, wanaanza kukimbia mchakamchaka hadi saa 3, hadi kuja kuanza masomo ni saa nne, kwa nini wasiende shule saa tano wakiwa wamefanyakazi nyumbani ambazo tunatarajia kuwarudisha huko wakimaliza vyuo vikuu mheshimiwa Mwenyekiti?"

Alisema kwa kufanya hivyo watakuwa wamefanyakazi nyumbani hadi saa tano asubuhi, watarudi kutoka shuleni saa 10 hadi 11. Kwa mujibu wa Kishimba utaratibu wa watoto kwenda shule asubuhi ni wa nchi za Uingereza, Ulaya na nyinginezo.

Alitoa mfano kwamba nchi za Ulaya bwana na bibi wanafanyakazi, wanaondoka na watoto wao wanawaacha shule, wanaporudi wanawapitia.

"Kule Ulaya kuna tishio la barafu, inaweza kupiga London ukawa hauwezi kurudi nyumbani, kwa hiyo kumuacha mtoto nyumbani ni hatari, lakini kwa Ulaya kule nyumbani hakuna kazi zozote za kufanya, lakini sisi tunazo kazi nyingi za kufanya, kwa nini watoto wetu wasiende shuleni saa 5 hadi saa 6, wakiwa wamefanyakazi?

Leo hii tuna watoto wa shule za msingi za kutwa milioni 4 hadi tano, wakifanyakazi nyumbani kwa kuzalisha kilo moja moja ya mahindi, mtama au mpunga, tutakuwa tumeinua uchumi wetu kwa kiwango cha juu, lakini pia watakuwa wamepata elimu ya kutosha, hivyo watakapomaliza vyuo vikuu na tukawalazimisha wajitegemee hawatakuwa na tatizo lolote la kurudi kijijini."

Katika suala lake la pili, Kishimba alizungumzia watoro wa wanafunzi, akisema utafiti na uzoefu walionao, watoro ndiyo watu waliofanikiwa katika maisha.Hivyo alihoji kwa nini Wizara ya Elimu isianzishe mtaala wa watoto watoro na watu wazuri (wasiokuwa watoro).

"Kuna ubaya gani wa kuwa na mtaala wa watoro watakaofundishwa na watu waliokuwa watoro, ambao wameonesha mafanikio?"Alihoji.
Alitoa mfano akisema aliyevumbua Amerika hakuwa msomi, bali alikuwa kwenye safari zake kwenda India, alipopotea alijibuta Amerika, ndipo akawa amevumbua Amerika kwa kwamba sasa wote tunakwenda kuomba pesa Amerika?

"Leo hii tunashuhudia watu wakubwa wakifanya mambo makubwa, leo tuna wana michezo, wana muziki, bahati nzuri na humu ndani (bungeni) tuna zaidi ya wabunge 50 watoro, lakini wana mafanikio makubwa sana, kwa ridhaa yako kama utakubali nitaje hata 10," alisema.

Hata hivyo, alikatishwa na taarifa iliyotoka kwa mbunge wa Itilima (CCM), Njalu Siyanga aliyesema Kishimba naye hakumaliza shule ya msingi, lakini alifanikiwa sana kuchenjua dhahabu na mwaka 1992, alianzisha ununuzi wa pamba hapa nchini.

Akijibu taarifa hiyo, Kishimba alikiri kuwa hakumaliza shule ya msingi na kwamba aliishia darasa la nne, alielewa kitu wanachofundisha kina faida maeneo fulani.

"Mimi nimeishia darasa la nne nikagundua ndani ya elimu kuna faida fulani, kwa nini mzazi wangu na mimi tukamatwe kurudishwa shuleni? Tuendelee miaka 20 isiyokuwa na faida?" Alihoji na kuongeza kwamba utaratibu wote huo ambao wanahangaika nao ni wa Ulaya. Alisema katika suala la elimu ni lazima wizara ifanye utafiti kwa vitu vingi. 

"Leo hii kuna Watanzania zaidi ya milioni 10 wanaomiliki simu, lakini VETA haina mtaala wa kutengeneza simu, leo hii kuna biashara nyingi za madalali zimepatikana, lakini hatuna mtaala wa madalali, wapo mtaani na wanaendesha shughuli zao, lakini VETA vitu walivyog'ang'ania havipo," alisema.

Pamoja na wananchi kadhaa kuunga mkono mchango huo, pia video inayoonesha Kishimba akichangia Bungeni imeonekana kusambaa katika makundi mbalimbali ya mitandao ya kijamii yakiwemo makundi ambayo yanahusisha masuala ya familia.Walio wengi kwenye makundi hayo ya kijamii yaliyoko katika mitandao ya kijamii nao wameonekana kumpongeza na kumuunga mkono.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...