Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza na wananchi kuhusu kuacha tabia ya kuingiza mifugo Hifadhini badala yake waheshimu sheria za Uhifadhi ambapo alitumia nafasi hiyo kuiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ( TAWA) iachie mifugo zikiwemo ng’ombe 179 zilizokuwa zimekatwa ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro mkoani Manyara

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Wazee maarufu wa Kijiji cha Kimotorok mara baada ya kufanya mkutano katika kijiji hicho kwa kuiagiza TAWA iachie mifugo zikiwemo ng’ombe 179 kwa makubaliano ya kutoingiza tena mifugo hiyo katika Pori la Akiba la Mkungunero.
Mbunge wa Simanjiro akizungumza na Wananchi kuhusiana na tabia iliyozuka ya kuwavamia na kuwadhuru Wahifadhi wakati wanapotekeleza majukumu yao na kuwa yeyote atayethubutu kutenda vitendo hivyo yeye hatakuwa upande wake wakati akizungumza nao katika mkutano uliofanyika katika kijiji cha Kimotorok wilayanii Simanjiro katika mkoa wa Manyara.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kimotorok wakimsiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kimotorok ambapo aliwataka wananchi hao wasiingize mifugo Hifadhini na atakayeingiza mifugo ndani ya Hifadhi atafrisiwa mifugo yote

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe, Constantine kanyasu akiwa na Wazee maarufu wa Kijiji hicho mara baada ya kumaliza kwa mkutano ambapo aliruhusu mifugo iliyokuwa imekamatwa katika Pori la Akiba la Mkungunero iachiwe.
Naibu Waziri wa Maliasili na utalii mhe. Constantine Kanyasu akiteta jambao na Naibu Kkamishna Uhifadhi wa TAWA,Mabula Misungwi ( kushoto) wakati wa mkutano wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Katika ni Mkurugenzi Mtendaji wa wialya ya Simanjiro, Yefred Myenzi.
(Picha zote na Wizara ya Maliasili na Utalii)
***************************

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ( TAWA) kuiachia na kuirudisha mifugo zikiwemo jumla ya ng’ombe 179 zilizokuwa zimekamatwa ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero ambayo ni Mali ya Mathayo Marao, Mwananchi wa Kijiji cha Kimotorok kilichopo ndani ya Pori hilo katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa makubaliano ya kutoingiza tena mifugo hiyo. 

Uamuzi huo umekuja kufuatia utata uliopo eneo ilipokamatiwa mifugo hiyo kwa vile Kijiji hicho cha Kimotorok ni miongoni mwa Vijiji na Vitongoji 366 vilivyo ndani Hifadhi na vinavyosubilia maamuzi ya Rais wa Tanzania, Mhe.John PombeMagufuli na moja kati ya maagizo aliyoyatoa kwamba wananchi wa Vijiji hivyo wasibugudhiwe hadi pale maamuzi ya mwisho yatakapotolewa. 

Kwa mujibu wa Wahifadhi, Mifugo hiyo iliyokamatwa mwishoni mwa mwaka jana inadaiwa kukutwa mita 450 ndani ya Pori hilo huku Wananchi wakidai kuwa Mifugo hiyo ilikutwa nje ya mita 450 kutoka kwenye mpaka mahali ambako wamekuwa wakiishi huku wakisubiri kauli ya mwisho ya Mhe.Rais.

Mvutano huo baina ya Wahifadhi na Wananchi umempekelea Mhe.Kanyasu kutumia busara na kufikia uamuzi huo kwa kuzingatia kuwa Kijiji hicho kipo ndani ya Hifadhi. 

Kutokana na majadiliano ya pande hizo mbili, Naibu Waziri huyo amelazimika kutoa uamuzi huo wa kuachia mifugo hiyo kwa makubaliano ya Wananchi wa Kijiji hicho kuheshimu sheria za Uhifadhi kwa kutoingiza mifugo ndani ya Hifadhi hadi pale maamuzi ya mwisho yatakapotolewa na Rais Magufuli.

