Rais Shirikisho la mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) ,Phares Magesa




1. USHIRIKI WA TIMU YA TAIFA KATIKA MICHUANO YA KUFUZU MATAIFA YA AFRIKA 2021

Timu ya Taifa Kikapu ya Tanzania ya Wanaume ambayo ilishiriki katika mashindano ya awali ya kufuzu katika kombe la Mataifa ya Afrika la Kikapu 2021, imerejea nyumbani salama na tunashukuru Mungu kwa uwakilishi mzuri katika mashindano haya. Kwa niaba ya Shirikisho tunatoa pongezi nyingi kwa vijana hawa kwa uzalendo wao uliotukuka, itakumbukwa kuwa timu ya Taifa ya Tanzania kwa miaka mingi ilikuwa haishiriki mashindano ya Kimataifa. 
 
Tangu uongozi mpya uingie madarakani miaka miwili iliyopita tumechuka hatua kadhaa kuhakikisha kuwa timu ya Taifa ya Tanzania inaundwa na inashiriki mashindano ya Kimataifa, mwaka 2018 timu za Taifa za vijana (wasichana na wavulana) chini ya miaka 18 zilishiriki mashindano ya kanda ya tano ya Afrika, mwaka jana 2019 timu ya wasichana ya chini ya maika 16 ilishiriki mashindano ya kanda ya tano ya Afrika na ikafuzu kucheza Kombe la Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu na ilishirki (Afrobasket 2019 U16 iliyofayika Kigali , Rwanda).
 
 Timu ya Taifa ya wakubwa ya Wanaume pia ilishiriki mashindano ya Kanda ya tanoya Afrika, Kampala, Uganda 2019 na mwaka huu pia kama ilivyoonyeshwa hapo juu tumeshiriki mashindano haya ya awali ya (Afrobasket 2021 Pre Qualifiers) yaliyofayika 14-18 Januari 2020, Nairobi, Kenya. Tunashukuru sana Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na wadau wengine waliotusaidia kufanikisha ushiriki wetu katika mashindano haya.

2. PONGEZI KWA SAMATTA

Tunatoa pongezi nyingi kwa Mbwana Samatta kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kuchezsa ligi kuu ya England (EPL), kama ambavyo Hasheem Thabeet alikuwa Mtanzania wa kwanza wa kikapu kucheza ligi kuu ya Kikapu ya USA ya NBA, ni mfano mzuri kwa wanamichezo wote.

3. KALENDA YA MWAKA 2020
Shirikisho liko katika maandalizi ya utekelezaji wa kalenda ya mwaka, ambapo ligi za mikoa zitaanza mwezi Februari , kufuatiwa ni ligi za kanda, na baadae ligi ya Taifa na kuhitimisha na kombe la Taifa mwishoni mwa mwaka, tutakuwa na mashindano kadhaa ya kimataifa ya timu za Taifa na vilabu ya kikanda na Afrika na mikutano ya Shirikisho, 1 Feb kamati ya utendaji itakutana ili kupitisha kalenda hiyo.

Tutakuwa na mashindano ya kanda ya tano ya Afrika kati ya mwezi wa nne na sita 2020 ambayo pia yatakuwa ni ya kufuzu kwa mashindano ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 18 ambapo tunatarajia timu zetu zote mbili za Taifa za Tanzania wasichana na wavulana zitashiriki.

4. USHIRIKI WA MASHINDANO NA MAFUNZO MBALIMBALI

Ili kuboresha uwezo wetu wa kushindana kimataifa, hatua ya kwanza tuliyoamua ni kushiriki mashindano ya kimataifa kadri itakavyowezekana kwa timu za vijana na watu wazima na hilo limefanyika kwa mafanikio licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza kutoka na uhaba wa rasilimali fedha na wafadhili. 
 
Hatua inayofauata ni kuboresha kiwango cha kiufundi cha mchezo ili tuweze kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa, na hili linafanyika kwa muendelezo ikiwa ni pamoja na kuendesha mafunzo kwa Walimu wetu wa kikapu nchi nzima , ambapo mwaka jana kwa msaada wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) tumeendesha mafunzo ya Ukocha kwa walimu 30 mafunzo ya ‘FIBA Level 1 Technical course for coaches’, na mapema mwaka huu kwa msaada wa Shirikisho la mpira wa kikapu duniani (FIBA) tutaendesha mafunzo kwa Walimu 15 na waamuzi 15 ya ‘FIBA level 1 technical courses for Coaches and Referees’ . 
 
TBF itaendelea kuweka mkazo mkubwa kwa program za vijana na watoto tayari tumewasiliana na Serikali na kuomba mchezo wa kikapu uingie katika michezo ya shule za msingi ili vijana waanze kucheza mchezo wa kikapu mapema zaidi na kwa ubora, hatua nyingine ni kusimamia vizuri mpango wa kupeleka vijana wetu ili wakasome na kucheza nje ya nchi , hadi sasa tuna vijana 6 Marekani wanaosoma na kucheza kikapu, tunakusudia kuwasaidia wengi zaidi ili waende mwaka huu na miaka ijayo, vijana hawa na wengine ndio watakuwa chachu ya kuwa na timu bora za Taifa miaka ijayo.
 
