Na Said Mwishehe,Michuzi Globu ya jamii

WAKALA wa Usajili ,Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na Shirika la Posta nchini wamesaini hati ya makubaliano kwa ajili ya wakala huo kutumia shirika hilo kusafirisha vitendea kazi na nyaraka muhimu zilipo katika ofisi mbalimbali nchini ili kurahisisha utoaji huduma kwa Watanzania kwa wakati.

Akizungumza wakati wa utiwaji saini wa hati hiyo ya makubaliano yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu au Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA Emmy Hudson amesema kuwa wamekutana kusaini makubaliano hayo kwa ajili ya kufanya pamoja na Shirika la Posta katika kusafirisha vitendea kazi vyao na nyaraka.

"RITA ni kifupi cha Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini ambayo inajumuisha majukumu makuu matatu ambayo tunayatekeleza , kwa wale ambao mmefika RITA kwa shughuli mbalimbali tunaamini mmeona huduma zetu.Tunasajili vizazi, vifo, ndoa, talaka, tunasimamia mirathi, tunasajili bodi za wadhamini, tunasimamia mali ambazo hazina wenyewe na tunatunza wosia na kuandika.Hivyo leo tuko hapa kwa ajili ya kusaini hati ya makubaliano kwa ajili ya kufanya kazi pamoja na Shirika la Posta katika kusafirisha vitendea kazi vyetu,"amesema Hudson.

Amefafanua kwamba kama inavyofahamika kuwa RITA ni mratibu wa shughuli za usajili wa matukio muhimu ya binadamu kama alivyozoeleka hapo awali , wanahusika na kusajili  vizazi vifo, ndoa , talaka, na watoto wa kuasili na katika kutekeleza majumu yao yote muhimu yanayowahusu wanasadiana na wadau mbalimbali kuyafanikisha kwa upande wa Tanzania Bara.

"Ili kuwezesha majukumu hayo kufanyika RITA inalojukumu la kutengeneza nyaraka na vitenda kazi ili viweze kutumika katika maeneo ambayo tunafanya  nayo kazi  na hasa katika ofisi mbalimbali ambazo shughuli zao zinafanyika.Pamoja na kutengeneza na kununua hivyo vifaa lazima vifike mahali kupitia njia ya usafiri.Tumekuwa tukitumia njia mbalimbali kusafirisha vifaa hivyo katika ofisi zetu na tumekuwa tukitumia usafiri wetu.

"Hata hivyo kumekuwepo na changamoto ya kufikisha vifaa na nyaraka muhimu kwa wakati, hivyo tumeona fursa iliyopo kwa Shirika la Posta ambao wamesambaa nchi nchi nzima, tumeona tuingie nao makubaliano kwa ajili ya kusafirisha vitendea kazi na nyaraka zetu.Kwa hiyo kimsingi kama nchi ilivyokuwa kubwa nasi tumekuwa tukisafirisha tani 10 kwa mwaka.Nyaraka ambazo tunasafirisha nusu yake zinatakiwa kurudi tena Ofisi ya RITA Makao Makuu kwa ajili ya kuzitunza,"amesema na kuongeza jukumu la kutunza nyaraka hizo ni lao ili ziweze kutumika katika matumizi ya Serikali na mtu binafsi.

Amesema kuwa wanatambua kuwa wanayo mifumo imara ya Tehama ya kutunza kumbukumbu lakini bado kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na nyaraka halisi. Ametoa mfano kuwa Rais mstaafu wa Marekani Barack Obama wakati anataka kugombea aliwekewa vikwazo kuhusu mahali alipozaliwa."Tunafahamu Marekani teknolojia yao iko juu lakini Obama alilazimika kupeleka cheti halisi kuthibitisha kuwa amezaliwa katika nchi hiyo.Hivyo tunaona umuhimu wa nyaraka halisi na hivyo kwetu lazima tuhakikishe inasafiri katika mikono salama,"amesema.