Akizungumza jana katika mkutano huo uliofanyika kwenye Kijiji cha Kimotorok, Naibu Waziri Mhe.Kanyasu amesema uamuzi huo umefanyika kwa busara kwa vile mifugo hiyo ilibidi ipelekwe mahakamani.
Amesema kitendo cha kuacha kupeleka kesi hiyo mahakamani kinasaidia kupunguza idadi kubwa ya mifugo kufa ambapo hadi sasa zaidi ya ndama kumi wameshakufa.

Kufuatia hali hiyo, Mhe.Kanyasu amewataka wananchi hao kuacha kutumia vibaya kauli ya Rais Magufuli kwa kuanza kuvamia maeneo mapya ya Hifadhi kwa kisingizio cha kauli hiyo ilhali wanatakiwa kubaki na mifugo yao mahali walipo. 

Amefafanua kuwa kulikuwa na uwezekano wa kupeleka mifugo hiyo mahakamani ila kutokana na Wananchi hao kuomba maridhiano kwa kutambua kuwa wametenda kosa imepelekea mifugo hiyo kuachia.
Katika hatua nyingine, Mhe Kanyasu amesema Serikali haipendi kutaifisha mifugo inayokamatwa Hifadhini kama sheria inavyoelekeza kwa vile wananchi wengi wamejikuta kwenye umaskini wa hali ya juu, Hivyo amewataka wananchi hao kuacha tabia ya kuingiza mifugo hifadhini kwa vile watafrisiwa. 

” Serikali inafurahi kuona Wafugaji wananeemeka kupitia mifugo yao huku uhifadhi ukiendelea kwa maslahi mapana ya Taifa” alisisitiza Kanyasu
Aidha, Mhe.Kanyasu ametoa onyo kwa Wananchi wanaovamia Wahifadhi wakiwa wanatekeleza majukumu yao na kuahidi kuwa Serikali haitamvumilia Mwananchi yeyote atakayethubutu kutumia mabavu dhidi ya Wahifadhi. 

” Tukikubaini ni miongoni mwa Mwanakijiji uliyejitokeza ukiwa umeshika mkuki au unapiga mwano kwa nia ya kuwahamasisha wenzako kwa ajili ya kuwadhuru Wahifadhi, Tutakushughulikia ipasavyo” Alisisitiza
Kwa upande wake Mbunge wa Simanjiro, Mhe. James Millya amewataka wananchi waache tabia ya kuingiza mifugo ndani ya Hifadhi. 

Pia amelaani vikali vitendo vya baadhi ya wananchi wanaohamasisha ghasia kwa Wahifadhi na kuahidi kuwa yeye hatakuwa tayari kumsaidia mwananchi yeyote atakayekamatwa kwa kutenda kosa hilo kwa vile Wahifadhi hao wanafanya kazi za kulinda Hifadhi hizo kwa niaba ya Watanzania wote. 

Kufuatia hali hiyo, Mhe.Millya amewataka Wazee wa mila ‘Olaibon’ kutumia nafasi hiyo kwa kuitaka jamii yao kufuata sheria za Uhifadhi kwa kuheshimu Sheria zilizopo zinazokataza kulisha mifugo ndani ya Hifadhi
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mhe.Millya amewataka Wananchi hao kila mmoja awe Mlinzi wa mwenzake kwa kuimarisha ujirani mwema kati ya Wananchi na Wahifadhi badala ya kuendekeza uhasama kwa kuingiza mifugo ndani ya Hifadhi. 

Awali, Joseph Olematwaa ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho alisema uamuzi wa kuachia mifugo utarudisha mahusiano mema kati ya Wahifadhi wa Pori hilo na Wananchi na kuahidi kuwa hawataingiza tena mifugo ndani ya Hifadhi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...