Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Pauline Gekul ametoa rai kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kutoa elimu kuhusu mawakala wa michezo na kwa siku za usoni  itengeneze kanuni zitakazowasimamia mawakala hao.

Mhe.Gekul ametoa rai hiyo Julai 30 alipofungua Kongamano la wadau wa mpira wa miguu (Tanzania Football Summit 2021) linalofanyika kwa siku mbili Jijini Da er Salaam ambapo amesema ni vizuri wachezaji wote na vilabu kutumia  mawakala pale wanaposajili wachezaji.

"Tanzania mpaka karne hii tuna mawakala takribani  6 tu nchi nzima ambao wanatambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) ikiwemo AFRISOCCER Kampuni iliyoandaa kongamano hili, Idadi hii ni ndogo sana hairidhishi na  hii inamaanisha wachezaji na wadau wa soka bado hawajafahamu umuhimu wa kutumia mawakala katika soka" amesema Mhe.Gekul

Naibu Waziri Gekul ameongeza kuwa Dunia ya sasa inakwenda kidijitali wachezaji wanauzwa na kutafutiwa timu kwa kutumia tovuti (Websites) na mifumo mbalimbali, pia taarifa za vilabu, wachezaji, makocha na mawakala katika ulimwengu wa sasa zinahifadhiwa kidijitali, Wachezaji wa kisasa wanafuata ratiba za mazoezi, aina za mazoezi na vyakula kidijitali. Hivyo ni wakati sasa  nchi yetu kukimbizana na ulimwengu wa teknolojia hiyo.

"Matumizi ya mawakala yatapunguza kama sio kuondoa migogoro ya kunyang’anyana wachezaji kabla ya mikataba baina ya vilabu, Pia itapunguza migogoro kati ya wachezaji na vilabu kwakuwa pale unapotokea mgogoro kati ya mchezaji na klabu, klabu itawasiliana na wakala wa mchezaji husika badala ya kuwasiliana moja kwa moja na mchezaji. Pia mchezaji atapata muda wa kuendeleza kipaji chake  badala ya kuwaza kujitafutia timu au kusuluhisha migogoro kati yake na klabu"amesisitizs Mhe.Gekul.

Kongamano hilo  la siku mbili tarehe 30 na 31 Julai 2021  litakua na mada mbalimbali na litawakutanisha pamoja wadau tofauti tofauti, Maafisa Michezo, viongozi wa vyama vya mpira wa miguu, waalimu wa michezo, waamuzi, wachezaji, wakala wa wachezaji na waandishi wa habari za michezo ambapo watapata fursa ya majadiliano, kubadilishana mawazo  na mafunzo kutoka kwa wataalamu na wawezeshaji wenye taaluma na ubobevu katika maeneo tofauti katika medani ya soka.





 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...