Ameongeza hivyo mashirikiano hayo ambayo wameingia na Shirika la Posta wanaamini kwamba nyaraka hizo zitawafikia kwa wakati na  kubwa zaidi iliyopewa jukumu hilo i taasisi ya umma na hivyo wanaamini kutakuwa na usalama, uadilifu na nidhamu kubwa.

"Tulikutana  siku moja tukazungumza na hatimaye tukakubaliana na leo tupo hapa kwa ajili ya kuweka makubaliano ili haya ambayo tumezungumzwa yawe kwenye utekelezaji kwa vitendo.Ni matarajio yetu  huu utakwenda vizuri na tumeanza kwa makubaliano ya mwaka mmoja na huko mbele tutaangalia kama tuendelee au tusiendelee maana tunafahamu makubaliano si Msahafu au Biblia,"amesema.

Kwa upande wake Posta Master Mkuu Hassan Mwang'ombe amesema jambo ambalo linafanyika leo halijawaji kufanyika huko nyuma na kwamba ni muhimu sana kwani linahusu ushirikiano kati ya Shirika la Posta na RITA katika kusafirisha nyaraka na vitendea kazi.

Amesema kuwa makubaliano hayo yanakwenda kurahisisha utoaji huduma kati ya eneo moja ya jingine na kwamba makubaliano hayo ni sehemu ya magizo ambayo wamepewa , kwamba wananchi wa Tanzania wanapaswa kupata huduma bora na kwa haraka.

"Tunaamini mambo yatakuwa mazuri yatarahisisha utoaji huduma na kwa haraka.Sisi Posta kwa sasa tupo katika kipindi cha mabadiliko makubwa na haya tunayafanya katika eneo zima la usafirishaji.Nitoe  mfano mmoja zamani tulikuwa tunatumia mawakala kusafirisha bidhaa lakini sasa tumenunua magari yetu wenyewe, tunakwenda katika mikoa mbalimbali nchini.Tuko kila mahali ili kuhakikisha tunasafirisha bidhaa za Watanzania,'amesema.

Amesema ndani ya saa 36 wanakuwa wamefika na kufanya huduma na kuongezawanatumia muda mchache, hivyo RITA hawajakosea kuwatumia Posta katika kufanikisha huduma hiyo inatekelezwa kwa wakati."Kwa makubaliano haya tunasema RITA wamelamba dume na hatuko tayari kuona watu wanaharibu uhusiano  huu."amesema.

Amesema kuwa Watanzania wanaweza kufanya mambo makubwa na kueleza kuwa ile dhana ya mambo mazuri yanafanywa na Wazungu tu inapaswa kuondewa kwani sio kweli.Hata Watanzania wanaweza kufanya mambo makubwa kuliko hata yanayofanywa na Mzungu.
  Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu au Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA Emmy Hudson (kushoto) akiwa  na Posta Master Mkuu Hassan Mwang'onde wakisaini hati ya makubaliano leo jijini Dar es Salaam baada ya RITA kuamua kuanza kutumia Shirika hilo kusafirisha nyaraka na vitendea kazi katika maeneo mbalimbali nchini. Wanaoshuudia na maofisa wa RITA na Shirika la Posta
  Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu au Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA Emmy Hudson akiwa  na Posta Master Mkuu Hassan Mwang'onde wakiwa amesimama na kushika hati za makubaloano baada ya kutia saini leo jijini Dar es Salaam.Makubaliano hayo yanahusu RITA kuanza kutumia Shirika hilo kusafirisha nyaraka na vitendea kazi katika maeneo mbalimbali . Wanaoshuudia  kulia ni ofisa wa RITA na Shirika la Posta
 Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu au Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA Emmy Hudson akiwa  ameshikana mkono na  Posta Master Mkuu Hassan Mwang'onde baada ya kusaini hati ya makubaliano  leo jijini Dar es Salaam ambapo RITA wataanza kutumia Shirika hilo kusafirisha nyaraka na vitendea kazi katika maeneo mbalimbali nchini. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...