Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Tanga

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli ameendelea kuchanja mbuga kwa kufanya mkutano mkubwa katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga huku akitumia nafasi hiyo kuelezea mambo makubwa ya maendeleo yatakayofanyika katika mkoa huo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Dk.Magufuli ameeleza mikakati iliyopo katika kurudisha heshima ya Mkoa wa Tanga ambayo hapo zamani ilikuwa na viwanda vingi na kwamba anataka kufanya majaabu makubwa kuendeleza mkoa huo na anataka uwe kitovu cha uchumi.

Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Korogwe na Mkoa wa Tanga kwa ujumla leo Oktoba 20, mwaka huu 2020 wakati akiomba kura kwa wananchi hao ili achaguliwe tena kuongoza nchi kwa kipindi kingine cha miaka mitano, Dk.Magufuli amesema anaufahamu mkoa huo na historia yake , hivyo amejipanga kurejesha heshima yake kama ilivyokuwa zamani.

"Tumejipanga kufanya maaajabu katika Mkoa wa Tanga , mkoa wenye historia tangu enzi za ukoloni, ndio mkoa ambao Wajeruman walijenga shule ya kwanza na ndio tukapata neno shule,"amesema Dk.Magufuli na kusisitiza Jiji la Tanga ni miongoni wa majiji ya kwanza kabisa nchini na kwamba hata kwa upande wa viwanda Tanga ilikuwa na viwanda vingi ambavyo vilitoa ajira nyingi kwa wananchi na kwamba mkoa huo ulikuwa na kila kitu lakini umaarufu wake ukashuka.

Dk.Magufuli amesema katika kipindi cha miaka mitano kuna mambo makubwa ya maendeleo yamefanyika katika sekta mbalimbali za kijamii na maendeleo hayo yamefanyika na mkoani Tanga na wananchi ni mashahidi kwani yaliyofanyika wanayaona na wagombea ubunge na udiwani wamekuwa wakiyaelezea vizuri.

Amewaeleza wananchi wa mkoa huo katika kipindi cha miaka mitano ijayo iwapo watachaguliwa kuongoza nchi wamejipanga kuendeleza miradi ya maendeleo ya mkoa huo ikiwa pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara, maji, elimu, afya, reli na huduma nyingi za msingi.

Amezungumzia mkakati wa Serikali ambao umefanyika wa kuifufua reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Arusha ambayo imepita Korogwe mkoani Tanga na kwamba kupita kwa reli hiyo katika mkoa huo kunafungua fursa kwa wananchi kujiimarisha kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali za kimaendeleo ambazo watakuwa wakizifanya.

"Tulipoingia madarakani mwaka 2015 tuliamua kuanza kuifufua reli hii ya Dar es Salaam hadi Arusha , tunataka hii reli ambayo imepita hapa itumieni kwa kufanya biashara,"amesema Dk.Magufuli na kuongeza kuwa mkakati wa kuimarisha miundombinu ya usafirishaji unalenga kutoa nafasi kwa wananchi kuamua wanataka kutumia magari, reli, meli usafiri wa ndege kwani tunakwenda kuupanua uwanja huo na ndege kubwa zitatua hapo.

Pamoja na hayo amewaeleza wananchi hao kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta ambalo litatoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleeni mkoani Tanga ambalo litakuwa na urefu wa kilometa 1445 ambapo gharama za ujenzi wa bomba hilo ni Sh.trilioni nane."Bahati nzuri bomba hilo kwa Tanzania nzima litapita katika Wilaya 24 na unakwenda kutengeneza ajira 15,000. Kwa hapa Tanga utapita katika Wilaya za Kilindi, Handeni, Korogwe, Muheza na Tanga, utapita katika kata 25 na vijiji 46."

Amefafanua uwepo wa bomba hilo unakwenda kufungua fursa nyingine za kiuchumi kwa wananchi kwani kuna watu wafanya kazi katika ujenzi, wenye gesti watapata wageni, mama lishe watauza chakula pamoja na shughuli nyingine za kimaendeleo zitafanyika na kwamba tayari fidia ya Sh.bilioni tatu zimeanza kulipwa kwa wananchi ambao mradi utawapitia.

Dk.Magufuli amesema kwa mipango hiyo na mingine iliyopo katika Ilani ya Uchaguzi ndio maana anawaeleza wananchi wa Tanga kwamba mkoa huo unakwenda kufunguka kiuchumi na ndio mkakati wa Serikali ya CCM.Amewaambia wananchi kuwa ili maendeleo yafanyike lazima yapangwe na yasipopangwa hakuna ambacho kitafanyika.

Katika mipango hiyo ndio maana Serikali katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ilikuwa na kazi ya kuboresha na kuimarisha miundombinu mbalimbali kwani hata unapozungumzia bima ya afya lazima uwe na majengo, uwe na madkatari, uwe na bajeti ya dawa ya kutosha, vifaa tiba na wataalam na hiyo ndio imefanyika.

Katika kujenga huko miundombinu, imesababisha hata uchumi wa Tanzania kupanda na sasa iko uchumi wa kati na baada ya kuimarisha uchumi kazi inayokwenda kufanyika ni kuboresha maslahi ya wafanyakazi huku akieleza Serikali inaendelea na mchakato wa kulipa malimbikizo ya madeni ya wafanyakazi."Miaka mitano ijayo tunakwenda kuboresha maslahi ya wafanyakazi."

Akifafanua zaidi katika eneo la uchumi, amesema katika nchi 10 barani Afrika ambazo uchumi wake uko imara ,Tanzania ni miongoni mwao na kwamba Tanzania ina kila kitu, ni chi tajiri.

Kwa upande wa elimu, Dk.Magufuli amesema kwa Mkoa wa Tanga Sh.bilioni 55.7 zimetolewa kwa ajili ya elimu bure na Sh.bilioni 17.8 zimetumika kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu.Wakat katika afya Sh.bilioni 17.4 zimetolewa kujenga jengo la wagonjwa wa dharura na jengo la kuchuja damu kwa wagonja wa figo katika Hospitali ya Mombo.

Katika maji, Dk.Magufuli amesema jumla ya miaradi ya maji maji 64 imetekelezwa katika mkoa huo ukiwemo wa mradi wa maji Pongwe-Muheza kwa Sh.bilioni 3.07 ambao umefikia asilimia 85 na mradi wa maji wa Mabokweni uliogharimu Sh.bilioni 2.4 unaotelekezwa kwenda Mekeleni,pia kuna mradi wa maji Shume,Mwanolo na Madala wa Sh bilioni 2.64 pamoja na mradi wa maji wa Kibingo.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...