RAIS John Magufuli amesema kuwa Taasisi ya Benjamini Mkapa imeendelea kutoa mchango mkubwa hasa katika kufanya jitihada ya kuondoa umaskini na kuboresha maisha ya watanzania.

Amesema taasisi hiyo hadi mwaka juzi imefanikiwa kujenga nyumba zaidi ya 300 kwa ajili ya utumishi wa afya nchini.

Magufuli ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua kitabu cha Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa cha Maisha Yangu, Kusudio Langu kilichoandaliwa tangu mwaka 2016 na Taasisi ya Uongozi.

Rais Magufuli amesema pamoja na Rais mstaafu Mkapa kusaidia maskini pia amekuwa akishiriki katika jitihada za kutatua migogoro mbalimbali katika baadhi ya nchi za Afrika ikiwamo Kenya na Burundi.

"Pia kupitia jukwaa la uongozi Afrika, mzee Mkapa amekuwa akishirikiana na viongozi wengine wa Afrika katika kujengewa uwezo wa kiongozi na kuhimarisha utawala bora," alisema Rais Magufuli na kuongeza

"Kwa haraka haraka nimefanikiwa kukisoma kitabu hiki cha Mkapa ambapo kwenye sura ya kwanza ya pili anagusia masuala ya imani, sala na kazi. Hii inadhihirisha kwamba mzee wetu alikuwa mcha Mungu," alisema.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja amesema walipewa jukumu la kuongoza kada ya uongozi nchini, moja ya jukumu lake ni kuandaa tawasifu za viongozi.

“Kuzindua tawasifu ya Rais mstaafu Mkapa ni mwanzo wa kuelekea sehemu nyingine ya programu hii na hivi punde tutakuwa tunasherehekea maisha ya Mwinyi (Ali Hassan- Rais wa Awamu ya pili) kitabu kipo karibu kukamilika,” amesema.

Profesa Semboja amesema kuandika vitabu kuhusu maisha ya viongozi inasaidia wengi kujifunza namna bora ya kuishi, akibainisha kuwa viongozi wengi hawaandiki vitabu kutokana na kukabiliwa na mambo mengi.

“Tunapoandika historia ya kiongozi tunaandika historia ya nchi na ndio maana imeshirikisha maisha ya Watanzania wengi, hili tukio si la kifamilia ila ni la Taifa la Tanzania,” amesema.

Amesema kitabu hicho kilianza kuandikwa mwaka 2016 na kimechukua muda mrefu kutokana na mambo mengi ya kuhakikiwa, kukutana na watu ili kukikamilisha.

Amebainisha kuwa kitabu hicho kimegharimu Sh.Milioni 230 na kinapatikana katika maduka mbalimbali ya vitabu na mitandaoni.

“Miaka 81 iliyopita siku ya Jumamosi mkoani Mtwara alizaliwa mtoto wa kiume, leo anasherehekea siku yake ya kuzaliwa na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai.”

“Ameamua kutuzawadia kitabu sehemu ya maisha kwa historia ya maisha yetu, ameamua hatachukua hata senti moja ya mauzo ya kitabu hii faida itarudi taasisi ya uongozi,” amesema.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia kabla ya kuzindua rasmi kitabu cha Historia ya Maisha ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumanne Novemba 12, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika picha ya pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa baada ya uzinduzi wa Kitabu cha Historia ya Mhe. Mkapa. Wengine ni Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na Marais wastaafu Alhaj Ally Hassan Mwinyi, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Balozi wa Finland nchini Mhe. Antila Sinikka na Mama Anna Mkapa na familia ya Mhe. Mkapa katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumanne Novemba 12, 2019

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...