Serikali ya Mkoa wa Kusini Unguja imedhamiria kuwapatia wafanyakazi wa Mkoa huo vifaa vya kufanyia kazi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa urahisi na ufanisi zaidi.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud ameeleza hayo wakati alipokuwa akiwakabidhi vyombo vya usafiri wafanyakazi  na viongozi wa wilaya ya Kati huko Halmashauri ya Wilaya Dunga.

Alisema lengo la kutolewa vifaa hivyo kwa wafanyakazi, ni kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi wa Wilaya ya Kati bila ya kupata vikwazo vya aina yoyte.

Amewataka wafanyakazi waliokabidhiwa vyombo hivyo kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa kwenda kwa wananchi kuwasikiliza na kuwasaidia katika kutatua changamoto zinazowakabili katika harakati zao za maisha.

Mkuu wa Mkoa amewasisitiza wafanyakazi hao kuhakikisha wanavitunza vyombo hivyo ili viweze kudumu kwa muda mrefu hasa ukizingatia vimenunuliwa kwa gharama kubwa.

Aidhaa Ayoub ametoa tahadhari  kwa wafanyakazi wanaokusanya kodi waepukane na ubadhirifu na atakaebainika kufanya vitendo vinavyoenda kinyume na kazi hiyo atachukuliwa hatua za sheria bila kumuonea aibu.

“Natoa onyo kwa yeyote atakaeshiriki katika uvujishaji mapato atashughulikiwa wala hatoonewa haya , kwani katika jambo hilo sina mzaha wala sitomuoneya mtu muhali”, alisema Mkuu wa Mkoa wa Kusini.

Aliwataka wafanyakazi wa vituo vya afya vilivyomo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kati kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa  wanapofika vituoni kutaka huduma kwani lugha mbaya inaongeza machungu kwa mgonjwa.

“Nawaasa madaktari wenye tabia ya kuwatolea wagonjwa lugha zisizofaa wanapofika kwenye vituo wajirekebishe mara moja  wapeni moyo wagonjwa ili wapate faraja na muwape matibabu mazuri”, alisisitiza Ayoub.

Mkuu wa Wilaya ya Kati Hamida Mussa Khamis amesema lengo la kutolewa vyombo vya usafria kwa Wafanyakazi ni kuwawekea mazingira mazuri ya kutekeleza majukumu waliopewa ya kuwahudumia wananchi kwa wakati na ufanisi.

 Amewataka wafanyakazi hao kuthamini juhudi zinazochukuliwa na Serikali kwa  watendaji wa kada mbali mbali ili kuona wanaongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kati Said Mtaji Askari alisema kupatiwa vyombo vya usafiri wafanyakazi ni kutekeleza azma ya Serikali ya kuimarisha sekta ya Afya, Kilimo  na Elimu baada ya kufanyika ugatuzi ambapo hivi sasa baadhi ya shughuli zimehamishiwa katika Halmashauri za Wilaya .

Zaidi ya shilingi Millioni 100 zimetumika kununulia vyombo vya usafiri ikiwemo pikipiki tatu, vespa tano, pasola nane na gari moja la kubebea wagonjwa.
  Mkuu wa  Wilaya ya Kati Unguja Hamida Mussa Khamis akizungumza na Wafanya kazi wa Wilaya hiyo katika hafla ya kukabidhi Vyombo vya Usafiri katika hafla iliyofanyika Ofisi ya Halmashauri Dunga .
 Baadhi ya Watendaji wa Mkoa wa kusini Unguja wakimsikiliza Mkuu wa  Wilaya ya Kati Hamida Mussa Khamis wakati wa kuwakabidhi Vyombo vya moto katika Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya Dunga .
 Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Muhamed Mahmoud akijaribu  moja ya Chombo cha usafiri vilivyotolewa kwa Wafanyakazi wa Wilaya ya Kati huko Ofisi ya Halmashauri Dunga.
 Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Muhamed Mahmoud akimkabidhi Pikipiki Mkuu wa Kitengo cha Misitu Haji Mohammed huko Halmashauri ya Wilaya ya kati Dunga.
 Gari ya Wagojwa (Ambulance) iliyokabidhiwa kwa ajili ya kuhudumia Vituo vya afya vya Halmashauri ya Wilaya ya Kati katika hafla ya kukabidhi vyombo vya usafiri huko Dunga.
 Vyombo vya moto vya maringi mawili aina ya Pasola, Pikipiki na Vespa vilivyokabidhiwa kwa Wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya kati Dunga na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Muhamed Mahmoud .

Picha na Maryam Kidiko  /  Maelezo Zanzibar .

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...