 Pia TBF inaendelea kuhamasisha wadau na taasisi mbali mbali kushiriki katika kusaidia kutatua changamotio ya viwanja , muitikio ni mzuri na kuna viwanja kadhaa viko katika mipango ya kujengwa na vingine vinajengwa maeneo mbali mbali ya nchi yetu ambayo awali yalikuwa hayana viwanja sasa yana viwanja vya umma na vingine vya taasisi binafsi kama Don Bosco, Oysterbay na kutoa fursa kwa vijana zaidi kucheza kikapu, Mikoa ya Simiyu, Mwanza imepiga hatua katika hili, mikoa ya Arusha, Dodoma iko katika hatua nzuri za ujenzi wa viwanja vya michezo ikiwemo kikapu na mikoa mingine nayo iko katika hatua mbalimbali za ujenzi wa viwanja, ni matumaini yetu kuwa idadi ya mikoa iliyo na miradi ya ujenzi wa viwanja itaongezeka mwaka huu.
Tuna imani kubwa ahadi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ya ujenzi wa viwanja vya Kikapu nayo itatekelezwa.

Kwa sehemu kubwa tunashukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukubali ombi la wadau wa michezo nchini la kujenga uwanja mkubwa wa ndani (Sports Arena) ambao utatumika kwa mchezo wa kikapu , mikutano, matamasha, maonyesho na michezo mingine ya ndani, ni matumaini yetu kuwa uwanja huu utakaojengwa utakuwa ni chachu kubwa katika kuchochea ukuaji wa michezo na kuvutia wawekezaji zaidi katika kikapu na michezo mingine ya ndani.

5. MASHINDANO MBALIMBALI YA NDANI KWA VIJANA

Hatua nyingine tunazochokua ni kuhakikisha kila mkoa unacheza ligi yake ya mkoa (RBA), kusimamia ligi hizo ziendeshwe vizuri, kuanzia ngazi ya mkoa (RBA) hadi Taifa (NBL) na mashindano ya Kitaifa kama Taifa Cup, Muungano Cup na mengineyo ili yawe na ufadhili wa uhakika kuwezesha timu nyingi kushiriki vizuri kwa ubora zaidi. 
 
Pia kwa kushirikiana na wadau kuimarisha ligi ya Junior NBA ili iweze kuwanufaisha vijana wengi zaidi nchini, Pia Shirikisho linatoa wito kwa mikoa yote nchini kuhakikisha inatoa kipaumbele kwa wanawake na watu wenye ulemavu nao kucheza kikapu. Mchezo wa kikapu aina ya 3x3 pia utaendelea kuimarishwa na mikoa yote nayo ianze kucheza aina hii ya mchezo wa kikapu katika ligi zao.

Shirikisho linaomba mikoa na vilabu vyote nchini kufanya maandalizi mazuri ya ligi za mikoa kwa kuwa ndio msingi wa kuwa na wachezaji wazuri ambao watatumika katika timu za Taifa na vilabu vione umuhimu wa kujiandaa vizuri ili viweze kupata nafasi ya kushiriki ligi ya Kikapu ya Afrika (BAL) mwaka 2021, ligi hii ya BAL ina manufaa makubwa ya kifedha kwa wachezaji, vilabu na nchi.

6. USHIRIKIANO NA WADAU MBALIMBALI
Shirikisho litaendelea kuimarisha ushirikino na vyama rafiki ili kuendeleza mchezo wa kikapu nchini kama vile NBA ya Marekani, CBA ya China, vyama vya kanda ya tano ya Afrika na vingine ambavyo vimeonyesha nia ya kushirikana nasi.

Shirikisho pia litaendelea kushirikiana na wadau wengine ambao wanafanya matukio ya kikapu kama kampuni ya EATV na Coca-Cola kupitia shindano la Sprite BBall Kings ili kuongeza mchango wao katika kuendeleza mchezo wa kikapu nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ushirikiano huu unakuwa na tija kwa wahusika wote, TBF itakutana na wadau hawa kuboresha ushirikano kwa manufaa ya pande zote.

7. MCHAKATO WA MABORESHO YA KATIBA NA MIFUMO
Pia Shirikisho linakusudia kuboresha (kuandika upya) katiba yake ili iende na wakati, kuboresha namna ya utendaji wa Shirikikisho kwa kuwa na miundombinu na mifumo bora ya ufanyaji kazi na kuongeza watedaji kazi ili kuboresha ufanisi wa utekezaji wa majukumu ya Shirikisho, hatua hizi zote zitapitia katika vikao husika vya Shirikisho.

Wafadhili na wadau mnaombwa kujitokeza kufadhili matukio haya ya kitaifa na kimataifa ili kusaidia juhudi za kuendeleza mchezo wa kikapu Tanzania, kuitangaza nchi yetu na kutumia mchezo wa kikapu kutatua baadhi ya changamoto zilizopo katika jamii yetu na kusaidia jitihada za kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

PHARES MAGESA
RAIS -TBF
23 Jan, 2020

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...