Adeladius Makwega,Chamwino- WHUSM

 

Katika sehemu ya awali ya makala haya nilimalizia juu ya taarabu asilia kuwa ipo ile inayochezwa na wanawake pekee na ile inayochezwa na wanaume. Hii ni kulingana na mazingira ya watu hao, haswa kwa kuiga mitindo ya taarabu za Kiarabu.

 

Makala haya katika sehemu ya pili leo yanatupia jicho juu ya mianisho ya mashairi ya taarabu asilia. Kulingana na Bi Hadija Kisubu Afisa Utamaduni wa Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo anasema kuwa Waswahili wameainisha ushairi wao katika mistari mitatu: shairi lenye mistari minne katika kila ubeti, utenzi-shairi refu lenye mistari mitatu au minne katika kila ubeti na ambalo huwa limetungwa kama utenzi) na wimbo (shairi lenye mistari mitatu lililotungwa ili liimbike).

 

“Taarabu imeainishwa katika aina ya tatu ya wimbo wenye mistari mitatu katika kila ubeti na mistari wa nne ujulikanao kama kiitikio au kibwagizo. Hata hivyo, kwa mujibu wa wanajadi wa taarabu, kuna Taraab aina moja tu ambayo hufuata mtindo wa mapigo ya taratibu huku wasikilizaji wake wakiwa wametulia tuli kama maji ya mtungini na kusikiliza wakiwa wameketi kitako.” Anaongezea Bi Kisubi.

 

Tofauti na maoni haya ni yale ya wanamapinduzi ambao wanasema kuwa kuna taarabu ya sasa ambayo imeiga midundo mipya na mabadiliko katika uchezaji ngoma na mavazi ya wasanii. Hili limesababishwa na haja ya muziki huu kubadilika kadri wakati ulivyozidi kubadilika kiuchumi, kisiasa na kijamii.

 

Mtaalamu huyu wa masuala ya utamaduni anaelezea kuwa historia ya taarabu imepitia katika vipindi vinne, cha kwanza ni mwaka 1905 hadi 1920. Huu ndio wakati ambapo Sultan Seyyid Bargash alikuwa mtawala wa Zanzibar. Taarabu iliimbwa katika ikulu yake kwa lugha ya Kiarabu kama ilivyokuwa imeigwa kutoka Misri.

 

Wachunguzi mbalimbali wa muziki huu wanasema kuwa uliletwa Zanzibar mnamo 1870 na kikundi cha wanamuziki kutoka Misri kilichokuwa kimealikwa na Sultan Barghash kuimba ikuluni mwake (kama nilivyokudokeza katika makala ya kwanza).

 

Kwa kipindi hiki Zanzibar ilikuwa ngome muhimu ya kibiashara chini ya utawala wa Kiarabu wa Sultani wa Oman. Nyimbo za taarabu katika nyakati hizo zilitumiwa katika kuwatumbuiza viongozi wenye asili ya Kiarabu, wafanyibiashara na mabepari. Sultan Sayyid Bargash aliishi maisha ya anasa na alipenda raha na starehe sana.

 

Baada ya kufanikiwa katika wajibu wake huu, Mohammed alirudi ikuluni mwa Barghash, na baadaye akawa mshairi wa kibinafsi wa Barghash. Mohammed pia aliwafunza marafiki zake kucheza muziki huu, ujuzi walioutumia baadaye walipoanzisha kikundi cha kwanza cha taarabu kilichojulikana kama Nadi Ikhwani Safaa, mwaka 1905 kule Zanzibar.

 

“Taarabu ilisambaa kwingineko katika mwambao wa Afrika Mashariki ikiwemo Mombasa na Lamu. Maudhui katika nyimbo za taarabu zilizoimbwa katika ikulu ya mfalme yalihusu kuomba dua ya mapenzi kati ya Sultan na Malkia, kumwombea Sultan maisha marefu katika utawala wake, kusifu maumbile, huku nyimbo zingine zikiimbwa kwa nia ya kumchangamsha na kumchekesha mfalme. “ Anasema Bi Amne Kassam Afisa Utamaduni wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo.

