KATIKA karne ya 21 ambayo dunia inashuhudia mabadilko makubwa na yenye kasi katika mambo mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na kwa kiwango cha pekee mabadiliko ya teknolojia, hakuna wakati sahihi kuliko sasa wa kufanya jitihada za kuziba pengo la uhaba wa wanawake katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano (tehama).

Ni ukweli kwamba mafanikio ya shughuli yoyote ya maendeleo yanahitaji si tu jitihada za pamoja lakini pia mipango muhimu kwa pande zote zinazohusika.

Endapo mtu ataamua kuangalia kwa kina masuala mbalimbali ambayo yanachukuliwa na dunia ya leo kama alama halisi ya mafanikio, basi atatambua kwamba mafanikio yake yalitokana, na pia ni matokeo ya juhudi za pamoja kati ya wanawake na wanaume.

Hii inatupeleka kwenye msemo maarufu kwamba 'nyuma ya kila mafanikio ya mwanamume kuna mwanamke.' Katika muktadha huo ni sahihi pia kusema mafanikio ya sekta ya tehama yanahitaji mchango mkubwa wa wanawake.

Katika kipindi hiki ambacho nchi zinazoendelea zinajitahidi kukabiliana na mabadiliko ya haraka yaliyoletwa na Mapinduzi ya Nne ya Viwanda ni muhimu sana kukawa na jitihada jumuishi katika kufikia malengo yaliyowekwa na kwa Tanzania, kwa mfano, ni kufikia malengo ya uchumi wa kidijiti.

Kiongozi wa zamani wa China na baba wa Taifa hilo, Mao Zedong, aliwahi kusema: ‘Wanawake wanashikilia nusu ya anga’. Msemo huo, ni uthibitisho na kielelezo hai cha jukumu la wanawake katika jamii kwenye kuhamasisha maendeleo ya kila kitu kinachomzunguka binadamu, kuanzia ngazi ya familia, jamii, taifa na hata dunia kwa ujumla.

Wanawake ni nusu ya idadi ya watu duniani, na kwa hivyo, ni sehemu muhimu ya maendeleo ya nchi na dunia. Katika Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, lengo namba tano linaeleza umuhimuwa dunia kufikia usawa wa kijinsia kwa kuwawezesha wanawake na wasichana.

Utambuzi na uwekwaji wa lengo hili kama sehemu ya mambo machache ambayo dunia imejidhatiti kuyafanikisha ni kielelezo cha jitihada za uhitaji wa dunia kupiga hatua mbele pasi kumuacha mtu nyuma.

Ni wazi kuwa mafanikio yanayoonekana katika sekta nyingine yalipatikana kupitia ushiriki mzuri wa wanawake, na katika muktadha huo ni matokeo hayo mazuri yaliyotokana na ushiriki wa wanawake ndiyo yanayotufanya tuamini kuwa ni kupitia kuwekeza kwa wasichana katika teknolojia ya habari na mawasiliano tunaweza kufikia uchumi wa kidijiti.

Nchini Tanzania, tehama kwa kiasi kikubwa imetawaliwa na wanaume. Tunapoangalia shule, taasisi za elimu ya juu na hata katika ajira wanawake ni sehemu ndogo ya kundi katika maeneno hayo.

Kwa mujibu wa takwimu za serikali zilizopo, wanawake walioajiriwa katika tehama si zaidi asilimia 25. Hii inaweza kuchangiwa na ukweli kwamba masomo ya sayansi yalionekana kuwa yanafaa kwa wanaume na si wanawake, lakini enzi zimebadilika.

Nchi inahitaji wanawake wengi katika tehama pengine wakati huu kuliko wakati mwingine wowote ili kufikia malengo iliyojiwekea.

Vikwazo kwa wanawake kushiriki katika sekta ya tehama ni lazima kuvunjwa. Hii inahitaji kuanza katika ngazi ya chini, kupitia elimu na mafunzo kwa kuwapa wasichana na wanawake wadogo fursa na ujuzi wa kuingia ulimwengu wa teknolojia. Hii haitatokea usiku mmoja, hivyo zinahitajika jitahada za makusudi.

Upungufu wa wanawake katika sekta ya tehama kwa kiasi kikubwa unadhoofisha jitihada za jamii na taifa kupiga hatua na kusonga mbele.

Pamoja na hayo, inaleta matumaini kuona kwamba serikali na wadau wengine wa tehama na wasio wa tehama wamekuja na mipango ya kuwekeza kwa wasichana katika eneo hili kwa sababu kupitia hatua hiyo tunaweza kupata vipaji thabiti katika sekta hii siku za usoni.

Kwa kutaja mifano michache, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kujenga shule moja ya sayansi kwa wasichana katika kila mkoa. Mpango huu kwa kiasi kikubwa utahamasisha wasichana wadogo kupiga hatua na kunyakua fursa ambazo hazifiki kwao kutokana na muundo wa imani, mtazamo na tamaduni za jamii.

