Oscar Munisi ambaye ni mwenyekiti wa makandarasi Mkoa wa Mwanza akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Injinia Consolata Ngimbwa mara baada ya kufungwa kwa mafunzo ya siku tatu kwa makandarasi wazalendo kuhusu usimamizi wa fedha. Kushoto ni Naibu Msajili wa CRB, anayeshughulikia utafiti na maendeleo Injinia David Jere.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Injinia Consolata Ngimbwa akizungumza na maofisa wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) mara baada ya kufunga mafunzo ya siku tatu ya usimamizi wa fedha na kodi yaliyofanyika Mkoani Mwanza.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Injinia Consolata Ngimbwa akiwa kwenye picha ya pamoja na makandarasi wa mikoa mbalimbali mara baada ya kufunga mafunzo ya siku tatu kuhusu usimamizi wa fedha na kodi iliyofanyika Mkoani Mwanza.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Injinia Consolata Ngimbwa akifunga mafunzo ya siku tatu kwa makandarasi wazalendo kuhusu usimamizi wa fedha na masuala ya kodi yaliyofanyika ukumbi wa chuo cha Benki Kuu jijini Mwanza

*Yawataka wakatae kutoa rushwa kwenye zabuni

Na Mwandishi Wetu
MAKANDARASI nchini wametakiwa kutoa taarifa kwa Taasisi ya Kupambana na kuzuia Rushwa Takukuru) wanapoombwa rushwa na watoaji wa zabuni ili wawawezeshe kupata miradi hiyo ya ujenzi.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki mkoani Mwanza na Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi, Mhandisi Consolata Ngimbwa wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa makandarasi wazalendo.

Ameema makandarasi hawapaswi kutoa rushwa wala kuwashawishi wengine kupokea rushwa kutoka kwao na kwamba iwapo watafanya kazi kwa weledi na maadili rushwa haitakuwa na nafasi kwenye shughuli zao za ujenzi.

“Tukikubali kubadilika wote tutaibadilisha na kuiboresha sekta ya ukandarasi hapa nchini hivyo nawasisitiza mjiepushe kabisa na vitend vya kutoa na kupokea rushwa,” alisema

Pia amewataka makandarasi kushirikiana kupitia ubia kama njia ya kuwawezesha makandarasi wazalendo kupata fursa ya kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi.

Amesema kutimiza masharti ya miradi mikubwa ni vigumu kwa makandarasi wengi wanapokuwa mmoja mmoja lakini kwa mfumo wa ubia wanaweza kuyatimiza masharti hayo na kushinda zabuni hivyo amewataka makandarasi wote kuwa na chama kimoja kitakachokuwa sauti yao kwani sekta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo haziwezi kutatuliwa kwa urahisi bila kuwa na umoja wenye nguvu.

"Mtakumbuka kwamba nimekuwa nikilisema hili kwa muda mrefu sana mliohudhuria mikutano ya mashauriano ni mashahidi, umoja ni jambo ambalo nalisisitiza sana kote nchini na nafurahi nimekaa na wenyeviti wa vyama vya makandarasi nao wameona umuhimu huo, “ amesema Injinia Ngimbwa

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa (CRB) anayeshughulikia Utafiti na Maendeleo, Injinia David Jere amesema mafunzo hayo yamehuhduriwa na washiriki 92 wa aina na madaraja mbalimbali kutoka Kanda ya Ziwa na mikoa mingine nchini.

Amesema mafunzo hayo ya usimamizi wa fedha yamelenga kuwasaidia makandarasi kuwa na uelewa wa usimamizi wa rasilimali fedha hususan taarifa za mizania au balance sheet na kwamba washiriki wa mafunzo hayo wamejifunza masuala ya kodi hususan namna nzuri ya kutunza kumbukumbu ili kuepuka kodi zisizostahili au faini kama adhabu kwa kukiuka misingi muhimu ya uandaji wa mahesabu ya fedha za kampuni.

Injinia Jere amesema mafunzo hayo ni endelevu na mengine yanatarajiwa kufanyika kwa nyakati tofauti kwenye mikoa ya Iringa, Dar es Salaam na Dodoma.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanafanyika lengo ikiwa ni kuwajengea uwezo makandarazi wazalendo kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi ambayo sasa hivi inafanywa na kampuni za kigeni.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...