Charles James, Michuzi TV
KATIKA kusherehekea miaka 43 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha vijana, Mhe Mariam Ditopile amekabidhi Kompyuta 10 zenye thamani ya Sh Milioni Tano.

Mhe Ditopile amekabidhi Kompyuta hizo kwa viongozi wa Wilaya zote za Mkoa huo lengo likiwa ni kurahisisha utendaji kazi wao na kuongeza ufanisi kwa viongozi hao katika kukitumikia chama, wanachama wao na wananchi kwa ujumla.

Tukio hilo limefanyika wilayani Korogwe ambapo Umoja wa Vijana Mkoa wa Tanga uliamua kusherehekea maadhimisho yao kwa kufanya Usafi, kutembelea wagonjwa na wafungwa Kwa ajili ya kuwafariji na kuwapelekea mahitaji yao mbalimbali.

Akiwa katika kituo cha afya cha Korogwe, Mhe Ditopile aliahidi kutoa mifuko 20 ya Saruji ili iweze kusaidia ujenzi wa kituo hicho ikiwa ni jitihada zake za kuunga mkono maendeleo yanayofanywa na serikali katika sekta ya afya.

" Nimefurahishwa kuambiwa tayari wananchi mshaanza kuchangishana kwa ajili ya kujenga ukuta kwenye kituo hiki ambao ndio changamoto kubwa. Huo ndio uzalendo ambao inatakiwa kwa Nchi yetu.

Lakini mimi kama Mbunge kijana Na Mwanamke ninatoa mifuko 20 isaidie ujenzi huo ili kuwepo na uzio kwani siyo jambo jema kila anaepita nje aone ndani haswa katika jengo hili la wazazi. Ni lazima tumpe Mama anayejifungua faragha," Amesema Mhe Ditopile.

Aidha akiongozana na vijana wa UVCCM, Mhe Ditopile ametembelea Gereza kongwe la Korogwe na kukabidhi vifaa vya Usafi pamoja na kuwafariji wafungwa wa Gereza hilo.

Akizungumza na vijana, Mhe Ditopile amewataka kusimama na kuhubiri mafanikio makubwa ambayo yameletwa na Rais Magufuli katika sekta mbalimbali ndani ya kipindi chake cha miaka minne ya uongozi wake.

" Uongozi wa Rais Magufuli umeacha alama, hakuna sehemu ambayo huyu Baba hajagusa. Sekta ya Afya vituo zaidi ya 300 Nchi nzima vinajengwa, madawa na vitanda mahospitalini ni ya kutosha.

Sekta ya elimu amevunja rekodi, elimu bila malipo hadi kidato cha nne. Kiasi cha Bilioni 21 kila mwezi kinalipwa kwa ajili ya watoto wetu. Sisi kama vijana tuna wajibu mkubwa wa kuhubiri mafanikio ya Serikali ambayo kimsingi inatekeleza ilani yetu tuliyowaahidi wananchi mwaka 2015," Amesema Ditopile.
 Kompyuta 10 zenye thamani ya Shilingi Milioni Tano ambazo Mbunge wa Viti Maalum, Mariam Ditopile amekabidhi kwa Viongozi wa UVCCM Wilaya zote za Mkoa wa Tanga leo wilayani Korogwe.
 Mbunge wa Viti Maalum, Mariam Ditopile akizungumza na wanachama na viongozi wa Umoja wa Vijana Mkoa wa Tanga alipokutana nao wilayani Korogwe kuadhimisha miaka 43 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi .
 Mbunge wa Viti Maalum, Mariam Ditopile (kushoto), akikabidhi Kompyuta kwa viongozi wa UVCCM Mkoa wa Tanga kwa ajili ya kusaidia utendaji kazi wao ikiwa ni ahadi yake kwa Umoja huo.
 Mbunge wa Viti Maalum, Mariam Ditopile akikagua kituo cha afya ya Korogwe ambapo ameahidi kutoa mifuko 20 ya Saruji kwa ajili ya ujenzi wa Uzio wa Ukuta kwenye kituo hicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...