Charles James, Michuzi TV

WIZARA ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Taasisi yake ya Chakula na Lishe imewapatia waandishi wa habari semina yenye lengo la kuwapa ufahamu kuhusu masuala ya lishe ya watoto wachanga na wadogo.

Semina hiyo imefanyika leo jijini Dodoma ikiwa ni mahususi katika Wiki hii ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama duniani ambapo Tanzania kama zilivyo nchi zingine inaadhimisha wiki hiyo ambayo hufanyika kila Agosti 1-7 ya kila mwaka.

Akizungumza katika semina hyo, Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Huduma za Lishe Wizara ya Afya, Grace Moshi amesema mafunzo hayo yatawasaidia wandishi katika kuimarisha majukumu yao ya utoaji wa taarifa sahihi kwa jamii juu ya ulishaji sahihi wa watoto na hasa unyonyeshaji.

Amesema wiki ya unyonyeshaji wa mwaka huu inaeleza uhusiano uliopo kati ya unyonyeshaji watoto maziwa ya mama na afya bora pamoja na kulinda mazingira ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo inasema " Tuwawezesha wanawake kunyonyesha watoto kwa afya bora na ulinzi wa mazingira".

Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni fursa muhimu ya kutoa hamasa kwa jamii katika kulinda, kuimarisha na kuendeleza unyonyeshaji ambao umekua suluhisho ambalo linampa kila mtu msingi imara wa mwanzo wa maisha na husaidia kuboresha afya na ustawi wa wanawake na watoto duniani kote.

Kwa upande wake Afisa Lishe Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe, Mary Kibone amewataka wandishi kutumia kalamu zao katika kuandaa makala na vipindi mbalimbali vinavyohamasisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa mtoto.

Amewataka akina Mama kuwa na utaratibu wa kunyonyesha watoto mara kwa mara ili kuongeza utokaji wa maziwa na kusaidia kupata maziwa yenye maji mengi ambayo hukata kiu ya mtoto.

Amezitaja faida za mtoto kunyonya maziwa maziwa ya mama kuwa ni kusaidia kinga dhidi ya maradhi mbalimbali kama kuhara na magonjwa ya hewa pamoja na kumpatia mtoto virutubisho vyote kwa uwiano sahihi kwa ukuaji wa maendeleo yake.

Kibone amzitaja faida pia za mama kunyonyesha ikiwemo kusaidia tumbo la uzazi kurudi katika hali ya kawaida na kuzuia uwezekano wa upungufu wa damu kwa mama.

" Niwasihi wandishi kuhamasisha akina Mama wanaonyonyesha watoto wenye umri chini ya miezi sita kutowapa vyakula vingine kwani kiafya sio nzuri na vyakula hivyo vina madhara kwa mtoto mwenye umri chini ya miezi sita.

Madhara ambayo yanaweza kumpata mtoto anayepewa vyakula vingine tofauti na maziwa ya mama akiwa na umri chini ya miezi sita ni pamoja na Utapiamlo, Kupata Mzio (Allergy), Magonjwa ya kuhara, Kupunguza uhusiano kati yake na mama na kupata uzito uliozidi," Amesema Kibone.
Afisa Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe, Mary Kibone akitoa mada ya faida ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa mtoto katika semina waliyoiandaa mwa wandishi wa habari jijini Dodoma kuwajengewa uelewa wa masuala ya lishe na chakula cha watoto wachanga na wadogo.

 Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Huduma za Lishe Wizara ya Afya, Grace Moshi akieleza dhumuni la mafunzo na semina hiyo waliyoiandaa kwa wanahabari wa vyombo mbalimbali jijini Dodoma leo.
 Wandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali jijini Dodoma wakifuatilia mafunzo maalum yaliyoandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe juu ya Wiki ya Unyonyeshaji duniani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...