Ofisa madini mkazi (RMO) wa Mkoa wa kimadini wa Simanjiro, Daudi Ntalima, akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani.
……………..
WAFANYABIASHARA maarufu wa madini ya Tanzanite 28 wakiwemo wenye asili ya bara la Asia na baadhi ya wamiliki wa migodi hiyo, wameitwa katika ofisi ya madini Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara ili watoe taarifa juu ya madini waliyonayo. 

Kwa mujibu wa barua ya Ofisa madini mkazi wa Mkoa wa kimadini wa Simanjiro, Daudi Ntalima imewataka wamiliki hao wa migodi, madalali na wanunuzi wa madini hayo kufika ofisini kwake kuanzia leo jumanne ya Novemba 12.

Ntalima alisema shughuli hiyo itafanyika kwenye ofisi yake, kwa muda wa siku tatu mfululizo kuanzia Novemba 12 hadi Novemba 14.

Alisema wahusika wote wameshaandikiwa barua wakiwemo wale ambao siyo wanachama wa chama cha wafanyabiashara wa madini nchini (Tamida). 

Aliwataka wahusika wote kuhudhuria bila kukosa ili kuweka uelewa wa pamoja juu ya biashara ya madini ya Tanzanite ili kujenga Taifa bora. 

Wafanyabiashara hao walioandikiwa barua ya kutii wito huo ni Hussein Lemali, Emmanuel Wado (Sunda), Saitoti, Tarimo, Bima, Hamad Mjaluo, Manesh Kotog, Edward Mollel na George Kivuyo. 

Wengine ni Ben Nkya, Peter Periera, Sam Mollel, Rakesh, Vinal, Reno, Bima, Rajan, Saran, Salesh, Sidor, Faisal, Jitu, Muller, Shah, Sumil na Frizble. 

Oktoba 29 mwaka huu Ntalima alitaja majina ya vigogo wenye kumiliki madini ya Tanzanite ofisini kwao au majumbani mwao, kufika ofisini kwake ili watoe taarifa zao juu ya madini hayo. 

Mmoja kati ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, Hawa Athuman alisema baadhi ya watu hawakuamini kama serikali ingeweza kuwaita wafanyabiashara hao na wakatii amri. 

“Tusomeshe watoto jamani, huyu RMO Daudi Ntalima ni kijana mdogo lakini anatimiza wajibu wake ipasavyo yaani hawa wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite wametoka Arusha na kuja Mirerani kuleta taarifa zao,” alisema. 

Mkazi mwingine, Hamis Hamza alisema tukio hilo ni zuri kwa serikali kwani inapokuwa na mashaka juu ya suala lolote lile hufanya mahojiano ili kujiridhisha. 

“Hii serikali ya Rais John Magufuli inafanya kazi kweli kweli jana tumewaona vigogo wametoka Arusha na kuja Mirerani kuhojiwa na kutoa taarifa zao,” alisema Hamza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...