Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kuhusiana na Mradi wa Nyumba za Shirika la Nyumba za Taifa (NHC) uliopo eneo la Ilembo Manispaa ya Mpanda mkoa wa Katavi kutoka kwa Meneja Mawasiliano wa Shirika hilo Muungano Saguya jana wakati akikagua utekelezaji wa miradi ya NHC mkoani Katavi. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa wilaya ya Mpanda Lilian Matinga na kushoto ni Kaimu Meneja wa NHC mkoa wa Katavi na Rukwa Msumbuko Majaliwa.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioneshwa eneo inapojengwa ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika halmashauri ya wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi na Meneja wa TFS Mlele Godfrey Mlele (Kulia) wakati wa ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika mkoa wa Katavi jana.  Wa pili kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Mlele Recho Kasanda na wa pili kulia ni Meneja Mawasiliano wa NHC Muungano Saguya
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na Mkuu wa wilaya ya Mpanda Lilian Matinga wakiangalia jengo la Biashara la Paradise lilipo  halmashauri ya Manispaa ya Mpanda jana wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)  katika mkoa wa Katavi.
(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).
*********************************

Na Munir Shemweta, WANMM KATAVI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoa wa Katavi kwa kuwa moja ya mkoa wenye miradi mingi ya Shirika hilo.

Dkt Mabula alitoa pongezi hizo jana wakati akikagua miradi ya NHC kwenye mkoa wa Katavi akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi pamoja na ujenzi wa miradi inayotekelezwa na  Shirika la Nyumba la Taifa.

Miradi aliyoikagua Naibu Waziri Mabula katika mkoa wa Katavi ni ujenzi wa nyumba za watumishi katika Halmashauri ya wilaya ya Mlele, Ofisi na Nyumba ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) pamoja na ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Mpanda. Pia alikagua mradi wa nyumba sabini za Ilembo ambapo Nyumba kumi kati ya hizo ziliuzwa na nyumba sitini zimepangishwa.

Alisema, mkoa wa Katavi unaweza kuwa mkoa wa kwanza ama wa pili kwa kuwa na miradi mingi ya Shirika la Nyumba la Taifa na hali hiyo siyo tu inaonesha jinsi Shirika lilivyo makini kwenye uwekezaji miradi mbalimbali kama vile ujenzi wa nyumba za kuuza, kupangisha na majengo ya biashara bali inalifanya kuimarika kimkoa.

Akigeukia mradi wa Jengo la Biashara la Paradise lililopo Manispaa ya Mpanda, Dkt Mabula alilisifu jengo hilo kwa kuwa na mazingira mazuri ya kibiashara na kushauri taasisi za serikali katika mkoa wa Katavi kutumia fursa ya kupanga na kuwekeza kwenye jengo hilo kwa kuwa gharama zake ni nafuu ukilinganisha wapangishaji wengine.

Aidha, amelitaka Shirika la NHC mkoa wa Katavi kuhakikisha inalifanyia matangazo jengo hilo la biashara la Paradise kwa lengo la kuvutia wateja kupanga hasa ikizingatiwa kutolitangaza kunaweza kusababisha kukosa wateja.

Kauli hiyo ya kutaka kufanyika matangazo kwenye jengo hilo inafuatia Naibu Waziri Mabula kuelezwa na Kaimu Meneja wa Shirika la NHC  mkoa wa Katavi na Rukwa Masumbuko Majaliwa kuwa mpaka sasa jengo hilo la kibiashara limepangisha asilimia thelathini tu ya wateja.

‘’Mrudi kwenye kutangaza miradi yenu kupitia kipindi cha Maisha ni Nyumba na ikiwezekana kazi hiyo ifanyike mkoa kwa mkoa na mhakikishe miradi yenu mnaifanya kwa kasi, viwango na wakati ili kujenga trust kwa wateja’’ Alisema Dkt Mabula.

Kwa upande wake Meneja Mawasiliano wa NHC Muungano Saguya alisema, kwa sasa Shirika lake linafanya vizuri katika masuala ya ujenzi jambo lililosababisha kuaminwa na serikali ambapo katika mji wa serikali eneo la Mtumba Dodoma liliweza kujenga majengo ya Wizara nne na sasa Shirika linaendelea na utekelezaji wa miradi mingine kama vile ujenzi wa nyumba na ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) nchi nzima.

Awali Kaimu Meneja wa Shirika la Nyumba mkoa wa Katavi na Rukwa Masumbuko Majaliwa alimueleza Naibu Waziri kuwa kwa sasa NHC mkoa wa Katavi inatekeleza miradi mbalimbali katika mikoa ya Katavi na Rukwa.
Alisema katika mkoa wa Katavi Shirika la Nyumba linatekeleza miradi ya nyumba za watumishi Mlele, ukumbi wa manispaa ya Mpanda pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu Kibaoni wakati upande wa mkoa wa Rukwa miradi inayotekelezwa ni ile ya mradi wa nyumba za makazi jangwani Sumbawanga pamoja na duka la dawa katika hopspitali ya rufaa mkoa wa Rukwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...