Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amefika kijiji cha msamalia wanapoishi watu walioathirika na ugonjwa wa Ukoma kilichopo Hombolo mkoani Dodoma
=======  =======  =======  ========

HOMBOLO, DODOMA

Ndugu wananchi na wanahabari, 
Siku ya Ukoma Duniani huadhimishwa ulimwenguni kote kila Jumapili ya mwisho ya mwezi Januari. Kwa mwaka huu, siku hii itaadhimishwa tarehe 26 Januari, 2020. Kama ilivyokuwa mwaka uliopita kule kwenye makazi ya wasiojiweza ya Nunge – Kigamboni, mwaka huu, tumeona ni vyema kutoa tamko hili hapa Hombolo. Hiki ni kituo cha kutunza wazee na miaka ya nyuma kilikuwa kituo cha wagonjwa wa Ukoma. Lengo kuu la maadhimisho haya ni kuwakumbusha na kuwahamasisha wananchi wa Tanzania kuhusu ugonjwa huu ili waongeze kasi katika kuchukua hatua stahiki na kuutokomeza kabisa. Historia ya ugonjwa huu inaonyesha ya kuwa Ukoma huambatana na unyanyapaa mkubwa ikiwa ni pamoja na kuwatenga wale ambao wanaugua hususani walioathirika viungo. Ugonjwa huu husababisha ulemavu wa kudumu na kufanya waathirika kuwa tegemezi na kutothaminiwa.

Ndugu wananchi na wanahabari
Siku hii ni muhimu kwa jamii kukaa chini na kutafakari madhara na shida zinazotokana na maradhi ya Ukoma. Ugonjwa wa Ukoma huleta madhara makubwa kwa mwili wa binadamu ikiwa ni pamoja na upofu, vidonda sugu miguuni na mikononi, kukatika vidole vya mikono na miguu, pua, masikio na kusababisha ulemavu wa kudumu.

Ndugu wananchi na wanahabari, 
Tanzania tayari ilifikia viwango vya kidunia vya utokomezaji wa Ukoma vya kuwa na chini ya wagonjwa 10 kati ya 100,000 mnamo mwaka 2006. Kutokana na juhudi za serikali, viwango hivyo vya utokomezaji vimeendelea kuboreshwa na kushusha idadi ya waathirika wa Ukoma kutoka 4.3/100,000 mnamo mwaka 2014 na kufikia wagonjwa 3/100,000 mwaka 2019.
Aidha, jitihada kubwa za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli zimeweza kupunguza viwango vya maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukoma kutoka wagonjwa 43 kati ya watu milioni moja mwaka 2014 hadi kufikia wagonjwa 26 kwa watu milioni moja mwaka 2019. Vile vile, tumepunguza idadi ya watoto wanaougua Ukoma kwa asilimia 41, kutoka watoto 90 mwaka 2014, hadi 53 mwaka 2019.  Hadi kufikia mwaka 2019, mikoa yote isipokuwa Lindi ilikuwa tayari imefikia kiwango cha utokomezaji. Hata hivyo bado tunazo  Halmashauri 16 tu ambazo bado hazijafikia viwango hivyo.  Halmashauri hizo ni pamoja na Manispaa ya Lindi, Liwale, Nachingwea, Ruangwa, Masasi, Nanyumbu, Morogoro, Mvomero, Mpanda, Nkasi, Manispaa ya Shinyanga, Manispaa ya Kigoma, Kibaha, Mkinga na Tunduru.


Ndugu wananchi na wanahabari
Napenda kuchukua fursa hii, kuzikumbusha Halmashauri hizi na mikoa kuongeza kasi ya kutokomeza Ukoma na kuhakikisha kaya zote hatarishi na zenye wagonjwa wa Ukoma zinafikiwa, wanakaya wanachunguzwa dhidi ya ugonjwa wa Ukoma na wale ambao tayari wanaugua wanatibiwa kikamilifu. Mikoa na Halmashauri zihakikishe zinatenga bajeti katika mipango yao ili kuendesha kampeni za uhamasishaji, uelimishaji, na uibuaji wa wagonjwa wapya.

Ndugu wananchi na wanahabari
Siku ya Ukoma Duniani inatupa fursa ya kutathmini mwelekeo wa jitihada zetu nchini na zile za kimataifa katika kupambana na ugonjwa huu. Kauli mbiu katika maadhimisho ya mwaka huu ni “TUTHAMINI HAKI NA UTU WA WAATHIRIKA WA UKOMA KWA KUTOKOMEZA UBAGUZI, UNYANYAPAA NA CHUKI”. Ni kweli kuwa waathirika wengi wa Ukoma wananyanyapaliwa na kubaguliwa katika maeneo mengi. Takriban asilimia 50 ya wagonjwa wa Ukoma hupatwa na sonona na huishi maisha ya huzuni na wasi wasi mkubwa. Haya yote husababishwa na mtazamo potofu wa jamii dhidi ya waathirika wa ugonjwa wa Ukoma. Mtazamo huu hasi ndio kikwazo kikubwa katika vita ya kutokomeza Ukoma duniani na hapa nchini.


