Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Mhe. George Simbachawene akichukua kipande cha nyama kavu iliyokaushwa na viungo maalum kwa ajili ya kuonja alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Maonesho ya Nane Nane, Dodoma Mwishoni mwa Wiki. Kulia ni Afisa Mauzo wa Kampuni ya Ina’s, Hussein Juma.

………………………………………………………………………….

Na Mbaraka Kambona, Dodoma

Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Mhe. George Simbachawene amewashauri wafugaji kubadilika na kufanya ufugaji wa kisasa na wenye tija kwani ufugaji wa kienyeji pamoja na kuwa na tija ndogo, pia umekuwa ndio chanzo kikuu cha migogoro ya ardhi na uharibifu wa Mazingira nchini.

Simbachawene aliyasema hayo alipotembelea Maonesho ya Nane Nane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, Kanda ya Kati, Dodoma Mwishoni mwa wiki ( Agosti 7, 2020).

Akiwa katika banda la Maonesho la Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Simbachawene alisema wafugaji wazingatie ushauri wa wataalamu na kufanya ufugaji wa kisasa ambao unahimiza kuwa na ng’ombe wachache wenye tija kuliko kuwa na ng’ombe wengi ambao tija yao ni ndogo.

“Ni lazima wafugaji wafikirie kubadilika ili waende na hali halisi ya gharama za uzalishaji, ifikie hatua wafugaji waanze kufuga kibiashara, ili mfugaji anapotaka milioni moja au mbili aipate kwa kuuza ng’ombe mmoja na sio kuuza kundi la ng’ombe ili aweze kupata hiyo pesa,”alisema Simbachawene

“Unakuta mfugaji huyo ana ng’ombe karibu 500, kwa nyama hawafai, kwa maziwa hawafai, ng’ombe wamekonda na yeye mwenye kakonda, kimsingi ni hasara juu ya hasara lakini pia migogoro ni mingi kati ya wakulima na wafugaji, na wanasababisha uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa, hivyo ni muhimu wafugaji wetu wakafundishwa na kuelekezwa kubadilika na kufuga kisasa,”aliongeza Simbachawene

Aliendelea kueleza kuwa Serikali na taasisi zake wamefanya kazi kubwa ya kufanya utafiti mbalimbali wa kuboresha mifugo ikiwemo upatikanaji wa madume bora, mbegu bora za malisho na kutenga maeneo maalum kwa ajili ya malisho.

“ Serikali imehakikisha kuwa karibu kila kanda huduma za kupandikiza mbegu bora kwa ng’ombe majike zinapatikana hivyo ni suala la wananchi kuwa tayari kutumia huduma hizo ili kufanya ufugaji wa kisasa,”alifafanua Waziri huyo

Aidha, Simbachawene alitoa rai kwa viongozi kuanzia ngazi ya kata na Wilaya kuona uwezekano wa kufanya maonesho hayo katika maeneo yao ili wananchi wanaoishi vijijini huko waweze kuendelea kupata fursa ya kujifunza na kuangalia ubunifu mbalimbali utakaowasaidia kuboresha ufugaji wao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...