Pamoja na jitihada hizo za serikali, bado juhudi zaidi zinahitajika kutoka kwa wadau wengine hasa katika kuwekeza katika kuwawezesha watoto wa kike katika kuwapatia maarifa na ujuzi husika utakaowawezesha kuwa mstari wa mbele kama kiungo muhimu katika maendeleo ya sekta za tehama.

Tunahitaji shule zaidi, vyuo zaidi, na programu zaidi ambazo zinatoa fursa zaidi kwa wasichana katika tehama. Nchini Tanzania kumekuwa na programu kadhaa za tehama ambazo zinawapa wanawake nafasi ya kujifunza na kujipambanua katika tehama. Programu hizi zinafanywa na wadau wa tehama. Na inafaa kutaja wachache ili wengine waweze kuchochewa na kuanzisha programu kama hizo.

Wadau hawa ni pamoja na Kampuni ya Huawei Technologies, kupitia ushirikiano wake na taasisi za elimu ya juu imepanga kutoa mafunzo kwa wasichana zaidi katika tehama kupitia mpango wake wa utunzaji na ukuzaji wa vipaji unaojulikana kama Huawei ICT Academy.

Mipango ya namna hii ni ya kupongezwa sana kwani inagusa moja kwa moja mustakabali wa Tanzania katika eneo la tehama.

Kupitia program hii inaonekana wazi kuwa Huawei imejidhatiti kuunga mkono jitihada za serikali, jumuiya ya kimataifa pamoja na wadau wengine katika kukomesha upungufu wa wanawake katika tehama.

Lengo la Huawei ni katika kuhamasisha kizazi kipya cha wanawake kujifunza teknolojia ya habari na mawasliano na kufanya kazi katika eneo hilo na hivyo hili linapaswa kuungwa mkono ili ikiwezekana kuwa na programu za namna hii nyingi zaidi.

Ni wazi kuwa uwepo wa msururu wa programu hizi nchi kutaifanya Tanzania kupaa katika sekta ya tehama kwani taifa litakuwa na rasilimali watu ya kutosha yenye ujuzi na uwezo unaohitajika katika kusongesha mbele ajenda ya uchumi wa kidijiti.

Sasa ni wakati mwafaka kwa serikali na wadau wengine wa tehama kuwekeza zaidi kwa wasichana kwa sababu wana uwezo unaotakiwa ili kuisogeza mbele nchi. Ni muhimu wasichana wote nchini wachangamkie fursa zinazotolewa kwao hasa zile zinazohusu tehama na kuzitumia vyema kwa ajili ya uboreshaji wa nchi.

Chuo kikuu cha sayansi na teknolojia Mbeya (MUST) kimekuwa moja ya vyuo vya kwanza Tanzania kuingiza kozi ya tehama ya Datacom ambayo inatolewa na Huawei kwenye mitaala miwili ya shahada za tehama (Bachelor of Computer Science and Bachelor of Information and Communication Technology).

Pamoja ni hilo, Must imekuwa ikihakikisha wasichana wengi wanajihusisha na teknolojia za tehama na kujiunga na kozi mbalimbali za eneo hilo zinazotolewa na Huawei kupitia program yake ya Huawei ICT Academy.

Kwa kupitia programu ya Seeds for the Future, mwaka 2021 wanafunzi wa kike sita na mwaka 2022 wanafunzi watano wasichana wameshiriki kikamilifu katika kujifunza teknolojia mpya kama 5G, Cloud Computing, AI na Blockchain na IoT.

Sambamba na hilo, chuo kikuu cha sayansi na teknolojia Mbeya (MUST) kwa kupitia mitaala ya shahada za tehama, wanafunzi 27 wasichana walifundishwa somo la wasichana (Computer network) kwa mwaka wa masomo 2021/2022.

Mwezi June na Agosti mwaka huu (2022) madarasa mawili ya tehama (Must Datacom na DataCom Must) yalifunguliwa kupitia tovuti ya Huawei kwenye program ya Huawei ICT Academy ambapo wasichana 12 walihudhuria mafunzo hayo yaliyokuwa yanatolewa kwa njia ya mtandao.



Katika kuhakikisha wasichana wengi wanaendelea kujifunza na kushiriki mafunzo ya tehama, Klabu ya Huawei imeanzishwa chuoni na ikisimamiwa na Bi Scholastica Milanzi, mwanafunzi wa tehama.


Tunategemea kuwa hawa wasichana waliopitia katika programu mbalimbali za Huawei watakuwa mabalozi wazuri kwa wasichana wengine ndani na nje ya chuo ili kupenda kusoma tehama na kujihusisha na masomo ya sayansi.

Imeandaliwa na:

Justin Alipoki Mwakatobe,

Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...