MKUU wa Mkoa wa
Mwanza Mhe. John Mongella ameaagiza watendaji wote wanaohusika na usajili wa
Vizazi na Vifo kuweka mikakati itakayowezesha wananchi katika maeneno yao
kusajiliwa ili kuwaondolea usumbufu wa kutokuwa na nyaraka mara wanapohitaji
huduma nyingine.
Hayo yamesemwa
hii leo Jijini Mwanza kupitia hotuba ya Mkuu wa Mkoa huo iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya
ya Nyamagana Mhe.Dkt. Philis Nyimbi wakati wa kufungua mafunzo kwa Makatibu Tawala wa Wilaya na
Maafisa Tarafa wa Mkoa huo yaliyoandaliwa
na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) yatakayosaidia kutekeleza
majukumu yao ya usajili wa Kizazi,Vifo, ndoa na talaka kikamilifu.
Ameeleza kwamba umuhimu
wa nyaraka mbalimbali zinazotolewa na RITA unaendelea kuongezeka hivyo lazima
kuwe na mkakati wa kuwaelimisha wananchi kujisajili na kuwe na mikakati mahsusi
itakayowezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma kwa wakati.
Mhe. Mongella
amewapongeza RITA kwa hatua ambazo wanaendelea kuchukua katika kuboresha mfumo
wa usajili kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu
na Takwimu ambao unaendelea kutekelezwa kupitia Progam Mbalimbali. Ameongeza
kwamba Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano umeleta
matokeo chanya kwa kuwawezesha watoto kupata cheti cha kuzaliwa karibu na
maeneo wanayoishi ambapo na takwimu zake zimepatikana na kutumika katika
kupanga mipango ya maendeleo.
Mhe. Mongella amewapongeza RITA kwa kuandaa mafunzo haya kwani inawezekana baadhi ya watendaji katika ofisi za Wilaya ni wageni katika nafasi hizo hivyo mafunzo haya yataongeza ufanisi. Amewataka washiriki kuzingatia mafunzo wanayopata na kuwataka kutunza Miongozo wanayopewa ili iwasaidie watendaji wengine siku za usoni.
Akizungumzia
huduma za Mirathi na Wosia, Mhe. Mongella amewaonya baadhi ya wananchi hasa ndugu na jamaa wa karibu wa marehemu ambao wamekuwa na tabia za mnyanyasaji na uporaji wa mali za marehemu
mara baada ya mazishi na hivyo kusababisha uvunyifu wa amani, upotevu wa mali
na kuwanyima haki warithi halali kwa kigezo kwamba wao ni wasimamizi wa
mirathi.
"Nawasihi
viongozi wenzangu tutoe elimu kwa wananchi wetu kuanzia sasa wajenge utamaduni
wa kuandika wosia mapema na waondokane na dhana mbaya kwamba ni uchuro,dhana
hii siyo sahihi kama kufa tutakufa tu na kuacha matatizo makubwa ya ndugu
kugombania mali".Alisema Mhe. Mongella.
Kwa upande wake
Kaimu Mkurugenzi wa Msaada wa haki za kisheria kutoka RITA Bi. Lina Msanga
amesema kuwa sheria imetamka wazi kwamba kila tukio la kizazi, kifo, ndoa na
talaka yanapotokea lazima yasajiliwe na kuhifadhiwa katika daftari la Msajili
Mkuu wa matukio hayo ambaye ni Kabidhi Wasii Mkuu.
" Usajili ni
takwa la kisheria lakini kuna sehemu kama watumishi wa umma hatutekelezi
ipasavyo majukumu yetu na ndiyo maana leo hii tupo hapa kuwapatia mafunzo
Maalum kuhusu sheria na miongozo mbalimbali itakayowasaidia kutekeleza majukumu
yenu".Alisema Bi. Msanga.
Vilevile Katibu
Tawala wa Wilaya ya Kwimba Ndugu Nyakia Chirukile amesema kuwa baadhi ya
viongozi wa dini na kimila wamekuwa wakifungisha ndoa bila ya kufuata utaratibu
na sheria hivyo kutosajili na kusababisha migogoro na hata vifo kwa wanandoa.
" katika
wilaya yangu kuna binti ameozeshwa kimila na umri wake ulikuwa mdogo sana na
hivyo kupata matatizo ya uzazi kwa kupungukiwa damu, tulimsaidia damu kwa
bahati mbaya ndugu zake wakamtoroshwa kwa kuogopa vyombo vya
sheria".Alisema Chirukile.
Kwa upande wake
Afisa Tarafa ya Katunguru Bw. Batalangile Kaswahili amesema kuwa kukosekana kwa
uadirifu na uwajibikaji kwa watumishi waliopewa dhamana ya kuwahudumia wananchi
ndiyo chanzo kinachosababisha kukosekana kwa uratibu mzuri wa kuyasajili
matukio mbalimbali yanapotokea.
" kwa mfano
mimi katika Tarafa yangu nimepewa pikipiki nashindwaje kufuatilia utendaji kazi
wa maafisa watendaji wa kata na vijiji
ili wanipe hizo taarifa? huu ni usembe wetu sisi watumishi wa
umma".Alisema Bw. Kaswahili.
RITA inaendelea
kutoa mafunzo kwa Makatibu Tawala, maafisa Tarafa, maafisa watendaji kata na
Watumishi wa vituo vya tiba vinavyotoa huduma ya mama na mtoto katika Mikoa
yote ya Tanzania bara lengo likiwa ni kuwajengea uwezo katika uwajibikaji na
kuongeza kasi ya usajili wa matukio hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...