Ndugu wananchi na wanahabari
Unyanyapaa na chuki dhidi ya waathirika wa Ukoma, huwafanya wajifiche na kushindwa kujitokeza katika vituo vya huduma kwa ajili ya matibabu na hivyo kupelekea kupata ulemavu wa kudumu. Baya zaidi ni kuwa, kuchelewa kwa wagonjwa hawa kupata matibabu ndio chanzo cha mwendelezo wa mnyororo wa maambukizi mapya katika jamii yetu.
Serikali, wadau na wananchi wote wanahimizwa kuungana na kuongeza nguvu katika kupinga matukio yote ya ubaguzi na unyanyapaa. Kwa kufanya kazi pamoja na kupinga kwa nguvu zote vitendo hivi, itatusaidia kupiga hatua kubwa mbele kuelekea kutokomeza Ukoma.

Ndugu wananchi na wanahabari
Ukoma husababishwa na vimelea aina ya bakteria na ni ugonjwa wa kuambukiza ambao huenezwa kwa njia ya hewa toka kwa mtu anayeugua na ambaye hajaanza matibabu. Dalili za Ukoma ni pamoja na baka au mabaka yenye rangi ya shaba mwilini.  Mabaka haya hayaumi wala hayawashi, bali hupoteza hisia ya kugusa na yanaweza kujitokeza mahala popote mwilini, kuanzia kichwani hadi miguuni.       
“Napenda kutoa wito kwa kila mtu na familia kujijengea tabia ya kujichunguza ngozi mwili mzima kila wakati na pale utakapoona dalili kama hizo au mabadiliko yoyote, nenda kituo cha kutolea huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi, ushauri na tiba”.
Dawa za Ukoma zinatolewa bila malipo yoyote katika vituo vya kutolea huduma za afya vya serikali na binafsi. Serikali itaendelea kuhakikisha zipo dawa za kutosha na zinapatikana wakati wote na kwa kila mgonjwa wa Ukoma mahali popote nchini. Tunaendelea na juhudi za kutoa elimu kwa umma na kwa watoa huduma hususan katika maeneo ambayo bado Ukoma ni tatizo kubwa.

Ndugu wananchi na wanahabari, 
Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI inatekeleza shughuli mbali mbali katika kuhakikisha Ukoma unatokomezwa  kabisa. Shughuli hizo ni pamoja na:
·       Kuhakikisha dawa za kutibu Ukoma zinaendelea kupatikana wakati wote na bila malipo yoyote
·       Kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu dalili za Ukoma na upatikanaji wa huduma kwa kutumia vifaa vya habari, elimu na mawasiliano kama vile vipeperushi, mabango na mikanda ya video,
·       Uwezeshaji na utekelezaji wa shughuli za kuzuia ulemavu unaotokana na Ukoma, ikiwemo kufanya upasuaji maalum, huduma za kitaalam za macho na utoaji wa viungo bandia pamoja na viatu maalum
·       Kununua na kusambaza viatu maalum kwenye maeneo yenye waathirika wa Ukoma ambapo kwa mwaka 2018, jumla ya jozi 1,800 za viatu hivyo zilisambazwa katika mikoa yote yenye uhitaji.


Ndugu wananchi na wanahabari,
Pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kutokomeza Ukoma, bado zipo changamoto kubwa mbili ambazo ni jamii kuendelea kushikilia imani potofu juu ya Ukoma kuwa ni ugonjwa wa kurithi au kulogwa; na wagonjwa kuchelewa kujitokeza kupata matibabu hadi wanapopata ulemavu.
Ndugu wananchi na wanahabari,
Aidha, napenda kuwashukuru watoa huduma katika vituo vya huduma za afya kote nchini kwa juhudi wanazofanya kila siku kuhakikisha ugonjwa huu si tatizo la kiafya tena nchini. Pia wanahabari kwa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu magonjwa mbalimbali. Pia nachukua nafasi hii kwa niaba ya serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kuyashukuru mashirika mbali mbali ya ndani na nje, yanayounga mkono juhudi zetu za kutokomeza Ukoma nchini kama vile Norvatis Foundation ya Uswisi, Germany Leprosy and Tuberculosis Relief Association (GLRA) ya Ujerumani, Nippon Foundation chini ya Sasakawa Memorial Health Initiative ya Japani na Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa michango yao ya hali na mali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma hapa nchini Tanzania. 

“TUTHAMINI HAKI NA UTU WA WAATHIRIKA WA UKOMA KWA KUTOKOMEZA UBAGUZI, UNYANYAPAA NA CHUKI”.

Asanteni kwa kunisikiliza!

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...