Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB
akiongea katika kikao kazi kilichofanyika mkoani Morogoro kuanzia
Februari 3 – 4, 2020 kwa lengo la kuandaa muongozo utakaotumika kufanya
ufuatiliaji na ukaguzi wa Magereza na maeneo mengine walipozuiliwa watu.
Kulia ni Kalliopi Kambanella, Mwanasheria kutoka Dignity. Wa kwanza
kushoto ni Mkurugunzi kutoka THBUB, Alexander S. Hassan, wa pili kushoto
ni Una Marquards-Busk, Meneja Mradi kutoka DIGNITY na wa tatu ni
Kamishna Dkt, Fatuma Rashid Khalfan.
Kamishna Dkt, Fatuma Rashid
Khalfan akiongea wakati akifungua kikao kazi kilichofanyika mkoani
Morogoro kuanzia Februari 3 – 4, 2020 kwa lengo la kuandaa muongozo
utakaotumika kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa Magereza na maeneo
mengine walipozuiliwa watu.
Una Marquards-Busk, Meneja Mradi kutoka DIGNITY akitoa maelezo mafupi kuhusu taasisi ya DIGNITY na lengo la kikao kazi hicho.
Kamishna Dkt, Fatuma Rashid
Khalfan (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa
kikao kazi pamoja na maafisa kutoka taasisi ya Dignity.
……………………………………………………………………………………
Na Mbaraka Kambona,
Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora (THBUB) kwa kushirikiana na taasisi ya DIGNITY kutoka
Denmark wamekutana na wadau mbalimbali wa haki za binadamu kuandaa
muongozo wa ukaguzi na ufuatiliaji wa Magereza nchini.
Wadau hao wamekutana katika kikao
kazi kinachofanyika mkoani Morogoro kuanzia Februari 3 – 4, 2020 kwa
lengo la kuandaa muongozo utakaotumika kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa
Magereza ili kuboresha maeneo hayo.
Kikao kazi hicho kilichojumuisha
wadau mbalimbali wa masuala ya haki za binadamu kimelenga pia
kubadilishana uzoefu katika masuala ya ukaguzi na ufuatiliaji wa maeneo
wanapozuiliwa watu ikiwemo magerezani, mahabusu na vituo vya polisi kwa
lengo la kujenga uelewa wa pamoja.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa
kikao kazi hicho, Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,
Mhe. Dkt. Fatuma Rashid Khalfan alisema kuwa kikao kazi hicho ni fursa
nzuri kwa tume na wadau wengine kuboresha mbinu utendaji wao wa ukaguzi
na ufuatiliaji wa maeneo wanapozuiliwa watu.
“Kikao kazi hiki ni fursa nzuri
kwetu sote kama wadau kubadilishana uzoefu katika hatua za msingi za
kufanya ufuatiliaji na ukaguzi na kukubaliana namna nzuri ya uandaaji wa
muongozo wa ufuatiliaji na ukaguzi wa maeneo wanapozuiliwa watu”,
alisema Dkt. Fatuma
Aliendelea kusema kuwa kikao kazi
hicho kinaenda sambamba na jukumu la kikatiba la tume la kutembelea
magereza na maeneo walimozuiliwa watu na kutoa mapendekezo mahususi kwa
serikali ili kuboresha maeneo hayo.
Dkt. Fatuma alieleza kuwa kikao
kazi hicho kimefanyika wakati muafaka ambapo Wizara na Taasisi
mbalimbali za serikali na binafsi zikiwa katika juhudi kubwa ya
kuboresha mazingira na maisha ya wafungwa nchini.
“Katika jitihada hizo, siku ya
Maadhimisho ya Uhuru, Disemba 9, 2019 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa 5533 kwa
lengo la kupunguza msongamano magerezani”, aliongeza Dkt. Fatuma
“Tume inaendelea kupongeza maamuzi
hayo ya Rais, hivyo ni mategemeo yetu kuwa taasisi nyingine za serikali
na zisizo za serikali zitaendelea kushirikiana na tume katika utatuzi
wa changamoto zinazokabili Magereza na maeneo mengine wanapozuiliwa
watu”, alisisitiza Dkt. Fatuma
Aliongeza kuwa kikao kazi hicho
kitaleta matokeo ambayo yatapelekea kuimarika kwa uhamasishaji na ulinzi
wa haki za watu walioshikiliwa kulingana na miongozo ya kimataifa,
kikanda na kitaifa ya haki za binadamu.
Aidha, Dkt. Fatuma aliishukuru
taasisi ya DIGNITY ya Denmark kwa kuwezesha kikao kazi hicho na kuwataka
washiriki kutumia kikao kazi hicho kujifunza na kubadilishana uzoefu
kwa lengo la kuboresha maeneo walipozuliwa watu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...