 

Bi Kassam anasema kuwa watu wa tabaka la juu wakati huo walivaa mavazi yao nadhifu na kuketi vitini wakingoja kutumbuizwa na kikundi hiki cha Nadi Ikhwani Safaa .

 

Mwaka wa 1920 hadi 1940 hiki kilikuwa ni kipindi cha pili cha taarabu. Katika muhula huo, lugha ya Kiswahili ilitumika katika nyimbo za taarabu baada ya enzi ya utawala wa Sultan Barghash kufikia kikomo. Mabadiliko ya muziki wa huu yalisababisha kubadilika kwa hadhi ya nyimbo hizi kutoka kuwa nyimbo za watu wa tabaka la juu katika jamii hadi kuwa nyimbo za makabwela (akina yakhe). Mabadiliko haya yalihusishwa na mhusika wa taarabu aliyesifika sana Zanzibar na nchi za nje,Bi Siti binti Saad.

 

Taarabu ilianza kuwafikia watu wengine mbali na watawala na matajiri baada ya kuwepo kwa utendaji hai wa bendi mbele ya umma na pia kuwepo kwa mbinu ya kurekodi nyimbo hizi. Watu wa tabaka la kati waliweza kuzinunua na kuzisikiza nyimbo za taarabu. Huu ndio wakati ambao Siti Binti Saad, aliyeishi miaka ya 1880-1950, alianza kuimba akitumia lugha ya Kiswahili Zanzibar na Tanganyika.

 

“Siti alifanikiwa kuimba nyimbo nyingi sana za Kiarabu na Kiswahili katika santuri na sahani.Taarabu wakati huo iliweza kuenea hata zaidi kwani Siti alikuwa na uwezo wa kuimba kwa lugha za Kihindi, Kiarabu na Kiswahili. Uwezo huu wa kuchanganya lugha tofauti tofauti katika uimbaji wake uliweza kumpa Siti hadhi kubwa visiwani na kulikokuwa na utamaduni mseto wa Kiarabu na Kiswahili.” Anaongeza Bi Kassam.

 

Ndiyo maana baadhi ya watafiti wa muziki huu wanadai kuwa kwa Waafrika wengi, taarabu kwao ilianza na Siti. Aidha, Siti alianzisha aina ya taarabu iliyojulikana kama Womens’ taarabu ambayo ilikopa sana kutoka utamaduni wa nyimbo za Waswahili na za Kihindi. Siti aliifanya Taarabu kuwa ya Kiafrika kwa kuimba kwa Kiswahili na kuitoa nje ya kasri la kifalme kwa kuiwasilisha kwa watu wa kawaida.

 

Mwaka 1950 hadi 1960 kilikuwa ni kipindi cha tatu cha taarabu ambapo iliweza kuwa huru zaidi kutokana na kuwepo kwa upeperushaji wake katika mawimbi ya redio mbalimbali. Muziki wa taarabu uliweza kusambaa sana katika awamu hii. Katika kipindi hiki utakumbuka kuwa watawala wa kikoloni na Sultan wa Zanzibzr waliweza kusimika mitambo ya kurushia matangazo ya redio na ya kurekodi muziki na nyimbo  za kila aina.

 

Kuanzia mwaka wa 1970 hadi sasa. kumekuwa na ufanisi mkubwa zaidi wa taarabu uliochangiwa na kuwepo kwa runinga, video, tepurekoda,simu za mikononi, na mitandao hivyo ni miongoni mwa vifaa vingine vya kisasa vya kielektroniki. Taarabu imeweza kuenea hadi Msumbiji, Afrika Mashariki, sehemu za Maziwa Makuu kama vile Kongo, Afrika Kaskazini, Magharibi na Mashariki, Bahrain, Yemeni, Saudi Arabia, Uturuki na Bara Hindi.

 

“Mabadiliko katika uimbaji na utendaji yanayoonekana katika muziki wa taarabu ya kileo yamesababishwa na haja ya kuubadilisha muziki huu ili uweze kuambatana na mitindo na aina ya muziki wa kisasa. Utendaji wa muziki wa taarabu umeiga mengi kutoka tanzu nyingi.” Alimalizi Bi Kisubi.

 

Basi kwa leo naweka kalamu yangu chini ili kuweza kukuandalia makala ijayo kwa heri.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...