BENKI ya Absa Tanzania imesisitiza dhamira yake katika kujenga  ushirika na  makapuni yanayoibuka yenye ubunifu nchini katika kuanzisha miradi  ya kibiashara ambayo itakuwa na  faida kwa pande zote mbili,  ofisa wa ngazi ya juu wa benki hiyo ya kimataifa amesema leo mjini Dar  es Salaam katika warsha iliyoandaliwa kuzipa nafasi kampuni zinazoibuka kuonesha miradi yao ya kibiashara.

Warsha hiyo, iliyokuwa na kauli mbiu ya Uboreshaji wa Huduma kwa Wateja kwa njia ya Kidijitali na Ubunifu, iljikita katika kubainisha namna gani mabadiliko ya kidijitali yanaweza kusambazwa kwenye  sekta mbalimbali nchini  sambamba na uboreshaji wa huduma kwa wateja unaoendana na mabadiliko hayo.

 “Lengo  letu ni kutafuta njia mbalimbali ambazo tunaweza kuzitumia ili kujenga ushirika na  kampuni za ubunifu zinazoibuka, katika kubuni bidhaa mbalimbali na kuziweka sokoni ili zizalishe kibiashara,” alisema Samuel Mkuyu, Mkuu wa Huduma kwa Wateja na Dijitali, akiongeza kuwa benki hiyo imekuwa kwa muda mrefu inazitafuta kampuni  zinazoibuka.

Alisema kuwa kutokana na jinsi kampuni  zilizoshiriki kwenye  warsha hiyo zilivyowasilisha taarifa za miradi mbalimbali ya biashara waliyobuni , benki hiyo itachambua shughuli za kampuni hizo kwa lengo la kubaini  fursa na mawazo ambayo  yanaweza kugeuzwa bidhaa na huduma kwa njia ya  ubia na benki hiyo.

 “Lengo letu si tu kuzimwagia fedha kampuni hizo zinazoibuka na zinazoendesha miradi ya ubunifu ya kibiashara, msingi wa ubia ambao tunalenga kuujenga ni kugeuza mawazo ya kampuni hizo kuwa miradi ya kibiashara inayozaa faida ambapo sote tutanufaika,”  alisema Mkuyu,  na kutoa mfano wa programu iliyozinduliwa hivi karibuni na benki hiyo inayomuwezesha mteja  kupanga miadi  mtandaoni ( Virtual Branch Engagement Solution), kwamba ni  ushirika kati ya Absa na kampuni ya FastHub.

Mkuyu alisema kuwa Absa ina nia thabiti ya kuweka kipaumbele katika miradi ya ubunifu wa kidijitali  yenye uwezo wa kuzalisha masuluhisho endelevu ya kidijitali,  huku thamani ya mteja ikiwekwa mbele tofauti na miradi mingine ambapo haigusi  Mtindo wa Maisha wa mteja. Msimamo huu wa benki, alisema, unadhihirishwa na kutambuliwa kwake hivi karibuni kwa benki hiyo kushinda Tuzo ya  Taasisi bora ya Fedha kwenye matumizi ya Tehama wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), uliofanyika jijini Arusha.

Lengo kuu la  warsha hiyo, ambayo iliendana na  mjadala ulioshirikisha watoa mada  wabobezi kutoka kampuni mbalimbali, ilikuwa ni kujadili changamoto zinazokabili harakati za kuboresha huduma  kwa wateja  katika sekta mbalimbali  na namna  gani ubunifu wa kidijitali unaweza ukatatua mapungufu katika  mikakati hiyo.

Akiongea katika warsha hiyo, Msimamizi wa Hindsight Ventures Tanzania, Paul Mandele, alitoa mchango wake kuhusiana na namna warsha hiyo ilivyokuja  muda muafaka, ikizingatiwa kuwa warsha kama hizo ni muhimu kwa kuwa zinatoa fursa za kutatua changamoto ambazo zinafanya kampuni changa zishindwe kuboresha huduma kwa wateja kuendana na mabadiliko ya kidijitali kwa kasi ambayo wadau wa  sekta wanategemea.

Mandele aliongeza kuwa changamoto hizo kama hazitatatuliwa kwa sasa, zitafanya kampuni nyingi zinazoibuka  kushindwa kutekeleza miradi yake kama ambavyo imebainishwa kwenye dira zao ikizingatiwa kuwa wengi wa waanzilishi wa kampuni hizo ni wajasiriamali waliotoka vyuoni karibuni na wasiokuwa na mitaji, elimu  stahili ya biashara,  takwimu chache na kutokuwa na stadi maalum za biashara.

 “Kampuni nyingi zinazoibuka mara nyingi huwa zinakosa washirika wa kufanya nao kazi, jambo ambalo linazifanya zijiendeshe kwa kujitegemea zenyewe bila ya kuwa na kampuni kongwe kama mfano wa karibu wa kuigwa, “ Alisema Mandele.

Mkuu wa Huduma kwa Wateja na Digitali wa Benki ya Absa, Samuel Mkuyu (wa pili kulia), akichangia mada wakati wa warsha kuhusu uboreshaji wa huduma kwa wateja kwa kutumia njia za ubunifu wa kidigitali iliyoandaliwana kampuni ya teknolojia ya Hindsight Ventures kwa kushirikiana na Absa, jijini Dar esSalaam leo. Wanaongalia kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa echo Tanzania, Aashiq Shariff, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kifedha kwa Njia ya Simu za Mkononi wa Tigo, Faith Pella na Ofisa Mtendaji Mkuu na Mwanzilishi wa Kampuni ya Hindsight, Ajay Ramasubramaniam.

Mkuu wa Huduma kwa Wateja na Digitali wa Benki ya Absa, Samuel Mkuyu (mbele), pamoja na washikiri wengine katika warsha kuhusu uboreshaji wa huduma kwa wateja kwa kutumia njia za ubunifu wa kidigitali iliyoandaliwana kampuni ya teknolojia ya Hindsight Ventures kwa kushirikiana na Absa, jijini Dar esSalaam leo.

Ofisa Mtendaji Mkuu na Mwanzilishi wa Kampuni ya Hindsight Venture, Ajay Ramasubramaniam akizungumza katika hafla hiyo jijini Dar es Salaam leo.

Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Hindsight Venture wakipiga picha ya kumbukumbu mara baada ya kumalizika kwa warsha hiyo jijini Dar es Salaam leo.

Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya Absa Tanzania wakipozi mbele ya wapiga picha mara baada ya kumalizika kwa warsha hiyo jijini Dar es Salaam leo.

Baadhi ya washiriki katika warsha hiyo wakisikiliza mada mbalimbali kutoka kwa watoa mada katika hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Seedspace katika Jengo la Tanzanite Tower jijini Dar es Salaam leo.  

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...